Hofu Inayofaa na Isiyofaa
Hofu Inayofaa na Isiyofaa
KWA kawaida, neno hofu humaanisha kutazamia jambo baya au maumivu, kwa ujumla maumivu ya kihisia moyo yanayoletwa na kushtuka, kuogopa, au kufadhaika. Hata hivyo, hofu yaweza kumaanisha pia kutambua au kufikiria kitu ambacho kinaweza kujeruhi au kuharibu. Utambuzi huo humfanya mtu kuwa mwangalifu na mwenye busara.
Biblia huonyesha kwamba kuna hofu inayofaa na isiyofaa. Hofu inayofaa humwezesha mtu kuwa mwangalifu anapokabiliana na hatari, na hivyo kuepuka msiba, nayo hofu isiyofaa, huvunja matumaini na kudhoofisha mfumo wa neva hata kusababisha kifo.
Katika Mwanzo 9:2, neno ‘hofu’ linatumiwa kuhusiana na wanyama. Mungu alimwambia Noa na wanawe: “Kila mnyama wa katika nchi atawaogopa ninyi na kuwahofu.” Katika mwaka ambao Noa na familia yake walikuwa ndani ya safina, wanyama na ndege waliokuwa humo waliwahofu na hiyo ilisaidia kuwadhibiti. Vivyohivyo, walipotoka ndani ya safina baada ya Furiko, Yehova alimhakikishia Noa kwamba hofu hiyo ingeendelea. Jambo hilo linaungwa mkono na mambo ambayo wanadamu wameshuhudia. Dakt. George G. Goodwin, Afisa Msaidizi wa Jumba la Makumbusho la Marekani la Historia ya Asili alisema: “Kwa kawaida chui hashambulii wanadamu. Hata hivyo, wakimchokoza au kumjeruhi atawashambulia.” Vivyo hivyo, nyoka wenye sumu walio wakali kama vile songwe na fira, kwa kawaida hunyiririka polepole kuwahepa wanadamu badala ya kuwashambulia. Ijapokuwa mwanadamu amewatendea vibaya wanyama na kuwafanya wengine kuwa wakali, bado wanyama wanahofu mwanadamu na hivyo anaweza kuwadhibiti. Haya yanalingana na maneno ya Mungu katika Mwanzo 1:26-28, kwamba wanyama walipaswa kujitiisha chini ya mwanadamu tangu uumbaji.
Kumhofu Mungu kunafaa. Kwamaanisha kumwonyesha Muumba kicho na heshima pamoja na woga ufaao wa kutompendeza. Tunahofu kumchukiza Yehova kwa sababu tunathamini fadhili-upendo zake zisizostahiliwa na uzuri wake na kutambua kwamba yeye ni Hakimu Mkuu na Mungu Mweza Yote, aliye na uwezo wa kuwaadhibu au hata kuwaua wale wasiomtii.
Hofu ifaayo kwa Yehova Mungu ni muhimu kwa wale wanaotaka kumtumikia. Hofu hiyo yenye kina kwa Yehova ndiyo “mwanzo wa hekima.” (Zaburi 111:10; Mithali 9:10) Hofu ya aina hiyo siyo ile isiyofaa inayovunja moyo bali, ni ‘kicho cha BWANA ambacho ni kitakatifu.’ (Zaburi 19:9) Hofu hiyo imefafanuliwa hivi katika Mithali 8:13: “Kumcha [“kumhofu,” NW] BWANA ni kuchukia uovu.” Hofu hiyo itamfanya mtu aepuke mwendo mbaya, kwa sababu, “kwa kumcha [“kumhofu,” NW] BWANA watu hujiepusha na maovu.”—Mithali 16:6.
Kwa kutokuonyesha hofu ifaayo Adamu na Hawa walikosa kumtii Mungu. Hiyo ikatokeza ndani yao hofu mbaya yenye kutisha, iliyowafanya wajifiche kutoka mbele za Mungu. “Nalisikia sauti yako bustanini, nikaogopa,” Adamu akasema. (Mwanzo 3:10) Kaini mwana wa Adamu alikuwa na hofu ya namna hiyo pia baada ya kumwua Abeli nduguye, na huenda hofu hiyo ndiyo iliyomfanya aamue kujenga jiji.—Mwanzo 4:13-17.
Andiko la Waebrania 12:28 linaagiza Wakristo kuwa na hofu ya kimungu linaposema: “Acheni sisi tuendelee kuwa na fadhili isiyostahiliwa, ambayo kupitia hiyo twaweza kumtolea Mungu katika njia ya kukubalika utumishi mtakatifu kwa hofu ya kimungu na kicho.” Malaika katika mbingu ya kati aliye na habari njema idumuyo milele ili kuitangaza, alianza tangazo lake kwa maneno haya: “Hofuni Mungu na kumpa utukufu.” (Ufunuo 14:6, 7) Yesu alionyesha tofauti iliyopo kati ya kumhofu Mungu na kuhofu wanadamu aliposema hivi kwenye Mathayo 10:28: “Na msiwe wenye kuwahofu wale wauuao mwili lakini hawawezi kuiua nafsi; lakini badala ya hivyo mhofuni yeye awezaye kuangamiza vyote viwili nafsi na mwili katika Gehena.” Aliwashauri Wakristo hivi pia kwenye Ufunuo 2:10: ‘Msiogope mambo mliyo karibu kuteseka.’ Upendo halisi kwa Yehova huondolea mbali hofu isiyofaa ambayo inaweza kumfanya mtu aache imani yake.
Hata hivyo, hofu ifaayo hutia ndani kuheshimu mamlaka ya kilimwengu kwa sababu Wakristo wanajua kwamba adhabu ya haki kutoka kwa mamlaka kwa sababu ya tendo la uhalifu ni wonyesho usio wa moja kwa moja wa hasira ya Mungu.—Waroma 13:3-7.
Yesu alitabiri kwamba katika “umalizio wa mfumo wa mambo” kungekuwa na hofu nyingi duniani. Alisema kwamba kungekuwa na “mambo ya kuonwa yenye kutia hofu” na kwamba watu ‘watazimia moyo kutokana na hofu na tarajio la mambo yanayokuja juu ya dunia inayokaliwa.’ (Luka 21:11, 26) Ijapokuwa kwa ujumla watu wangeathiriwa kwa njia hii, watumishi wa Mungu wanapaswa kufuata kanuni inayoonyeshwa kwenye Isaya 8:12: “Msihofu kwa hofu yao.” Mtume Paulo aeleza: “Kwa maana Mungu alitupa sisi si roho ya woga, bali ile ya nguvu na ya upendo na ya utimamu wa akili.” —2 Timotheo 1:7.
Baada ya kuchunguza kwa makini binadamu na kazi zake na taabu zake, mwanamume mwenye hekima alisema: “Hii ndiyo jumla ya maneno; yote yamekwisha sikiwa; mche [“mhofu,” NW] Mungu, nawe uzishike amri zake, maana kwa jumla ndiyo impasayo mtu.”—Mhubiri 12:13.