Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kanisa na Serikali Huko Byzantium

Kanisa na Serikali Huko Byzantium

Kanisa na Serikali Huko Byzantium

MWANZILISHI wa Ukristo alionyesha wazi tofauti inayopaswa kuwepo kati ya wafuasi wake na ulimwengu wa wanadamu waliotengwa na Mungu. Yesu aliwaambia wafuasi wake: “Kama mngekuwa sehemu ya ulimwengu, ulimwengu ungependa kilicho chao wenyewe. Sasa kwa sababu nyinyi si sehemu ya ulimwengu, bali nimewachagua nyinyi kutoka ulimwenguni, kwa ajili ya hili ulimwengu huwachukia nyinyi.” (Yohana 15:19) Yesu alimwambia hivi Pilato, mwakilishi wa mamlaka ya kisiasa ya wakati wake: “Ufalme wangu si sehemu ya ulimwengu huu.”—Yohana 18:36.

Ili kutimiza wajibu wao wa kuhubiri “hadi sehemu ya mbali ya dunia,” Wakristo walipaswa kuepuka kukengeushwa fikira na mambo ya ulimwengu. (Matendo 1:8) Kama Yesu, Wakristo wa mapema hawangejihusisha na siasa. (Yohana 6:15) Ilikuwa wazi kwamba Wakristo waaminifu hawakujihusisha wala kuwa na vyeo katika usimamizi wa raia. Hata hivyo, mambo yalibadilika baadaye.

“Sehemu ya Ulimwengu”

Muda fulani baada ya mtume wa mwisho kufa, viongozi wa kidini walianza kubadili kimakusudi mtazamo wao kuhusu uhusiano wao na ulimwengu. Wakaanza kuwazia “ufalme” ambao haukuwa tu katika ulimwengu, bali uliokuwa sehemu yake pia. Tutaona hayo tuchunguzapo jinsi dini na siasa zilivyoungana katika Milki ya Byzantium—Ile Milki ya Roma Mashariki yenye mji mkuu huko Byzantium (sasa Istanbul).

Katika jumuiya ambayo kwa kawaida dini ilitimiza fungu kubwa, Kanisa la Byzantium ambalo makao yake makuu yalikuwa huko Byzantium, lilikuwa na uwezo mwingi sana. Mwanahistoria wa masuala ya kanisa, Panayotis Christou alisema: “Watu wa Byzantium waliona milki yao ya kidunia kuwa mfano wa Ufalme wa Mungu.” Hata hivyo, mamlaka ya kifalme hayakukubaliana na maoni hayo wakati wote. Kwa hivyo, wakati mwingine Kanisa na Serikali zilizozana. Kitabu, The Oxford Dictionary of Byzantium chasema: “Maaskofu wa Constantinople [au Byzantium] walikuwa na tabia mbalimbali, kutia ndani kujinyenyekeza kwa woga chini ya mtawala mwenye uwezo . . . , wakashirikiana kwa mafanikio na maliki . . . , na kupinga vikali maamuzi yake.”

Askofu mkuu wa Constantinople, aliye mkuu wa Kanisa la Mashariki, akawa mtu mashuhuri sana. Yeye ndiye aliyemtawaza maliki na kutazamia kwamba angekuwa mtetezi mwaminifu wa Kanisa Othodoksi. Alikuwa pia tajiri sana kwani alidhibiti mali nyingi za kanisa. Mamlaka yake ilitokana na uwezo aliokuwa nao juu ya watawa wengi wa kiume na vilevile uvutano aliokuwa nao juu ya watu wa kawaida.

Mara nyingi askofu mkuu angeweza kumpinga maliki. Angetisha kumtenga na kanisa—akifanya atakavyo katika jina la Mungu—au angeweza kutumia mbinu nyinginezo kumwondoa maliki mamlakani.

Kadiri usimamizi wa raia ulivyoendelea kuzorota hatua kwa hatua nje ya mji, ndivyo maaskofu walivyopata kuwa na uwezo mwingi katika majiji yao, kama ule wa magavana wa wilaya ambao wao walisaidia kuwateua. Maaskofu waliingilia kesi mahakamani na shughuli nyingine za kilimwengu wakati kanisa lilipohusishwa—hata wakati ambapo halikuhusishwa. Walikuwa na uwezo mwingi hivyo kwa sababu walisimamia maelfu ya makasisi na watawa wa kiume katika maeneo hayo.

Siasa na Usimoni

Kama inavyoonyeshwa, dini iliungana kabisa na siasa. Zaidi ya hayo, makasisi wengi walijihusisha na mambo ya kidini yaliyohitaji pesa nyingi. Wengi wa viongozi wa kidini wenye vyeo vya juu waliishi maisha ya anasa. Kadiri kanisa lilivyozidi kuwa na uwezo na mali, ndivyo hali ya umaskini na utakatifu wa kimitume ulivyotoweka. Baadhi ya makasisi na maaskofu walitoa rushwa ili wateuliwe. Usimoni ulikuwa jambo la kawaida hata kwa vikundi vya maaskofu wenye vyeo vya juu zaidi. Makasisi waliungwa mkono na vikundi vya washawishi wenye mali walipogombea vyeo vya kidini mbele ya maliki.

Rushwa ilitumiwa pia ili kuwashawishi viongozi wakuu wa kidini. Wakati Maliki wa kike Zoe (k. 978-1050 W.K.) alipoamuru mume wake, Romanus wa Tatu, auawe ili aolewe na mpenzi wake Michael wa Nne, ambaye sasa angekuwa Maliki, alimwita Askofu Mkuu Alexius mara moja kwenye makao ya kifalme. Akiwa huko, askofu mkuu huyo alijulishwa kuhusu kifo cha Romanus na kwamba alitarajiwa kusimamia sherehe za arusi. Kwa kuwa kanisa lilikuwa linasherehekea Ijumaa Kuu jioni hiyo, mambo hayakuwa rahisi kwa Alexius. Hata hivyo, alikubali zawadi nyingi alizopewa na maliki huyo wa kike na akatenda kulingana na ombi lake.

Kunyenyekea Chini ya Maliki

Katika historia ya Milki ya Byzantium, wakati mwingine maliki alitumia mamlaka yake ili kudhibiti uchaguzi wa askofu mkuu wa Constantinople. Katika pindi hizo, hakuna mtu angekuwa askofu mkuu au kushikilia cheo hicho kwa muda mrefu kinyume cha mapenzi ya maliki.

Maliki Andronicus wa Pili (1260-1332) alilazimika kuwabadilisha maaskofu wakuu mara tisa. Mara nyingi akikusudia kumteua askofu mkuu ambaye angeweza kushawishika kwa urahisi. Kulingana na kitabu The Byzantines, askofu mkuu mmoja hata alimwandikia maliki akimwahidi kwamba ‘atafanya lolote maliki aliloamuru, hata kama lingemaanisha kuvunja sheria, na kwamba angeepuka kufanya lolote kinyume cha mapenzi ya maliki.’ Mara mbili maliki walijaribu kulazimisha kanisa kufanya kulingana na mapenzi yao kwa kumteua mwana wa familia ya kifalme kuwa askofu mkuu. Maliki Romanus wa Kwanza alimfanya mwana wake Theophylact mwenye umri wa miaka 16 tu kuwa askofu mkuu.

Iwapo askofu mkuu hangetenda kulingana na mapenzi ya maliki, huenda maliki angemshurutisha ajiuzulu au kuagiza sinodi imwondoe katika cheo hicho. Kitabu Byzantium chasema: ‘Katika historia ya Byzantium, mamlaka ya juu na hata ushawishi wa moja kwa moja wa Maliki ulichangia sehemu muhimu katika uteuzi wa maaskofu.’

Maliki alisimamia pia mikutano ya kanisa akiwa pamoja na askofu mkuu. Aliongoza mijadala, akatunga vifungu vya imani, akabishana na maaskofu pamoja na wazushi wa kidini—ambao angeweza kuwahukumia kifo kwa kutundikwa mtini. Maliki pia aliidhinisha na kutekeleza sheria za kidini zilizokubaliwa katika mikutano hiyo. Alihukumu waliompinga si kwa sababu tu ya kukiuka mamlaka, bali pia kwa kuwa maadui wa kanisa na wa Mungu. Askofu mkuu mmoja wa karne ya sita alisema hivi: “Hakuna chochote kipaswacho kufanywa kinyume cha amri na mapenzi ya Maliki.” Maaskofu waliokuwa katika makao yake walikuwa wajanja, vigeugeu, na wenye kushawishika upesi wanapoahidiwa zawadi. Maaskofu hao waliiga Mkubwa wao kwa kutoteta pia.

Kwa mfano Waziri Mkuu Bardas alilipiza kisasi wakati Askofu Mkuu Ignatius (k. 799-878 W.K.) alipokataa kumpa sakramenti. Bardas alimsingizia Ignatius kwamba alihusika katika njama fulani na katika uasi. Askofu mkuu huyo alishikwa na kufukuzwa kutoka eneo hilo. Kisha waziri akamchagua Photius ambaye alikuwa tu mtu wa kawaida kuchukua mahali pake. Kwa muda wa siku sita Photius alipandishwa vyeo vyote vya kanisa, na hatimaye kufikia kuwa askofu mkuu. Je, Photius alistahili kuwa askofu mkuu? Yeye alisemwa kuwa mtu “mwenye tamaa mbaya ya makuu, kiburi kisicho na kifani, na ujuzi wa kisiasa uliozidi wa kawaida.”

Kuchanganya Imani na Siasa

Mara nyingi mabishano kati ya waumini wa asili na waasi yalifunika upinzani wa kisiasa, na maliki wengi walivutiwa na mambo ya kisiasa badala ya kuanzisha mafundisho mapya. Kwa kawaida, maliki alikuwa na haki ya kuanzisha mafundisho ya kidini na kuhakikisha kwamba kanisa lilitenda kulingana na mapenzi yake.

Kwa mfano Maliki Heraclius (575-641 W.K.) alijaribu sana kuondoa utengano uliosababishwa na mabishano kuhusu asili ya Kristo ambao ulitisha kuigawanya milki yake iliyokuwa imedhoofika sana. Alijaribu kutatua tatizo hilo kwa kuanzisha fundisho jipya lililoitwa Monothelitism. * Kisha ili kuhakikisha kwamba anaungwa mkono na majimbo yaliyo kusini mwa milki yake, Heraclius alimchagua Cyrus wa Phasis kuwa askofu mkuu wa Aleksandria ambaye alikubali fundisho hilo lililoungwa mkono na maliki. Mbali na kumfanya Cyrus kuwa askofu mkuu, maliki alimfanya pia kuwa gavana wa Misri akiwa na mamlaka juu ya watawala wenyeji. Kwa kutumia minyanyaso kidogo, Cyrus alifaulu kupata kibali cha wengi wa wafuasi wa kanisa la Misri.

Matokeo Mabaya

Matukio hayo yangewezaje kuthibitisha maneno na mtazamo wa Yesu katika sala aliposema kwamba wafuasi wake ‘hawangekuwa sehemu ya ulimwengu’?—Yohana 17:14-16.

Matokeo yalikuwa mabaya sana kwa viongozi waliodai kuwa Wakristo na wakati huohuo kujiingiza katika mambo ya kisiasa na ya kijeshi ya ulimwengu katika enzi za Byzantium na baadaye. Umejifunza nini kwa kuchunguza historia hii fupi? Je, viongozi wa Kanisa la Byzantium walipata kibali cha Mungu na cha Yesu Kristo?—Yakobo 4:4.

Viongozi wa kidini wenye pupa kama hao pamoja na makahaba wao wa kisiasa hawajawahi kutumikia Ukristo wa kweli. Muungano huo usio mtakatifu wa dini na siasa hauwakilishi dini ya kweli iliyofundishwa na Yesu. Na tujifunze kutokana na yaliyopita na tuendelee tukiwa “si sehemu ya ulimwengu.”

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 21 Fundisho la Monothelitism husema kwamba Kristo ajapokuwa na utu wa Mungu na wa kibinadamu, ana kusudi moja.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 10]

‘KAMA MUNGU ATEMBEAYE KATIKA MBINGU’

Matukio yanayomzunguka Askofu Mkuu Michael Cerularius (k. 1000-1059) yanaonyesha jinsi kiongozi wa kanisa angesukumwa na tamaa ya makuu na kuingilia mambo ya siasa. Baada ya kuwa askofu mkuu, Cerularius alitaka cheo cha juu hata zaidi. Alisemwa kuwa mtu mwenye kiburi, kimbelembele, na mshupavu—‘yaelekea tabia hii yake ilimfanya aonekane kama mungu atembeaye katika mbingu.’

Kwa sababu ya tamaa ya makuu, Cerularius alichochea mtengano wa papa wa Roma na Milki ya Byzantium katika mwaka wa 1054, na kumshurutisha maliki amwunge mkono. Akifurahia ushindi huo, Cerularius alipanga kumtawaza Michael wa Nne kuwa maliki na kumsaidia kuimarisha mamlaka yake. Mwaka mmoja baadaye, Cerularius alimwondoa huyo maliki na badala yake akamtawaza Isaac Comnenus (k. 1005-1061) achukue mahali pake.

Uhasama kati ya maaskofu na maliki uliendelea kuwa mbaya hata zaidi. Akiwa na uhakika kwamba ataungwa mkono na raia, Cerularius alitumia vitisho, nguvu na jeuri. Mwanahistoria wa wakati wake alisema: “Yeye alitabiri hadharani kuanguka kwa Maliki kwa kutumia matusi, akisema, ‘Nilikukweza, ewe punguani, lakini nitakuangamiza.’” Hata hivyo, Isaac Comnenus aliamuru akamatwe, afungwe na kupelekwa uhamishoni huko Imbros.

Mifano kama hii inaonyesha matatizo ambayo askofu mkuu wa Constantinople angesababisha na jinsi angempinga maliki kwa ujasiri. Mara nyingi ilimbidi maliki akabiliane na watu kama hao ambao walikuwa na ujuzi kisiasa, na wangeweza kukiuka amri ya maliki na ya kijeshi.

[Ramani/Picha katika ukurasa wa 9]

 

Maeneo Yote Chini ya Milki ya Byzantium

Ravenna

Roma

MAKEDONIA

Constantinople

Bahari Nyeusi

Nisea

Efeso

Antiokia

Yerusalemu

Aleksandria

Bahari ya Mediterania

[Hisani]

Ramani: Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.

[Picha katika ukurasa wa 10, 11]

Comnenus

Romanus wa Tatu (kushoto)

Michael wa Nne

Maliki wa kike Zoe

Romanus wa Kwanza (kushoto)

[Hisani]

Comnenus, Romanus wa Tatu, na Michael wa Nne: Courtesy Classical Numismatic Group, Inc.; Maliki wa kike Zoe: Hagia Sophia; Romanus wa Kwanza: Photo courtesy Harlan J. Berk, Ltd.

[Picha katika ukurasa wa 12]

Photius

[Picha katika ukurasa wa 12]

Heraclius na mwanaye

[Hisani]

Heraclius na mwanaye: Photo courtesy Harlan J. Berk, Ltd.; all design elements, pages 8-12: From the book L’Art Byzantin III Ravenne Et Pompose