Kuwa na Dhamiri Safi Kwahusisha Nini?
Kuwa na Dhamiri Safi Kwahusisha Nini?
“SERIKALI Imeamriwa Ipokee Dola 20,000 za Brazili.” Maneno haya yasiyo ya kawaida yalikuwa kichwa cha gazeti la karibuni la Brazili la Correio do Povo. Makala hiyo ilisimulia kisa cha Luiz Alvo de Araújo, mwanamume anayefanya kazi ya kupelekea watu barua huko Brazili, aliyeuzia serikali shamba lake. Baada ya kutia sahihi hati ya kuiuzia serikali shamba hilo, Luiz alishangaa kugundua kwamba alikuwa amelipwa dola 20,000 za Brazili (takriban dola 8,000 za Marekani) zaidi ya bei iliyokubaliwa!
Haikuwa rahisi kurudisha pesa hizo za ziada. Baada ya kwenda katika idara mbalimbali za serikali bila mafanikio, Luiz alishauriwa kutafuta wakili ili kutatua tatizo hilo kortini. “Yaelekea mtu fulani alikosea, na kwa sababu ya utaratibu tata uliofuatwa katika ununuzi huo, hakuna aliyejua jinsi ya kutatua tatizo hilo,” akasema hakimu aliyeamua kesi hiyo na kuiamrisha serikali ipokee pesa hizo na pia ilipie gharama ya kesi hiyo. “Sijawahi kushughulikia kesi nyingine kama hii.”
Luiz aliye mmoja wa Mashahidi wa Yehova, aeleza: “Dhamiri yangu iliyozoezwa na Biblia haingeniruhusu kuchukua kitu ambacho kwa hakika si changu. Ilinibidi nijitahidi kuzirudisha pesa hizo.”
Kwa wengi, hilo ni jambo lisilo la kawaida au hata lisilo la akili. Lakini Neno la Mungu huonyesha kwamba Wakristo wa kweli hujitahidi sana kudumisha dhamiri safi wanaposhughulika na serikali za ulimwengu. (Waroma 13:5) Mashahidi wa Yehova wameazimia kudumisha ‘dhamiri yenye kufuata haki, na kujiendesha wenyewe kwa kufuata haki katika mambo yote.’—Waebrania 13:18.