Ulimwengu Mzima Waharibiwa!
Ulimwengu Mzima Waharibiwa!
Unapotazama ulimwengu huu wenye majiji, utamaduni, mafanikio ya kisayansi, na mabilioni ya watu, ni rahisi kufikiri kwamba utadumu. Je, unafikiri kwamba siku moja ulimwengu huu unaweza kutoweka kabisa? Huenda ikawa vigumu kwako kuwazia jambo hilo. Hata hivyo, je unajua kwamba kulingana na chanzo chenye kutegemeka, kulikuwa na ulimwengu mwingine ambao uliharibiwa kabisa?
HATUZUNGUMZII ulimwengu wa makabila yasiyostaarabika. Ulimwengu ulioangamia ulikuwa umesitawi sana na ulikuwa na majiji, sanaa, na ujuzi wa kisayansi. Hata hivyo, rekodi ya Biblia hutuambia kwamba katika siku ya 17 ya mwezi wa 2, miaka 352 kabla ya kuzaliwa kwa mzee wa ukoo Abrahamu, gharika ilianza ghafula na kuangamiza ulimwengu mzima. *
Je, rekodi hiyo ni sahihi? Je, kweli gharika hiyo ilitokea? Je, kweli kulikuwa na ulimwengu wa kale kabla ya ulimwengu wa sasa ambao ulisitawi kisha ukaharibiwa? Ikiwa ndivyo, kwa nini uliharibiwa? Tatizo lilikuwa nini? Na tunaweza kujifunza chochote kutokana na kuharibiwa kwa ulimwengu huo?
Je, Kweli Kuna Ulimwengu wa Kale Ulioharibiwa?
Ikiwa kwa kweli msiba mkubwa kama huo ulitokea, basi haungeweza kusahaulika kamwe. Kwa hiyo, katika nchi nyingi kuna mambo yanayotukumbusha uharibifu huo. Kwa mfano, fikiria tarehe kamili iliyorekodiwa katika Maandiko. Mwezi wa pili wa kalenda ya kale ulianza katikati ya Oktoba na kumalizika katikati ya Novemba kulingana na kalenda ya siku hizi. Kwa hiyo siku ya 17 inakaribiana sana na siku ya kwanza ya mwezi wa Novemba. Hivyo, huenda haikutukia tu kwamba katika nchi nyingi watu hufanya sherehe kwa ajili ya wafu wakati huo wa mwaka.
Uthibitisho mwingine kwamba kulikuwa na Gharika wapatikana katika mapokeo ya wanadamu. Karibu watu wote wa kale wana hekaya zinazosema kwamba wazazi wao wa kale waliokoka furiko la ulimwenguni pote. Mbilikimo wa Afrika, Wainka wa Marekani, Waselti wa Ulaya—wote wana hekaya zinazofanana na za watu wa Alaska, Amerika Kaskazini, Australia, China, India, Lithuania, Mexico, Micronesia, na New Zealand, kwa kutaja nchi chache tu.
Bila shaka, kadiri wakati ulivyopita ndivyo hekaya hizo zilivyotiwa chumvi, lakini zote zina mambo kadhaa yanayoonyesha kwamba zilikuwa na chanzo kimoja: Mungu alichukizwa na uovu wa wanadamu. Akaleta furiko kubwa lililoangamiza wanadamu wote isipokuwa wachache tu waliokuwa waadilifu. Wanadamu hao waadilifu walijenga meli ambayo ilitumiwa kuwaokoa na kuokoa wanyama pia. Baadaye, ndege walitumwa kutafuta nchi kavu. Hatimaye meli ilitua juu ya mlima. Waliposhuka kutoka katika meli hiyo, waokokaji hao walitoa dhabihu.
Jambo hilo linathibitisha nini? Haiwezekani mambo hayo yanayofanana yawe yalitokea tu. Hekaya hizo zote zinathibitisha ushuhuda wa kale wa Biblia kwamba wanadamu wote ni wazao wa waokokaji wa furiko lililoangamiza wanadamu. Hivyo, hatuhitaji kutegemea hekaya au ngano kujua yaliyotokea. Tuna Maandiko ya Kiebrania ya Biblia yaliyohifadhiwa vizuri.—Mwanzo, sura ya 6-8.
Biblia ina historia iliyopuliziwa ambayo inataja jinsi uhai ulivyoanza. Hata hivyo, kuna uthibitisho unaoonyesha kwamba hiyo si historia tu. Unabii wake wenye kutegemeka na hekima yake nyingi huonyesha kwamba Biblia ni njia ya Mungu ya kuwasiliana na wanadamu. Tofauti na
ngano, Biblia inataja majina, tarehe, nasaba, na maeneo ya kijiografia katika masimulizi yake ya kihistoria. Inatueleza jinsi maisha yalivyokuwa kabla ya Furiko na kufunua ni kwa nini ulimwengu mzima ulifikia kikomo kwa ghafula.Ni nini kilichofanya watu hao walioishi kabla ya gharika waharibiwe? Makala inayofuata itajibu swali hilo. Hilo ni swali muhimu kwa wale ambao huenda wanataka kujua kama wakati ujao wa jamii ya leo ni salama.
[Maelezo ya Chini]
[Chati katika ukurasa wa 4]
Hekaya za Ulimwenguni Pote Kuhusu Lile Furiko
Nchi Waleta Habari 1 2 3 4 5 6 7 8 9 10
Ugiriki 7 ◆ ◆ ◆ ◆ ◆ ◆ ◆
Roma 6 ◆ ◆ ◆ ◆ ◆ ◆
Lithuania 6 ◆ ◆ ◆ ◆ ◆ ◆
Ashuru 9 ◆ ◆ ◆ ◆ ◆ ◆ ◆ ◆ ◆
Tanzania 7 ◆ ◆ ◆ ◆ ◆ ◆ ◆
India - Hindu 6 ◆ ◆ ◆ ◆ ◆ ◆
New Zealand - Maori 5 ◆ ◆ ◆ ◆ ◆
Micronesia 7 ◆ ◆ ◆ ◆ ◆ ◆ ◆
Washington Marekani - Yakima 7 ◆ ◆ ◆ ◆ ◆ ◆ ◆
Mississippi Marekani - Choctaw 7 ◆ ◆ ◆ ◆ ◆ ◆ ◆
Mexico - Michoacan 5 ◆ ◆ ◆ ◆ ◆
Amerika Kusini - Quechua 4 ◆ ◆ ◆ ◆
Bolivia - Chiriguano 5 ◆ ◆ ◆ ◆ ◆
Guyana - Arawak 6 ◆ ◆ ◆ ◆ ◆ ◆
1: Mungu akasirishwa na uovu
2: Uharibifu kupitia furiko
3: Kwa agizo la Mungu
4: Mungu atoa onyo
5: Wanadamu wachache waokoka
6: Waokolewa katika meli
7: Wanyama waokolewa
8: Ndege au kiumbe mwingine atumwa nje
9: Hatimaye meli yatua juu ya mlima
10: Dhabihu yatolewa