Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Inafaa Wakristo Kuhifadhi maiti kwa Kuipaka Dawa?

Je, Inafaa Wakristo Kuhifadhi maiti kwa Kuipaka Dawa?

Je, Inafaa Wakristo Kuhifadhi maiti kwa Kuipaka Dawa?

Mzee mwaminifu wa ukoo Yakobo alipokaribia kufa, alitoa ombi hili la mwisho: “Mnizike pamoja na baba zangu, katika pango iliyomo shambani mwa Efroni, Mhiti katika ile pango iliyomo shambani mwa Makpela, iliyo mbele ya Mamre katika nchi ya Kanaani.”—Mwanzo 49:29-31.

YOSEFU aliheshimu ombi la baba yake kwa kufuata desturi iliyoenea huko Misri wakati huo. Aliwaagiza “watumishi wake, waganga kwamba wampake babaye dawa asioze.” Kulingana na Mwanzo sura ya 50, waganga walichukua siku 40 kuitayarisha maiti kama ilivyokuwa desturi. Kupakwa dawa kwa maiti ya Yakobo kuliwezesha msafara mkubwa wa familia yake pamoja na watu mashuhuri kutoka Misri kusafiri mwendo wa kilometa 400 kupeleka maiti hiyo kuizika huko Hebroni.—Mwanzo 50:1-14.

Je, inawezekana kwamba siku moja mwili wa Yakobo uliopakwa dawa utapatikana? Uwezekano wa kupatikana kwa mwili huo ukiwa katika hali nzuri ni mdogo sana. Jambo linalofanya vitu vingi vya kale visipatikane katika Israeli ni kwamba eneo hilo lina maji mengi. (Kutoka 3:8) Vifaa vya chuma na mawe vinapatikana kwa wingi, lakini vingine vilivyo hafifu kama nguo, ngozi, na miili iliyopakwa dawa vimeharibiwa na unyevunyevu na mabadiliko ya muda mrefu.

Kuhifadhi maiti kwa kuipaka dawa kwahusisha nini? Kwa nini watu wamekuwa wakifanya hivyo? Je, jambo hilo linafaa kwa Wakristo?

Desturi Hiyo Ilianzia Wapi?

Kuhifadhi maiti kwa kuipaka dawa kwaweza kufafanuliwa kuwa njia ya kuzuia maiti ya mwanadamu au mnyama isioze. Wanahistoria waelekea kukubali kwamba kuhifadhi maiti kwa kuipaka dawa kulianza huko Misri lakini Waashuru, Waajemi, na Wasikithe walikuwa na zoea hilo pia. Huenda majaribio ya mapema ya kuhifadhi maiti kwa kuipaka dawa yalisababishwa na kupatikana kwa miili iliyokuwa imezikwa katika mchanga wa jangwani na kuhifadhiwa kiasili. Kuzika kwa aina hiyo kungezuia unyevunyevu na hewa kufikia maiti na hivyo kuizuia isioze. Watu fulani wanadhani kwamba desturi hiyo ilianza wakati miili ilipopatikana ikiwa imehifadhiwa ndani ya magadi, ambayo ni aina ya chumvi inayopatikana kwa wingi nchini Misri na maeneo yanayoizunguka.

Kusudi la kuhifadhi maiti ni kuzuia utendaji wa kawaida wa bakteria unaoanza muda mfupi tu baada ya kifo, ambao hufanya mwili uoze. Iwapo hali hii itazuiwa, mwili utaacha kuoza au hautaoza upesi. Kuna mambo matatu muhimu yanayohitaji kufanywa: Kuhifadhi mwili kama ulivyokuwa ukiwa hai, kuuzuia usioze, na kuzuia wadudu wasiushambulie.

Wamisri wa kale walihifadhi wafu hasa kwa sababu za kidini. Dhana yao ya uhai baada ya kifo ilihusiana na tamaa ya wafu kuendelea kuwasiliana na walio hai. Waliamini kwamba miili yao ingeendelea kutumiwa kwa umilele na kwamba ingerudishiwa uhai tena. Ijapokuwa desturi ya kuhifadhi maiti ilikuwa ya kawaida, kufikia sasa hakuna habari yoyote ambayo imepatikana kuhusu jinsi Wamisri walivyohifadhi maiti. Habari iliyo bora inayopatikana ni ile ya Herodoto, mwanahistoria Mgiriki wa karne ya tano K.W.K. Hata hivyo, imeripotiwa kwamba kujaribu kuhifadhi maiti kwa kufuata mielekezo iliyotolewa na Herodoto hakujafanikiwa sana.

Je, Inafaa kwa Wakristo?

Mwili wa Yakobo ulipakwa dawa na watu ambao imani yao ilikuwa tofauti na yake. Hata hivyo hatuwezi kuwazia Yosefu akiwapa waganga mwili wa babaye, na kutaka watoe sala na kufuata desturi zilizoambatana na kupaka maiti dawa huko Misri wakati huo. Yakobo na Yosefu walikuwa wanaume wenye imani. (Waebrania 11:21, 22) Maandiko hayashutumu kuhifadhiwa kwa mwili wa Yakobo kwa kupakwa dawa ingawa Yehova hakuagiza jambo hilo lifanywe. Kupakwa dawa kwa mwili wa Yakobo ili kuuhifadhi hakukukusudiwa kuwe kielelezo kwa taifa la Israeli au kwa kutaniko la Kikristo. Kwa hivyo, hakuna maagizo hususa kuhusu jambo hilo katika Neno la Mungu. Baada ya mwili wa Yosefu kuhifadhiwa kwa kupakwa dawa huko Misri, desturi hiyo haitajwi tena katika Maandiko.—Mwanzo 50:26.

Maiti zilizooza ambazo zilipatikana makaburini huko Palestina zaonyesha kwamba haikuwa desturi ya Wayahudi kupaka wafu dawa ili wasioze, au kuwahifadhi kwa muda mrefu. Kwa mfano, mwili wa Lazaro hakupakwa dawa ili usioze. Ijapokuwa alikuwa amefungwa nguo, watazamaji walikuwa na wasiwasi wakati jiwe lililofunika kaburi lake lilipokuwa likiondolewa. Kwa sababu Lazaro alikuwa amekufa siku nne mapema, dada yake alikuwa na hakika kwamba kungekuwa na uvundo wakati kaburi lingefunguliwa.—Yohana 11:38-44.

Je, mwili wa Yesu ulipakwa dawa ili usioze? Vitabu vya Injili haviungi mkono maoni hayo. Wakati huo, ilikuwa ni desturi ya Kiyahudi kuutayarisha mwili kwa viungo na mafuta yenye manukato kabla ya kuuzika. Kwa mfano, ili kuutayarisha mwili wa Yesu, Nikodemo alitoa kiasi kikubwa cha viungo kwa kusudi hilo. (Yohana 19:38-42) Kwa nini alitoa viungo vingi hivyo? Huenda alionyesha ukarimu huo kwa kuchochewa na upendo wake wa kutoka moyoni pamoja na heshima yake kwa Yesu. Hatupaswi kufikiria kwamba matumizi ya viungo hivyo yalikusudiwa kuuhifadhi mwili.

Je, Mkristo aweza kupinga desturi ya kupaka maiti dawa ili isioze? Kwa hakika kupaka maiti dawa ni kuchelewesha tu jambo lisiloweza kuepukika. Tulitoka mavumbini, na tukifa tunarudi mavumbini. (Mwanzo 3:19) Lakini itachukua muda gani kabla ya mfu kuzikwa? Ikiwa washiriki wa familia na marafiki wanatoka mbali na wanatamani kuuona mwili, bila shaka utahitaji kuhifadhiwa kwa kupakwa dawa ili usioze.

Kulingana na Maandiko hatuna sababu ya kuhangaika, iwapo mamlaka ya kwetu inaamuru au washiriki wa familia wanataka mwili uhifadhiwe kwa kupakwa dawa. Wafu “hawajui neno lolote.” (Mhubiri 9:5) Iwapo wako katika kumbukumbu la Mungu, watafufuliwa waishi katika ulimwengu wake mpya alioahidi.—Ayubu 14:13-15; Matendo 24:15; 2 Petro 3:13.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 31]

KUPAKA MAITI DAWA—WAKATI ULIOPITA NA SASA

Katika Misri ya kale njia ambayo ilitumiwa kupaka maiti dawa ili isioze ilitegemea hali ya familia. Yaelekea familia yenye utajiri ingefuata utaratibu huu:

Ubongo ungetolewa kwenye fuvu kupitia mianzi ya pua kwa kutumia kifaa cha chuma. Baada ya hilo, fuvu lingepakwa dawa. Jambo lililofuata lilitia ndani kuondoa viungo vyote vilivyo ndani ya mwili isipokuwa moyo na figo. Kufikia viungo vilivyo ndani ya tumbo, mwili ulihitaji kupasuliwa, lakini jambo hilo lilionwa kuwa dhambi. Ili kuepuka jambo hilo lenye ubishi, Wamisri waliopaka maiti dawa walimchagua mtu waliyemwita mkataji ili kufanya upasuaji huo. Mara tu alipopasua maiti, alitoroka ili kuepuka kuadhibiwa kwa kulaaniwa na kupigwa kwa mawe kwa sababu ya upasuaji huo ulioitwa eti uhalifu.

Baada ya matumbo kuondolewa, tumbo lilioshwa kabisa. Mwanahistoria Herodoto aliandika: “Walijaza tumbo kwa vipande vya manemane safi pamoja na mdalasini na viungo vya aina nyingine mbalimbali isipokuwa uvumba, kisha walishona mahali palipopasuliwa.”

Baadaye, mwili ulikaushwa kwa kuwekwa ndani ya magadi kwa siku 70. Kisha maiti hiyo ilioshwa kwa ustadi na kufungwa kwa kitani. Halafu kitani hicho kilifunikwa kwa utomvu wa aina fulani uliotumika kama gundi, kisha mummy (maiti iliyopakwa dawa) iliwekwa kwenye sanduku la mbao lililorembwa sana na lililokuwa na umbo la binadamu.

Siku hizi kupaka maiti dawa ili isioze kwaweza kufanywa kwa muda mfupi sana. Kwa kawaida maiti huhifadhiwa kwa kuweka kiasi kinachofaa cha umaji-maji wenye dawa ya kuhifadhi maiti kwenye mishipa ya damu na katika tumbo na kifua. Michanganyiko mbalimbali imetengenezwa na kutumiwa kwa miaka mingi. Hata hivyo, kwa sababu ya gharama na usalama, mchanganyiko uitwao fomaldehidi ndio unaotumiwa sana kuhifadhi maiti.

[Picha]

Jeneza la dhahabu la Mfalme Tutankhamen