Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Wawaldo Waacha Uzushi na Kuwa Waprotestanti

Wawaldo Waacha Uzushi na Kuwa Waprotestanti

Wawaldo Waacha Uzushi na Kuwa Waprotestanti

Ulikuwa mwaka wa 1545 huko Lubéron, eneo maridadi la Provence, kusini mwa Ufaransa. Wanajeshi walikusanyika ili kufanya mashambulizi makali yaliyochochewa na watu wasiovumilia dini. Mashambulizi hayo yalisababisha umwagaji wa damu ulioendelea kwa muda wa juma moja.

VIJIJI vikateketezwa, wakazi wakatiwa gerezani au kuuawa. Wanajeshi wakatili walihusika katika mauaji ya kinyama yaliyotetemesha Ulaya. Mbali na mateso yaliyowapata wanawake na watoto, wanaume 2,700 waliuawa, 600 wakapelekwa kupiga-makasia kwenye manchani. Jemedari wa kijeshi aliyesimamia kampeni hiyo ya umwagaji damu alisifiwa sana na Mfalme wa Ufaransa pamoja na papa.

Marekebisho Makubwa ya Kidini tayari yalikuwa yameigawanya Ujerumani wakati Mfalme Mkatoliki Francis wa Kwanza wa Ufaransa, aliyekuwa na wasiwasi kuhusu kuenea kwa Uprotestanti, alipofanya uchunguzi wa walioitwa eti wazushi wa kidini katika ufalme wake. Badala ya visa vichache vya hapa na pale vya uasi, wenye mamlaka katika Provence waligundua vijiji vizima-vizima vya wapinzani wa kidini. Tangazo likatolewa la kuangamiza uasi na hatimaye likatekelezwa kwenye yale mauaji ya mwaka wa 1545.

Wazushi hawa wa kidini walikuwa nani? Na kwa nini walitendewa jeuri na watu wasiovumilia dini?

Waacha Utajiri na Kuwa Maskini

Waliouawa katika mauaji hayo makubwa walikuwa wa kikundi cha kidini kilichoanzishwa huko nyuma katika karne ya 12 na kuenea katika sehemu kubwa ya Ulaya. Namna kikundi hicho kilivyoenea na kuendelea kwa karne nyingi ilikifanya kiwe cha kipekee katika historia ya wapinzani wa kidini. Wanahistoria wengi wanakubali kwamba kikundi hicho kilianza karibu mwaka wa 1170. Katika jiji la Lyons huko Ufaransa, mfanya-biashara tajiri aliyeitwa Vaudès alipendezwa sana kujua jinsi ya kumpendeza Mungu. Inaonekana alichochewa na shauri la Yesu kwa mtu fulani tajiri kwamba auze mali yake na kuwapa maskini. Kwa kufuata shauri hilo, Vaudès aliandalia familia yake kifedha kisha akaacha mali yake ili kuihubiri injili. (Mathayo 19:16-22) Punde si punde akawa na wafuasi waliokuja kuitwa Wawaldo. *

Vaudès alihangaikia zaidi Biblia, umaskini, na kuhubiri. Upinzani dhidi ya vyeo vya starehe vya kidini haukuwa jambo geni. Kwa muda fulani wapinzani wa vyeo vya kidini walikuwa wamepinga mazoea ya kanisa yenye ufisadi na matumizi mabaya ya mamlaka. Lakini Vaudès na wafuasi wake wengi walikuwa watu wa kawaida tu. Bila shaka hii inaonyesha sababu iliyomfanya aone uhitaji wa kuwa na Biblia katika lugha ya kienyeji. Kwa kuwa Biblia ya kanisa iliyokuwa tafsiri ya Kilatini ilitumiwa na makasisi peke yao, Vaudès aliagiza kutafsiriwa kwa Gospeli na vitabu vingine vya Biblia katika Kiprovençal, lugha iliyoeleweka na wenyeji wa mashariki ya kati ya Ufaransa. * Kwa kufuata amri ya Yesu ya kuhubiri, Maskini hao wa Lyons walihubiri ujumbe wao hadharani. (Mathayo 28:19, 20) Mwanahistoria Gabriel Audisio aeleza kwamba kusizitiza kwao kuhubiri hadharani kukawa suala la maana kuhusu maoni ya kanisa kuelekea Wawaldo.

Waacha Ukatoliki na Kuwa Wazushi

Katika siku hizo, kazi ya kuhubiri ilifanywa na makasisi tu, na kanisa ndilo lililokuwa na haki ya kutoa kibali cha kuhubiri. Makasisi waliwaona Wawaldo kuwa watu wasio na ujuzi na wasio na elimu, lakini katika mwaka wa 1179, Vaudès alitafuta kibali rasmi cha kuhubiri kutoka kwa Papa Alexander wa Tatu. Alikubaliwa kuhubiri iwapo tu makasisi wa kwao wangekubali. Mwanahistoria Malcolm Lambert asema kwamba hiyo “ilikuwa njia ya kumnyima kibali.” Kwa hakika, Askofu Mkuu Jean Bellesmains wa Lyons alitoa agizo rasmi kwamba watu wa kawaida wasihubiri. Vaudès alijitetea kwa kunukuu andiko la Matendo 5:29: “Lazima sisi tumtii Mungu kuwa mtawala kuliko wanadamu.” Kwa sababu Vaudès hakutii kizuizi hicho, alitengwa na ushirika wa kanisa mnamo mwaka wa 1184.

Ijapokuwa Wawaldo walifukuzwa kutoka dayosisi ya Lyons na kutoka jijini, yaelekea amri ya kutoruhusiwa kuhubiri haikuzingatiwa sana. Watu wengi wa kawaida walivutiwa na unyofu wa Wawaldo na njia yao ya maisha, hata maaskofu waliendelea kuzungumza nao.

Kulingana na mwanahistoria Euan Cameron, yaelekea wahubiri Wawaldo ‘walikuwa na sababu nzuri ya kupinga Kanisa Katoliki.’ “Walitaka tu kuhubiri na kufundisha.” Kulingana na wanahistoria, Wawaldo walikuja kuwa wazushi kwa sababu ya maagizo yaliyotolewa mfululizo ambayo hatua kwa hatua yalidhoofisha uwezo na uvutano wao. Shutuma za Kanisa zilifikia upeo wakati Baraza la Nne la Lateran lilipowapiga marufuku Wawaldo mnamo mwaka wa 1215. Jambo hilo liliathirije mahubiri yao?

Waendelea Kuhubiri Kisiri

Vaudès alikufa katika mwaka wa 1217, na kwa sababu ya minyanyaso, wafuasi wake wakatawanyika katika mabonde ya Alps ya Ufaransa, Ujerumani, Italia Kaskazini, Ulaya Mashariki na ya Kati. Minyanyaso pia iliwafanya Wawaldo waishi vijijini, jambo lililowazuia kuhubiri katika maeneo mengi.

Mnamo mwaka wa 1229 Kanisa Katoliki lilimaliza krusedi yao dhidi ya Wakathari, au Waalbi walioishi kusini ya Ufaransa. * Baadaye Wawaldo walianza kushambuliwa vikali na punde si punde Baraza la Kuhukumu Wazushi likaanza kuwashambulia kikatili wapinzani wote wa kanisa. Woga uliwafanya Wawaldo waendelee kuhubiri kisiri. Kufikia mwaka wa 1230 hawakuwa wanahubiri hadharani. Audisio aeleza: “Badala ya kutafuta wafuasi wapya . . . , walijitolea kuwalinda waumini wapya, kuwasaidia kudumisha imani yao kujapokuwa mikazo na minyanyaso kutoka nje.” Yeye aongezea kwamba “kuhubiri kuliendelea kuwa muhimu lakini njia ya kuhubiri ilikuwa imebadilika kabisa.”

Imani na Mazoea Yao

Kufikia karne ya 14 badala ya Wawaldo wote, yaani wanaume kwa wanawake kuhubiri, kukawa na vikundi viwili, wahubiri na waumini. Wanaume waliozoezwa vizuri pekee ndio walioshughulikia wajibu wa uchungaji. Wahudumu hao wenye kuzunguka baadaye walikuja kuitwa barbes (wajomba).

Wajomba hao walitembelea familia za Wawaldo nyumbani mwao, walijitahidi kukiimarisha kikundi chao badala ya kukipanua. Wajomba wote walijua kusoma na kuandika, na walipata mafunzo ya Biblia yaliyochukua miaka sita. Kutumia Biblia ya lugha ya kienyeji kuliwasaidia kuieleza kwa waumini wao. Hata wapinzani wakaja kukubali kwamba Wawaldo, kutia ndani watoto wao, waliijua Biblia vizuri na wangeweza kunukuu Maandiko mengi.

Baadhi ya mambo yaliyokataliwa na Wawaldo wa mapema yalikuwa, kusema uwongo, fundisho la purgatori, ibada ya wafu, msamaha wa papa na maghufira, na kuabudu Maria na “watakatifu.” Waliadhimisha pia Mlo wa Jioni wa Bwana au Chakula cha Jioni. Kulingana na Lambert, njia yao ya kuabudu, “ilikuwa kwa hakika dini ya watu wa kawaida.”

“Maisha Maradufu”

Jamii za Wawaldo zilikuwa na umoja. Walioa au kuolewa na watu wa kikundi chao na kwa karne nyingi hilo likatokeza majina ya ukoo ya Wawaldo. Hata hivyo, katika jitihada yao ya kuendelea kuwepo, Wawaldo walijaribu kuficha maoni yao. Kwa kuwa walificha imani na mazoea yao ya kidini kukawa mashtaka mengi yenye kufedhehesha dhidi yao kutoka kwa wapinzani. Kwa mfano, walisema kwamba waliabudu Ibilisi. *

Njia moja ambayo Wawaldo walitumia kuepuka mashtaka hayo ilikuwa kulegeza msimamo wao na kufanya kile mwanahistoria aitwaye Cameron alikiita “kukubaliana kwa kiasi kidogo” na ibada ya Katoliki. Wawaldo wengi walitubu kwa kasisi wa Katoliki, wakahudhuria Misa, wakatumia maji matakatifu, na hata wakaenda hija. Lambert asema: “Katika mambo mengi, waliiga majirani wao Wakatoliki.” Audisio asema wazi kwamba baada ya muda, Wawaldo “waliishi maisha maradufu.” Yeye aongezea kusema: “Kwa upande mmoja walitenda na kuonekana kama Wakatoliki ili kulinda amani waliyokuwa nayo, na kwa upande mwingine wakashikilia utaratibu na desturi fulani miongoni mwao zilizowawezesha kuungana kama jamii na kuendelea kuwepo.”

Waacha Uzushi na Kuwa Waprotestanti

Katika karne ya 16, Marekebisho Makubwa ya Kidini yalibadili kabisa dini huko Ulaya. Watu wasiovumiliwa ama wangetafuta kutambuliwa kisheria nchini mwao au wangehamia sehemu nyinginezo ili kutafuta hali bora zaidi. Maoni ya uzushi pia yakapoteza maana, kwani watu wengi sana walianza kutilia shaka mafundisho ya kidini yaliyotambuliwa na wengi.

Mapema mwaka wa 1523, Mteteaji wa Marekebisho Makubwa ya Kidini Martin Luther aliwataja Wawaldo. Mnamo mwaka wa 1526 mmoja wa wale wajomba wa Wawaldo alirudi kwenye milima ya Alps akiwa na habari za maendeleo ya kidini huko Ulaya. Hayo yalifuatwa na kipindi cha mabadilishano ya maoni kati ya jamii za Waprotestanti na Wawaldo. Waprotestanti waliwatia moyo Wawaldo wadhamini tafsiri ya kwanza ya Biblia katika Kifaransa kutoka kwa lugha ya awali. Tafsiri hiyo ilichapishwa mwaka wa 1535, na ikaja kuitwa Biblia ya Olivétan. Kwa kusikitisha, Wawaldo wengi hawakuelewa Kifaransa.

Mnyanyaso kutoka kwa Kanisa Katoliki ulipoendelea, Wawaldo wengi waliishi katika maeneo salama ya Provence kusini mwa Ufaransa pamoja na Waprotestanti waliohamia huko. Serikali ilijulishwa mara moja kuhusu kuhama kwao. Wajaposemwa kuwa na maisha na maadili bora, Wawaldo walilaumiwa na watu fulani walioshuku unyofu wao na kuwashtaki kuwa tisho kwa amani na usalama. Sheria ya Mérindol ilitolewa na ilisababisha umwagaji wa damu mbaya sana ambao ulitajwa mwanzoni mwa makala hii.

Uhusiano kati ya Wakatoliki na Wawaldo ukaendelea kuzorota. Ili kujihami kutokana na mashambulizi yaliyofanywa dhidi yao, Wawaldo waliamua kutumia silaha. Mapambano hayo yakawapeleka karibu na maeneo ya Waprotestanti. Hivyo Wawaldo wakajiunga na Uprotestanti.

Kwa karne nyingi, makanisa ya Wawaldo yalianzishwa katika nchi nyingi zilizo mbali sana na Ufaransa kama vile Uruguai na Marekani. Hata hivyo wanahistoria wengi wanakubaliana na Audisio, aliyesema kwamba “Uwaldo uliisha wakati wa yale Marekebisho Makubwa ya Kidini,” wakati “ulipomezwa” na Uprotestanti. Kwa kweli, kikundi cha Wawaldo kilikuwa kimepoteza bidii kilichokuwa nayo karne nyingi mapema. Hilo lilitokea wakati wafuasi wake waliacha kwa hofu mahubiri na mafundisho yaliyotegemea Biblia.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 7 Vaudès anajulikana kwa majina mbalimbali kama vile, Valdès, Valdesius, au Waldo. Usemi “Wawaldo” ulitokana na jina lake la mwisho. Wawaldo walijulikana pia kama Maskini wa Lyons.

^ fu. 8 Mapema mwaka wa 1199, askofu wa Metz, jiji lililoko kaskazini mashariki mwa Ufaransa, alimlalamikia Papa Innocent wa Tatu kwamba watu fulani walikuwa wakisoma na kujadili Biblia katika lugha yao. Ni wazi kwamba askofu huyo alikuwa akizungumza kuhusu Wawaldo.

^ fu. 15 Ona “Wakathari—Je, Walikuwa Wakristo Wafia-imani?” katika gazeti Mnara wa Mlinzi la Septemba 1, 1995, ukurasa wa 27-30.

^ fu. 21 Kuendelea kushutumiwa kwa Wawaldo kulitokeza neno vauderie (linalotokana na neno la Kifaransa, vaudois). Neno hilo hutumiwa kurejezea watu wanaodhaniwa kuwa wazushi au waabudu Ibilisi.

[Ramani/Picha katika ukurasa wa 23]

 

Sehemu zilizoathiriwa na Wawaldo

UFARANSA

Lyons

PROVENCE

Lubéron

Strasbourg

Milan

Roma

Berlin

Prague

Vienna

[Picha]

Wawaldo walikuwa wadhamini wa tafsiri ya Biblia ya Olivétan ya 1535

[Hisani]

Biblia: © Cliché Bibliothèque nationale de France, Paris

[Picha katika ukurasa wa 20, 21]

VAUDÈS

Kuteketezwa kwa wanawake wawili wazee Wawaldo

[Hisani]

Ukurasa wa 20 na 21: © Landesbildstelle Baden, Karlsruhe