Madhabahu kwa Mungu Asiyejulikana
Madhabahu kwa Mungu Asiyejulikana
MTUME Paulo alitembelea jiji la Athene, Ugiriki, yapata mwaka wa 50 W.K. Akiwa huko, aliona madhabahu iliyotengwa kwa mungu asiyejulikana na baadaye akaitaja alipokuwa akitoa ushahidi mzuri kuhusu Yehova.
Alipoanza hotuba yake kwenye Kilima cha Mars, au Areopago, Paulo alisema: “Wanaume wa Athene, naona kwamba katika mambo yote mwaonekana kuwa wenye mwelekeo zaidi wa kuhofu miungu kuliko wengine walivyo. Kwa mfano, nilipokuwa nikipita njiani na kutazama kwa uangalifu vitu vyenu vya kupewa heshima inayozidi nilikuta pia madhabahu ambayo juu yayo ilikuwa imeandikwa ‘Kwa Mungu Asiyejulikana.’ Kwa hiyo kile mnachokipa ujitoaji-kimungu bila kujua, hicho ninawatangazia nyinyi.”—Matendo 17:22-31.
Ijapokuwa madhabahu hayo ya Athene hayajawahi kupatikana, madhabahu yanayofanana na hayo yalikuweko sehemu nyingine za Ugiriki. Kwa mfano, mwanajiografia Mgiriki, Pausanias alitaja madhabahu ya ‘miungu Isiyojulikana’ iliyokuwa huko Phaleron karibu na Athene. (Description of Greece, Attica I, 4) Kitabu hichohicho kilisema kwamba, kulikuwa na “madhabahu ya miungu Isiyojulikana huko Olympia.”—Eleia I, XIV, 8.
Katika kitabu chake The Life of Apollonius of Tyana (VI, III), mwandikaji Mgiriki, Philostratus (wapata mwaka wa 170-245 W.K.) alisema kwamba huko Athene “kulikuwa na madhabahu za kutukuza miungu isiyojulikana.” Na katika kichapo Lives of Philosophers (1.110), Diogenes Laertius (wapata mwaka wa 200-250 W.K.) aliandika kwamba “madhabahu yasiyojulikana” yalionekana katika sehemu mbalimbali za Athene.
Pia Waroma walijenga madhabahu kwa miungu isiyojulikana. Picha tunayoona hapa ni ya madhabahu ya karne ya kwanza au ya pili K.W.K. iliyohifadhiwa kwenye Jumba la Kuhifadhi Vitu vya Kale la Palatine, huko Rome, Italia. Maandishi yake ya Kilatini yanaonyesha kwamba madhabahu hayo yalitengwa kwa kusudi takatifu kwa “mungu au mungu-mke”—usemi “ambao mara nyingi unapatikana katika sala au katika matamshi matakatifu kwenye maandishi yaliyochongwa na kwenye vichapo.”
Bado watu wengi hawamfahamu “Mungu aliyeufanya ulimwengu na vitu vyote vilivyo katika huo.” Lakini kama vile Paulo alivyowaambia Waathene, Mungu huyu—Yehova—“hayuko mbali sana na kila mmoja wetu.”—Matendo 17:24, 27.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 32]
Madhabahu: Soprintendenza Archeologica di Roma