Maisha Yanayoongozwa na Ushirikina
Maisha Yanayoongozwa na Ushirikina
UNAKUTANA na mtu unapotoka nyumbani. Unajikwaa kwenye jiwe. Ndege fulani anaimba usiku. Umekuwa ukiota ndoto fulani tena na tena. Watu wengi huona mambo hayo kuwa ya kawaida tu, yasiyodhuru. Lakini watu fulani huko Afrika Magharibi wanaweza kuyaona kuwa ishara, dalili ya jambo zuri au baya, au ujumbe kutoka kwa roho. Inasemekana kwamba mtu anaweza kupatwa na mambo mazuri au mabaya kulingana na ishara anayoona na jinsi ishara hiyo inavyofafanuliwa.
Bila shaka, si Waafrika tu wanaoamini ushirikina. Inashangaza kwamba watu wengi huko China na nchi za ule uliokuwa Muungano wa Sovieti huamini ushirikina, ijapokuwa wameishi kwa miaka mingi katika jamii ambayo haiamini kuna Mungu. Katika nchi fulani za Magharibi, watu wengi hufanya uaguzi kwa kutumia nyota, huogopa tarehe ya 13 ikifika siku ya Ijumaa, na huepuka paka weusi. Watu wengine wa Kaskazini ya Mbali huona mianga fulani inayotokea upande wa kaskazini kuwa ishara ya kutokea kwa vita au jambo baya. Huko India UKIMWI unaenezwa na madereva wa malori ambao wanaamini kwamba wanahitaji kufanya ngono kunapokuwa na joto jingi ili wapunguze joto mwilini. Huko Japan, wafanyakazi wanaochimba njia za chini ya ardhi huamini kwamba, mwanamke ataleta bahati mbaya ikiwa ataingia humo kabla hawajamaliza kuchimba. Pia wachezaji wengi wa kulipwa wanaamini ushirikina. Mchezaji mmoja wa voliboli alisema kwamba waliweza kushinda mfululizo kwa sababu ya kuvaa soksi nyeusi badala ya nyeupe. Bado kuna mambo mengi kuhusiana na ushirikina ambayo hayakutajwa.
Namna gani wewe? Je, huenda kuna jambo fulani lisiloelezeka ambalo linakutia hofu? Je, ‘kuna jambo ambalo unaamini au kufanya bila sababu?’ Jibu lako linaweza kuonyesha kama maisha yako yanaongozwa na ushirikina au la, kwa kuwa ushirikina ni hali au tabia ya kuogopa au kuamini mambo bila msingi.
Mtu anayeruhusu ushirikina uathiri maamuzi yake na ratiba yake ya kila siku anajiacha aongozwe na kitu asichojua. Je, hilo ni jambo la hekima? Je, tujiache tuongozwe na imani hiyo mbovu isiyo na msingi? Je, ushirikina ni udhaifu tu usiokuwa na madhara au ni jambo hatari?