Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Yoga Je, Ni Mazoezi Tu au Kuna Mengi Zaidi Yanayohusika?

Yoga Je, Ni Mazoezi Tu au Kuna Mengi Zaidi Yanayohusika?

Yoga Je, Ni Mazoezi Tu au Kuna Mengi Zaidi Yanayohusika?

WATU wengi leo hufikiria sana jinsi wanavyoweza kuwa na mwili mwembamba na afya nzuri. Jambo hilo limefanya wengi watafute msaada katika kilabu za mazoezi ya viungo vya mwili na pia za kuboresha afya. Kwa sababu hiyohiyo, maelfu ya watu kutoka nchi za Magharibi wamegeukia yoga (mfumo wa mazoezi ya maungo na kudhibiti pumzi) ya nchi za Mashariki.

Watu wanaokabiliana na mkazo, mshuko-moyo, na mfadhaiko pia wamegeukia yoga ili kupata faraja na utatuzi wa matatizo yao. Watu wa nchi za Magharibi walianza kupendezwa na dini za Mashariki na desturi zao za kifumbo hasa tangu miaka ya 1960. Kutafakari kama kule kunakofanywa na Dini ya Uhindu ambako kulitokana na yoga, kumependwa sana kwa sababu wacheza-sinema na wanamuziki wa roki wanapenda aina hiyo ya yoga. Kwa kuwa watu wengi wanazidi kupendezwa na yoga, huenda tukajiuliza: ‘Je, yoga ni mazoezi ya kawaida tu ambayo hufanya mtu awe mwembamba, mwenye afya nzuri na kumpa amani ya akili? Je, mtu anaweza kufanya mazoezi ya yoga bila kuingilia mambo ya kidini? Je, yoga inawafaa Wakristo?’

Jinsi Yoga Ilivyoanza

Neno la awali la Kisanskriti ‘yoga’ linaweza kuwa na maana ya kuweka kitu chini ya nira, kufunga pamoja au kudhibiti. Wahindu huona yoga kuwa mbinu au mfumo wa kudhibiti utendaji fulani ambao hatimaye huunganisha mtu na kiumbe wa roho au na nguvu zisizo za kawaida. Imefafanuliwa kuwa “kuunganisha nguvu zote za mwili, akili na nafsi pamoja na Mungu.”

Mazoezi ya yoga yalianza zamani kadiri gani? Michoro ya watu walioketi wakitazama pande mbalimbali huku wakifanya mazoezi ya yoga imepatikana katika Bonde la Indus, ambalo liko Pakistan ya sasa. Waakiolojia wanadai kwamba ustaarabu wa Bonde la Indus ulianza kati ya milenia ya tatu na ya pili K.W.K., karibu sana na kipindi cha utamaduni wa Mesopotamia. Sanamu zilizotengenezwa kutoka sehemu hizo mbili zinaonyesha mtu anayewakilisha mungu, aliyevikwa pembe za mnyama na ambaye amezungukwa na wanyama. Sanamu hizo zinatukumbusha Nimrodi, aliyekuwa “hodari wa kuwinda.” (Mwanzo 10:8, 9) Wahindu hudai kwamba watu hao walioketi wakitazama pande mbalimbali ni sanamu zinazowakilisha mungu Siva, bwana wa wanyama na bwana wa yoga, ambaye mara nyingi huabudiwa kupitia sanamu ya uume. Kwa hiyo, kitabu Hindu World kinaita yoga ‘mfumo wa mazoezi wenye sheria kali, ambao hasa ulianza kabla ya Waarya, na ambao unahusisha imani na desturi za kale.’

Mwanzoni, mbinu mbalimbali za kufanya mazoezi ya yoga zilipokezanwa kwa mdomo. Kisha zikaandikwa na kufafanuliwa zaidi na Patañjali, mwalimu Mhindi wa yoga mwenye hekima, katika kitabu Yoga Sutra—ambacho hadi sasa ndicho kitabu cha msingi cha mafundisho ya yoga. Kulingana na Patañjali, yoga ni ‘jitihada ya hatua kwa hatua ya kufikia ukamilifu, kwa kudhibiti mwili na akili.’ Tangu mfumo wa yoga uanzishwe hadi sasa, umekuwa sehemu muhimu ya dini za Mashariki, na hasa Uhindu, Ujaini, na Ubudha. Watu fulani wanaojihusisha na yoga huamini kwamba itawasaidia kufikia moksha, au ukombozi kwa kuungana na roho fulani iliyo kila mahali.

Twauliza kwa mara nyingine tena: ‘Je, mtu anaweza kujihusisha na yoga kama mazoezi tu ili awe na mwili wenye afya na akili tulivu pasipo kujihusisha na dini?’ Kwa sababu ya asili ya yoga, jibu ni la.

Yoga Inaweza Kukuelekeza Wapi?

Kusudi la yoga ni kumsaidia mtu aungane na roho fulani mwenye uwezo unaozidi wa kibinadamu na apate maono ya kiroho. Lakini kiumbe huyo wa roho ni nani?

Katika kitabu Hindu World, mwandishi Benjamin Walker asema hivi kuhusu yoga: ‘Labda yoga ni utaratibu wa kale wa kufanya mambo ya kichawi, na hata sasa yoga inahusisha mambo fulani ya kichawi.’ Wanafalsafa Wahindu wanakiri kwamba mtu akifanya mazoezi ya yoga anaweza kupata uwezo unaozidi wa kibinadamu, hata ingawa wanadai kwamba hilo si kusudi kuu la yoga. Kwa mfano, katika kitabu Indian Philosophy, aliyekuwa rais wa India, Dakt. S. Radhakrishnan anasema kwamba mtu anayefanya mazoezi ya yoga “hasikii joto kali au baridi kali kwa sababu ya kudhibiti mwili wake kwa kubadili vikao vyake. . . . Mtu anayefanya mazoezi ya yoga anaweza kuona na kusikia sauti kutoka mbali . . . Anaweza kuwasiliana na mwenzake pasipo kutumia njia za kawaida za mawasiliano. . . . Mtu anayefanya mazoezi ya yoga anaweza kufanya mwili wake usionekane.”

Huenda watu fulani wakafikiri kwamba ni mzaha au ni jambo la kuchekesha kuona mwalimu wa yoga amelala juu ya kitanda chenye misumari au akitembea juu ya makaa moto. Lakini mambo hayo ni ya kawaida nchini India, kutia ndani ile desturi ya kusimama kwa mguu mmoja na kutazama jua kwa muda wa saa nyingi na pia desturi ya kudhibiti pumzi ambayo humwezesha mtu kufunikwa kwa changarawe kwa muda mrefu. Mnamo Juni 1995, gazeti The Times of India liliripoti kwamba gari lenye uzito wa kilogramu 750 liliachiliwa lipite juu ya tumbo la msichana mwenye umri wa miaka mitatu na nusu aliyekuwa katika hali ya kuduwaa. Umati ulishangaa wakati msichana huyo alipoamka akiwa bila madhara yoyote. Ripoti hiyo iliendelea kusema: “Hizo ni nguvu za yoga tu.”

Bila shaka, mtu mwenye nguvu za kawaida hawezi kufanya mambo hayo. Kwa hiyo, Mkristo anapaswa kujiuliza: Matendo hayo ya ajabu huonyesha nini? Je, yanatoka kwa Yehova Mungu ‘Aliye juu, juu ya nchi yote,’ au yana chanzo kingine? (Zaburi 83:18) Biblia inatoa jibu lililo wazi juu ya jambo hilo. Waisraeli walipokaribia kuingia katika Bara Lililoahidiwa, ambalo lilikaliwa na Wakanaani, Yehova aliwaambia wana wa Israeli hivi kupitia Musa: “Usijifunze kutenda kwa mfano wa machukizo ya mataifa yale.” Ni “machukizo” gani hayo? Musa alionya kusiwe na ‘mtu atazamaye bao, mtu atazamaye nyakati mbaya, mwenye kubashiri, au msihiri.’ (Kumbukumbu la Torati 18:9, 10) Mambo hayo ni machukizo kwa Mungu kwa sababu ni matendo ya roho waovu na ya mwili wenye dhambi.—Wagalatia 5:19-21.

Si Chaguo la Wakristo

Huenda walimu wa masuala ya afya wasikubali habari iliyo juu. Hata hivyo, yoga si mazoezi ya mwili tu. Kitabu Hindu Manners, Customs and Ceremonies kinataja mambo ambayo watu wawili walijionea walipoanza kufanya mazoezi ya yoga wakiwa chini ya mwelekezo wa guru. Mmoja wao alinukuliwa kusema: “Kwa kutumia uwezo unaozidi wa kibinadamu, nilijitahidi kutopumua kwa muda mrefu kadiri nilivyoweza, na nilipumua tu nilipokaribia kuzimia. . . . Siku moja, saa sita mchana, nilifikiri kwamba niliona mwezi mpevu, ulioonekana kuwa ukisonga toka upande mmoja hadi mwingine. Wakati mwingine nilifikiri kwamba nimefunikwa na giza tititi mchana. Mwelekezi wangu . . . alifurahi sana nilipomtajia maono hayo. . . . Alinihakikishia kwamba, punde baada ya hapo nitajionea mambo mengi ya kushangaza kwa sababu ya majaribu yangu.” Wa pili anasimulia hivi: “Alinilazimisha kutazama anga kila siku bila kupepesa macho au kubadili kikao changu. . . . Nyakati nyingine nilifikiri kwamba niliona cheche za moto hewani; nyakati nyingine ni kana kwamba niliona matufe na vimondo vingine. Mwalimu wangu alifurahia sana mafanikio niliyopata kwa sababu ya jitihada zangu.”

Yaonekana walimu waliona mambo hayo ya ajabu kuwa matokeo mazuri ambayo yangeongoza kwenye kusudi halisi la mazoezi ya yoga. Naam, mradi mkuu wa yoga ni moksha, hali inayofafanuliwa kuwa kule kuungana na roho kuu isiyo na umbo. Unafafanuliwa kuwa “kuzuia (kimakusudi) uwezo wa kufikiri.” Jambo hili linapingana na mradi ambao Wakristo wamewekewa na ambao wanashauriwa hivi: “Mtoe miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, yenye kukubalika kwa Mungu, utumishi mtakatifu pamoja na nguvu zenu za kufikiri kuzuri. Na komeni kufanyizwa kulingana na mtindo wa mfumo huu wa mambo, bali mgeuzwe umbo kwa kufanya upya akili yenu, ili mpate kujithibitishia wenyewe mapenzi ya Mungu yaliyo mema na yenye kukubalika na makamilifu.”—Waroma 12:1, 2.

Mtu binafsi ndiye anayepaswa kujiamulia mwenyewe mazoezi ya mwili atakayofanya. Hata hivyo, Wakristo hawawezi kuruhusu jambo lolote—liwe ni mazoezi ya mwili, kula, kunywa, kuvaa, kujiburudisha, au jambo jingine lolote—liharibu uhusiano wao pamoja na Yehova Mungu. (1 Wakorintho 10:31) Kwa wale wanaofanya mazoezi kwa sababu ya afya, kuna aina nyingi za mazoezi ambazo hazihusishi hatari ya kuwasiliana na roho na mambo ya kimafumbo. Kwa kujiepusha na mazoea na imani ambayo inatokana na dini isiyo ya kweli, tunaweza kutazamia baraka za Mungu kwenye mfumo mpya wa mambo wenye uadilifu, ambapo tutakuwa na afya ya mwili na ya akili milele.—2 Petro 3:13; Ufunuo 21:3, 4.

[Picha katika ukurasa wa 22]

Wengi hufurahia mazoezi yafaayo yasiyohusisha kuwasiliana na roho