‘Sameheaneni kwa Hiari’
‘Sameheaneni kwa Hiari’
JE, UNAAMINI kwamba Mungu amekusamehe dhambi zako? Huko Marekani, inaonekana kwamba wengi wanaamini hivyo. Dakt. Loren Toussaint aliyekuwa wa kwanza kuandika juu ya uchunguzi fulani uliofanywa kwenye Chuo Kikuu cha Michigan Institute for Social Research anaripoti kwamba kati ya Wamarekani 1,423 wenye umri unaozidi miaka 45 ambao walihojiwa, asilimia 80 hivi ndio waliosema kwamba Mungu amewasamehe dhambi zao.
Hata hivyo, inashangaza kwamba asilimia 57 tu ya watu hao waliohojiwa ndio waliosema kwamba wanawasamehe wengine. Takwimu hizo zinatukumbusha maneno ya Yesu katika Mahubiri yake ya Mlimani: “Ikiwa mwasamehe watu makosa yao, Baba yenu wa kimbingu atawasamehe nyinyi pia; lakini ikiwa hamsamehi watu makosa yao, wala Baba yenu hatasamehe makosa yenu.” (Mathayo 6:14, 15) Naam, Mungu hutusamehe dhambi ikiwa tu tuko tayari kuwasamehe wengine.
Mtume Paulo aliwakumbusha Wakristo wa Kolosai kanuni hiyo alipowahimiza hivi: “Endeleeni kuchukuliana mtu na mwenzake na kusameheana kwa hiari mtu na mwenzake ikiwa yeyote ana sababu ya kulalamika dhidi ya mwingine. Kama vile Yehova alivyowasamehe nyinyi kwa hiari, fanyeni hivyo nyinyi pia.” (Wakolosai 3:13) Kwa kweli si rahisi kusameheana. Kwa mfano, si rahisi kumsamehe mtu anaposema juu yako bila kujali au bila fadhili.
Hata hivyo, kuna manufaa nyingi za kusamehe. Dakt. David R. Williams, mtaalamu wa mambo ya jamii alisema hivi kuhusu uchunguzi wake: ‘Tuligundua kwamba afya ya akili ya Wamarekani wa makamo na walio wazee inakuwa nzuri wanaposamehe wengine.’ Habari hiyo inapatana na maneno ya Mfalme Solomoni mwenye hekima aliyeandika hivi miaka ipatayo 3,000 iliyopita: “Moyo ulio mzima ni uhai wa mwili.” (Mithali 14:30) Tuna sababu nzuri ya kusameheana kwa hiari kutoka moyoni kwa kuwa kufanya hivyo huboresha uhusiano wetu pamoja na Mungu na jirani.—Mathayo 18:35.