Jumba la Ufalme Lapata Tuzo
Ripoti ya Watangazaji wa Ufalme
Jumba la Ufalme Lapata Tuzo
WIZARA ya Mazingira huko Finland iliteua mwaka wa 2000 kuwa “Mwaka wa Kutengeneza Mazingira.” Msimamizi mmoja wa mpango huo alisema kwamba ‘mwaka huo uliteuliwa ili kutukumbusha sote kwamba mazingira mazuri yanafanya maisha yetu na hali yetu iwe bora.’
Januari 12, 2001, ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova huko Finland ilipokea barua kutoka kwa shirika la Mandhari na Mazingira la Finland. Barua hiyo ilieleza kwamba Jumba la Ufalme la Mashahidi wa Yehova la Tikkurila limepewa mojawapo ya medali za mwaka huo kwa sababu ya mazingira yake mazuri na bustani zilizotunzwa vizuri. Barua hiyo iliendelea kusema kwamba ‘iwe ni wakati wa kiangazi au wa baridi kali, kwa ujumla mazingira ya Majumba ya Ufalme huvutia sana na utunzaji wake ni wa hali ya juu.’
Mashahidi wa Yehova walipewa medali hiyo katika hoteli moja iitwayo Rosendahl, huko Tampere, Finland. Sherehe hiyo ilihudhuriwa na wataalamu na wafanyabiashara 400. Shirika hilo linaloshughulikia mazingira lilitoa taarifa kwa waandishi wa habari ambayo ilisema hivi: “Katika sehemu mbalimbali nchini, karibu Majumba yote ya Ufalme ya Mashahidi wa Yehova yana mazingira mazuri. Karibu kila mtu anayepita karibu na Majumba hayo huvutiwa na mazingira yake yaliyotunzwa vizuri. Mazingira ya Jumba la Ufalme la Tikkurila ni mfano wa bustani nzuri. Majengo yake na uwanja wake mkubwa hudhihirisha hali ya utulivu na usawaziko.”
Huko Finland kuna Majumba ya Ufalme 233, na mengi ya Majumba hayo yana bustani nzuri sana. Hata hivyo, Majumba ya Ufalme yanakuwa mazuri hasa kwa sababu yanatumiwa kuwa vituo vya ibada ya kweli na elimu ya Biblia. Mashahidi wa Yehova zaidi ya milioni sita ulimwenguni hupenda Majumba yao ya Ufalme—yawe ni ya hali ya juu au ni ya kiasi. Hiyo ndiyo sababu wanapenda kuyatunza kwa bidii na kwa upendo. Wote katika eneo unamoishi wanakaribishwa kwenye Jumba la Ufalme!