“Wale Mamajusi Watatu” Walikuwa Nani?
“Wale Mamajusi Watatu” Walikuwa Nani?
Kwa kawaida, mandhari za kuzaliwa kwa Yesu huwa na watu watatu wenye kanzu na ngamia, wakiwasili kwenye kibanda ambapo mtoto Yesu amelala kwenye hori. Mara nyingi wageni hao waliovalia vizuri wanaitwa wale mamajusi watatu. Biblia husema nini kuwahusu?
Kulingana na Biblia, watu hao wanaoitwa mamajusi walitoka “sehemu za mashariki,” nao walipata habari za kuzaliwa kwa Yesu wakiwa huko. (Mathayo 2:1, 2, 9) Bila shaka iliwachukua muda mrefu kusafiri kutoka huko hadi Yudea. Hatimaye walipompata Yesu, hakuwa tena kitoto kichanga kwenye kibanda. Watu hao walimpata Maria na “huyo mtoto mchanga” wakiishi katika nyumba.—Mathayo 2:11.
Biblia huwaita watu hao magi, au watu wanaotabiri kwa kutumia nyota, nayo haisemi walikuwa wangapi. Kichapo The Oxford Companion to the Bible kinaeleza: “Tunaona uhusiano uliopo baina ya uchawi na kutabiri kwa kutumia nyota kwa kuwa wageni hao walivutiwa sana na nyota iliyowaongoza hadi Bethlehemu.” Biblia hushutumu namna zote za uchawi na desturi ya Wababiloni ya kujaribu kupata habari kutoka kwa nyota.—Kumbukumbu la Torati 18:10-12; Isaya 47:13.
Habari ambayo watu hao walipata haikuwa na matokeo mazuri. Ilimtia wivu na kumkasirisha Mfalme Herode mwovu. Hatimaye, habari hiyo pia ilifanya Yosefu, Maria, na Yesu wakimbilie Misri na pia ikafanya watoto wote wa kiume huko Bethlehemu “kuanzia umri wa miaka miwili kwenda chini” wauawe. Herode alikuwa amekadiria kwa makini wakati wa kuzaliwa kwa Yesu kutokana na habari alizopata kutoka kwa wale watu wanaotabiri kwa kutumia nyota. (Mathayo 2:16) Kwa sababu ya matatizo yote yaliyosababishwa na ziara yao, tunaweza kukata kauli kwamba nyota waliyoona na habari kuhusu “yule aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi” ilitoka kwa adui wa Mungu, Shetani Ibilisi, aliyetaka kumwua Yesu.—Mathayo 2:1, 2.