Je, Inawezekana Kuwa na Kazi ya Kudumu na ya Kuridhisha?
Je, Inawezekana Kuwa na Kazi ya Kudumu na ya Kuridhisha?
KILA mtu ana “haki ya kuajiriwa,” lasema azimio moja la Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu. Hata hivyo, si kila mtu anayefurahia haki hiyo. Kuwa na kazi ya kudumu kunategemea mambo mengi kama vile uchumi wa nchi na hali ya soko la dunia. Hata hivyo, watu wanapopoteza kazi ya kuajiriwa au wanapoona kwamba huenda wakaipoteza, mara nyingi wao hufanya maandamano, fujo, na migomo. Karibu mataifa yote yana matatizo hayo. Hata neno “kazi,” akasema mwandishi mmoja, “ni neno linalotokeza hisia kali.”
Kazi ni muhimu kwetu kwa sababu nyingi. Mbali na kutupatia riziki, kazi huboresha hali yetu ya kiakili na kihisia-moyo. Kazi huridhisha tamaa ya mwanadamu ya kuwa mtu anayenufaisha jamii na kuwa na maisha yenye kusudi. Kazi pia hufanya tujiheshimu. Kwa sababu hiyo, watu wengine huamua kuendelea kufanya kazi hata ingawa wana pesa za kutosha kutimiza mahitaji yao au wamefikia umri wa kustaafu. Naam, kazi ni muhimu sana hivi kwamba inapokosekana, kunakuwa na matatizo mabaya ya kijamii.
Kwa upande mwingine, kuna watu walioajiriwa ambao hawana furaha kwa sababu ya mikazo mingi wanayopata kazini. Kwa mfano, kwa sababu ya mashindano makali katika uuzaji wa bidhaa, makampuni mengi yamefuta baadhi ya wafanyakazi ili kupunguza gharama. Hivyo, huenda wafanyakazi waliosalia wakachoka sana kwa maana mara nyingi itawabidi kufanya kazi ya ziada.
Huenda tekinolojia ya kisasa, ambayo inatarajiwa kurahisisha maisha na kuboresha hali ya kazi, imeongeza mikazo kazini. Kwa mfano, kompyuta, mashine za faksi, na Internet huwawezesha watu kuendelea kufanya kazi nyumbani baada ya saa za kazi, na hivyo wanahisi kana kwamba wako kazini hata wakiwa nyumbani. Mfanyakazi mmoja wa kampuni fulani alisema kwamba simu ya mkononi aliyopewa kazini ilikuwa kama kamba isiyoonekana ambayo ilimfunga kwa mwajiri wake.
Wazee wengi wanahofia kwamba uchumi na hali ya kazi inayobadilika upesi itafanya waonekane kuwa hawafai ingawa bado wanaweza kufanya kazi. Kuhusu jambo hilo, Chris Sidoti, aliyekuwa mkuu wa Tume ya Haki za Binadamu alisema: “Waajiri wengi wana maoni ya kwamba usipokuwa na umri wa chini ya miaka 40, huwezi kufanya kazi kwa kutumia kompyuta au tekinolojia ya kisasa.”
Hivyo, siku hizi wafanyakazi wengi wazuri ambao zamani wangeonekana kuwa wamefikia umri wa kuwa na matokeo zaidi, huonekana kuwa wazee sana wasiwe na manufaa yoyote. Hiyo ni hali yenye kuhuzunisha kama nini!Ni jambo linaloeleweka kwamba katika miaka ya hivi karibuni watu wengi hawaoni umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii wala kuwa waaminifu kwa kampuni yao. Gazeti moja nchini Ufaransa liitwalo Libération lasema hivi: “Wafanyakazi huacha kuwa waaminifu kwa mashirika wanayofanyia kazi wakati mashirika hayo yanapowafuta wengine eti kwa sababu kumekuwa na mabadiliko kidogo katika soko la hisa. Naam, watu hufanya kazi kujinufaisha wenyewe tu wala si kampuni.”
Licha ya matatizo hayo yanayoongezeka, bado wanadamu wana ile tamaa ya asili ya kufanya kazi. Kwa hiyo, tunawezaje kusitawisha maoni yanayofaa kuhusu kazi ya kuajiriwa na wakati huohuo kuendelea kuhisi salama na wenye kuridhika kazini?
[Picha katika ukurasa wa 3]
Huenda tekinolojia ya kisasa imeongeza mikazo kazini