Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mahakama Kuu Yatetea Ibada ya Kweli Katika “Nchi ya Ararati”

Mahakama Kuu Yatetea Ibada ya Kweli Katika “Nchi ya Ararati”

Mahakama Kuu Yatetea Ibada ya Kweli Katika “Nchi ya Ararati”

Baba mwenye mvi wa Armenia mwenye watoto watatu asimama mbele ya mahakama kuu zaidi ya nchi yake. Uhuru wake na ule wa waamini wenzake umo hatarini. Mahakama inamsikiliza anaponukuu Biblia ili kueleza imani yake. Ili tupate kujua jinsi kesi hiyo ilivyoleta ushindi mkubwa kwa ibada ya kweli katika nchi hiyo, na tuchunguze jinsi mambo yalivyokuwa.

NCHI ya Armenia iko mashariki ya Uturuki kusini ya milima mikubwa ya Caucasus. Nchi hiyo ina wakazi zaidi ya milioni tatu. Ukiwa kwenye jiji kuu la nchi hiyo, Yerevan, unaweza kuona vilele viwili vyenye kuvutia sana vya Mlima Ararati, ambapo kulingana na mapokeo, safina ya Noa ilitua baada ya Gharika iliyokumba dunia nzima.—Mwanzo 8:4. *

Mashahidi wa Yehova wamekuwa wakifanya kazi yao ya Kikristo nchini Armenia tangu 1975. Baada ya Armenia kupata uhuru kutoka kwa ule uliokuwa Muungano wa Sovieti mwaka wa 1991, Baraza la Nchi la Kushughulikia Mambo ya Kidini lilibuniwa ili kusajili dini. Hata hivyo, mara kwa mara baraza hilo limekataa kuwasajili Mashahidi wa Yehova hasa kwa sababu ya msimamo wao wa Kikristo wa kutojiunga na jeshi. Hivyo, tangu mwaka wa 1991 zaidi ya Mashahidi vijana 100 nchini Armenia wamepatikana na hatia na mara nyingi kutiwa gerezani kwa sababu ya msimamo wao wa Kimaandiko wa kutojiunga na jeshi.

Baraza hilo pia liliiomba ofisi ya serikali ya kuendesha mashtaka ichunguze utendaji wa Lyova Margaryan, mzee Mkristo na mwanasheria mwenye bidii ambaye ameajiriwa kwenye mtambo wa nyukilia wa kutokeza nguvu za umeme. Hatimaye, Ndugu Margaryan alishtakiwa chini ya Kifungu cha 244, cha sheria ya zamani ya Sovieti iliyopitishwa wakati wa Khrushchev, ambayo ilikusudiwa kuwazuia na mwishowe kuwakomesha kabisa Mashahidi wa Yehova na dini nyinginezo.

Kulingana na sheria hiyo ni kosa kupanga au kuongoza kikundi cha kidini ambacho hutumia mahubiri kuwa kisingizio cha ‘kuwashawishi vijana kuhudhuria mikutano ya kidini ya dini ambayo haijasajiliwa’ na ‘kuwashawishi washiriki wake wakatae kufanya kazi ya serikali.’ Ili kuunga mkono dai lake, mwendesha-mashtaka alitaja kuwepo kwa watoto kwenye mikutano iliyoongozwa na Ndugu Margaryan katika jiji la Metsamor. Mwendesha-mashtaka pia alidai kwamba Ndugu Margaryan aliwalazimisha vijana wa kutaniko wakatae kujiunga na jeshi.

Kesi Yaanza

Kesi ilianza Ijumaa, Julai 20, 2001, katika mahakama ya wilaya ya Armavir nayo ilisikizwa na hakimu Manvel Simonyan. Iliendelea hadi katikati ya mwezi wa Agosti. Kesi hiyo ilipokuwa ikiendelea, mashahidi wa upande wa mashtaka walikiri kwamba Wizara ya Usalama wa Nchi (iliyoitwa KGB) ilikuwa imewaambia mashahidi hao taarifa ambazo wangeandikisha dhidi ya Ndugu Margaryan na kuwashurutisha kutia sahihi taarifa hizo. Pindi moja mwanamke mmoja alikiri kwamba afisa fulani wa Wizara ya Usalama alimwagiza adai kwamba “Mashahidi wa Yehova wanapinga serikali na dini yetu.” Mwanamke huyo alikiri kwamba hakujua Shahidi wa Yehova hata mmoja lakini alikuwa amesikia tu mashtaka yaliyofanywa dhidi yao na kutangazwa na kituo cha televisheni cha Taifa.

Wakati wa Ndugu Margaryan wa kujitetea ulipofika, alisema kwamba watoto wanaohudhuria mikutano ya Mashahidi wa Yehova huruhusiwa kufanya hivyo na wazazi wao. Pia alisema kwamba mtu binafsi ndiye huamua kama atajiunga na jeshi au la. Aliendelea kuhojiwa kwa siku kadhaa. Ndugu Margaryan, alitumia Biblia na kwa utulivu akajibu maswali aliyoulizwa kuhusu imani yake huku mwendesha-mashtaka akisoma kwenye Biblia yake Maandiko ambayo Margaryan alitaja.

Septemba 18, 2001, hakimu alitangaza kwamba Margaryan “hakuwa na hatia,” akisema kwamba kazi aliyokuwa akifanya “haikupingana na sheria hata kidogo.” Ripoti kuhusu kesi hiyo ilichapishwa katika gazeti la shirika la habari la Associated Press. Ilisema: “Leo kiongozi wa Mashahidi wa Yehova nchini Armenia aliondolewa mashtaka ya kugeuza watu imani na kuwalazimisha vijana wasijiunge na jeshi. Baada ya kesi hiyo kusikilizwa kwa muda wa miezi miwili, Mahakama ilisema kwamba hakukuwa na ushahidi wa kutosha kumshtaki kiongozi Levon Markarian [Lyova Margaryan]. Alikuwa ahukumiwe kifungo cha miaka mitano gerezani. . . . Ijapokuwa Katiba ya Armenia inaruhusu uhuru wa kidini, ni vigumu kwa vikundi vipya kusajiliwa kwani sheria inapendelea dini kubwa ya Armenian Apostolic Church.” Septemba 18, 2001, Muungano wa Usalama na Ushirikiano wa Ulaya (OSCE) ulitoa taarifa hii: “Ijapokuwa ofisi ya OSCE inakubaliana na uamuzi huo, inasikitika kwamba mashtaka hayo yalianzishwa.”

Kesi Yaendelea

Hata hivyo, waendesha-mashtaka walikata rufani na kesi hiyo ikaendelea tena kwa miezi mingine minne. Kesi ilipoanza na wakati wa Ndugu Margaryan wa kujitetea ulipofika, aliulizwa swali la kwanza na hakimu fulani wa jopo hilo. Ndugu Margaryan alipoanza kujibu mwenyekiti alimkatiza na kumpinga. Baada ya hapo, hakumruhusu Ndugu Margaryan kumaliza kujibu hata swali moja. Bila kutoa sababu, pia mwenyekiti huyo hakutia ndani maswali mengi ambayo Margaryan aliulizwa na wakili wa utetezi. Kesi ilipokuwa ikiendelea, wapinzani sugu wa kidini wanaowachukia Mashahidi na ambao walijaa mahakamani, walimtukana Ndugu Margaryan mara kadhaa. Baadaye, habari mbalimbali za uwongo na zenye kupotosha kuhusu kesi hiyo zilitangazwa kwenye televisheni, zikisema kuwa Ndugu Margaryan alikuwa amekubali kwamba ana hatia.

Kesi ilipokaribia kwisha, mwenyekiti wa jopo la mahakimu watatu aliwashangaza watazamaji kwa kutoa barua kutoka kwa Baraza la Nchi la Kushughulikia Mambo ya Kidini iliyodai ofisi ya mwendesha-mashtaka imchukulie hatua Ndugu Margaryan. Hatua hiyo iliwashangaza watazamaji kutoka nchi mbalimbali kwani Armenia ilipoomba kibali cha kujiunga na Baraza la Ulaya, ilikubali kwamba “itahakikisha kuwa Makanisa yote au vikundi vya kidini na hasa vile ambavyo havijakuwepo kwa muda mrefu, vitaruhusiwa kuendesha shughuli zao bila kubaguliwa.”

Kesi ilipokuwa ikiendelea katika majuma yaliyofuata, hali ilizidi kujaa wasiwasi. Wapinzani waliendelea kuwanyanyasa na kuwashambulia Mashahidi ndani na nje ya mahakama. Wanawake Mashahidi walipigwa mateke kwenye miundi. Shahidi mmoja aliposhambuliwa na kukataa kulipiza kisasi, alipigwa kwenye uti wa mgongo na akalazimika kulazwa hospitalini.

Wakati huohuo, hakimu mpya aliteuliwa kusikiliza kesi hiyo. Licha ya jitihada za watu wachache waliokuwa wanasikiliza kesi za kumwogopesha wakili wa utetezi, hakimu huyo alidumisha utulivu, hata aliwaamuru polisi wamtoe nje ya mahakama mwanamke fulani aliyekuwa akimtisha wakili wa utetezi.

Kesi Yapelekwa Kwenye Mahakama Kuu ya Armenia

Hatimaye, Machi 7, 2002, mahakama ya kukata rufani ilikubaliana na uamuzi wa mahakama ya wilaya. Jambo la kushangaza ni kwamba Baraza la Nchi la Kushughulikia Mambo ya Kidini lilivunjwa siku moja kabla ya uamuzi kutolewa. Kwa mara nyingine tena, waendesha-mashtaka walikata rufani dhidi ya uamuzi huo katika mahakama kuu zaidi ya Armenia. Sasa waendesha-mashtaka waliiomba Mahakama hiyo isikilize kesi hiyo tena, ili Margaryan “apatikane na hatia.”

Jopo la mahakimu sita, waliosimamiwa na Hakimu Mher Khachatryan, lilikutana saa 5:00 asubuhi Aprili 19, 2002. Katika maneno yake ya ufunguzi, mmoja wa waendesha-mashtaka alisema alikasirika sana kwamba mahakama mbili zilizosikiliza kesi hiyo awali zilishindwa kumpata Ndugu Margaryan na hatia. Hata hivyo, mwendesha-mashtaka huyo alikatizwa na kuulizwa maswali makali na mahakimu wanne. Hakimu mmoja alimkemea mwendesha-mashtaka kwa kujaribu kuathiri uamuzi wa Mahakama kwa kutaja mambo kama kuhubiri, kutosajiliwa kwa Mashahidi wa Yehova katika mashtaka yake dhidi ya Ndugu Margaryan, mambo ambayo hayakuwa kinyume cha sheria kupatana na Kifungu cha 244. Hivyo hakimu huyo akasema kwamba mwendesha-mashtaka ‘alimnyanyasa Margaryan kwa kutumia isivyofaa Kifungu cha 244 ili kumpata na hatia ya uhalifu.’ Hakimu mwingine alitaja kesi mbalimbali zilizosikilizwa na Mahakama ya Ulaya ambapo Mashahidi wa Yehova walitambuliwa kuwa “dini inayojulikana” inayostahili kulindwa na Mkataba wa Ulaya Unaohusu Haki za Kibinadamu. Wakati huo, kasisi mmoja kwenye mahakama alipiga kelele kwa ukali kwamba Mashahidi wa Yehova walikuwa wakiligawanya taifa, lakini Mahakama ikamwamuru anyamaze.

Kisha mahakimu wakamwita Lyova Margaryan kutoka miongoni mwa watu waliokuwa wakisikiliza kesi—hatua isiyo ya kawaida katika mahakama hiyo kuu. Ndugu Margaryan alitoa ushahidi mzuri kuhusu msimamo wa Kikristo wa Mashahidi wa Yehova kuhusiana na masuala mbalimbali. (Marko 13:9) Baada ya mashauriano mafupi, mahakimu hao walirudi na kwa pamoja wakaunga mkono uamuzi uliokuwa umetolewa awali kwamba Ndugu huyo hakuwa na hatia. Ndugu Margaryan alionekana kufarijiwa na uamuzi huo. Katika uamuzi ulioandikwa, Mahakama ilisema: “Kazi [ya Lyova Margaryan] haipingani na sheria iliyopo, na mashtaka yaliyofanywa dhidi yake yanapingana na Kifungu cha 23 cha Katiba ya Armenia na Kifungu cha 9 cha Mkataba wa Ulaya.”

Matokeo ya Uamuzi Huo

Kama mwendesha-mashaka angefaulu, wazee katika makutaniko yote ya Mashahidi nchini Armenia wangechukuliwa hatua ya kisheria. Tunatumaini kwamba uamuzi huo uliotolewa na Mahakama utazuia ndugu hao wasipatwe na mnyanyaso kama huo. Uamuzi usiofaa pia ungeweza kutumiwa kama kisingizio cha kutowasajili Mashahidi wa Yehova. Tunashukuru kwamba Mahakama hiyo sasa imeondoa kisingizio hicho cha uwongo.

Tutaona kama Mashahidi wa Yehova 7,000 katika nchi hiyo watasajiliwa. Lakini wakati huu, ibada ya kweli bado inaendelea vizuri “katika nchi ya Ararati.”

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 3 Hii ni sababu moja inayofanya Waarmenia wahusianishe nchi yao na Mlima Ararati. Zamani, nchi ya Armenia ilikuwa milki kubwa ambayo ilitia ndani milima hiyo. Hivyo, kwenye Isaya 37:38, Biblia ya Kigiriki ya Septuagint hutafsiri jina “nchi ya Ararati” kuwa “Armenia.” Sasa Mlima Ararati uko Uturuki karibu na mpaka wake wa mashariki.

[Picha katika ukurasa wa 12]

Lyova Margaryan wakati wa kesi yake

[Picha katika ukurasa wa 13]

Ndugu Margaryan na familia yake