Fadhili-Upendo Ni Muhimu Kadiri Gani?
Fadhili-Upendo Ni Muhimu Kadiri Gani?
“BIBLIA inasema: “Haja ya mwanadamu ni hisani [“fadhili-upendo,” NW] yake.” (Mithali 19:22) Kwa kweli, matendo ya fadhili yanayochochewa na upendo ni yenye kupendeza sana. Hata hivyo, katika Biblia neno “fadhili-upendo” linamaanisha fadhili ambayo huenda ikaonyeshwa kwa sababu ya uhusiano uliopo ambao unategemea tendo la fadhili ambalo mtu alitendewa hapo awali. Kwa hiyo linahusisha uaminifu.
Mfalme Yoashi wa Yuda hakusitawisha sifa hiyo yenye kupendeza. Alipaswa kumshukuru sana shangazi yake na mjomba wake, Yehoyada. Kabla ya Yoashi kufikia umri wa mwaka mmoja, nyanya yake mwovu alijitawaza kuwa malkia na kuwaua ndugu wote wa Yoashi ambao walikuwa warithi wa kiti cha ufalme. Hata hivyo, hakumwua Yoashi mdogo kwa sababu alikuwa amefichwa na shangazi yake na mjomba wake. Pia walimfundisha Sheria ya Mungu. Yoashi alipokuwa na umri wa miaka saba, mjomba wake aliyekuwa kuhani mkuu alitumia mamlaka yake kumwua malkia huyo mwovu na kumtawaza Yoashi kuwa mfalme.—2 Mambo ya Nyakati 22:10–23:15.
Kijana Yoashi alitawala kwa njia inayofaa hadi kifo cha mjomba wake, lakini baadaye akaanza kuabudu sanamu. Mungu alimtuma Zekaria mwana wa Yehoyada kumwonya Yoashi kwa sababu ya uasi wake. Yoashi aliamuru Zekaria auawe kwa kupigwa mawe. Tendo hilo la kukosa uaminifu kwa familia ambayo ilimwonyesha fadhili nyingi lilikuwa baya kama nini!—2 Mambo ya Nyakati 24:17-21.
Biblia inasema: “Mfalme Yoashi hakuukumbuka wema [“fadhili-upendo,” NW], ambao Yehoyada, baba yake, alimfanyia, bali alimwua mwanawe.” Alipokaribia kufa Zekaria alisema: “BWANA na ayaangalie haya, akayatakie kisasi.” Kama Zekaria alivyosema, Yoashi akawa mgonjwa sana na akauawa na watumishi wake.—2 Mambo ya Nyakati 24:17-25.
Badala ya kuwa kama Yoashi, wote wanaofuata ushauri ufuatao watakuwa na wakati ujao mzuri: “Rehema na kweli zisifarakane nawe; . . . Ndivyo utakavyopata kibali . . . mbele za Mungu na mbele ya mwanadamu.”—Mithali 3:3, 4.