Kila Mtu Ataketi Chini ya Mtini Wake
Kila Mtu Ataketi Chini ya Mtini Wake
KIVULI huthaminiwa sana wakati wa majira ya joto kali huko Mashariki ya Kati. Mti wowote wenye kivuli huthaminiwa sana hasa unapokua karibu na nyumba. Mtini una kivuli kizuri kuliko miti mingi huko Mashariki ya Kati kwa kuwa majani yake ni makubwa na mapana na matawi yake yamesambaa.
Kitabu Plants of the Bible kinasema kwamba “kivuli [cha mtini] hudhaniwa kuwa chenye kuburudisha na chenye baridi zaidi kuliko hema.” Katika Israeli la kale, mitini iliyopandwa kandokando ya mashamba ya mizabibu ilikuwa na kivuli kizuri ambapo wafanyakazi wa shambani wangeweza kupumzika kidogo.
Baada ya siku yenye joto na shughuli nyingi, washiriki wa familia wangeketi chini ya mitini yao na kufurahia kuwa pamoja. Isitoshe, mtini humthawabisha mwenye shamba kwa matunda mengi yenye kujenga mwili. Kwa hiyo, tangu siku za Mfalme Sulemani kuketi chini ya mtini kulimaanisha amani, ufanisi, na utele.—1 Wafalme 4:24, 25.
Karne kadhaa mapema, nabii Musa aliifafanua Nchi ya Ahadi kuwa ‘nchi ya mitini.’ (Kumbukumbu la Torati 8:8) Kwa kuleta tini na matunda mengine kwenye kambi ya Waisraeli, wapelelezi 12 walithibitisha kwamba nchi hiyo ilikuwa yenye rutuba. (Hesabu 13:21-23) Zaidi ya miaka 100 iliyopita, mtu aliyesafiri katika nchi zinazotajwa katika Biblia alisema kwamba kulikuwa na mitini mingi huko. Si ajabu kwamba mara nyingi tini na mitini inatajwa katika Biblia!
Mti Unaozaa Mara Mbili kwa Mwaka
Mtini unaweza kukua katika sehemu zenye udongo wa aina mbalimbali, na mizizi yake yenye kusambaa huuwezesha kustahimili majira marefu ya kiangazi huko Mashariki ya Kati. Mti huo ni wa kipekee kwa sababu zao lake la mapema hutokea mwezi wa Juni, kisha zao kuu mwezi wa Agosti na kuendelea. (Isaya 28:4) Kwa kawaida Waisraeli walikula zao la mapema kabla ya kukaushwa. Walikausha zao kuu kwa matumizi ya mwaka mzima. Tini zi lizokaushwa zingeweza kushinikizwa ili kutengeneza keki za mviringo ambazo nyakati nyingine zilichanganywa na lozi. Keki hizo zilikuwa rahisi kutayarisha, tamu, na zenye kujenga mwili.
Abigaili, mwanamke mwenye busara alimpa Daudi keki 200 za tini zilizoshinikizwa na yaelekea alifikiri kwamba zilikuwa chakula kinachowafaa watoro. (1 Samweli 25:18, 27) Tini zilizoshinikizwa zilitumiwa pia kama dawa. Tini zilizokauka ambazo zilishinikizwa na kufanywa laini zilipakwa kwenye jipu lililohatarisha maisha ya Mfalme Hezekia, ingawa baadaye Mungu hasa ndiye aliyemponya. *—2 Wafalme 20:4-7.
Zamani, tini zilizokaushwa zilithaminiwa sana kotekote Mediterania. Mwanasiasa mashuhuri Cato aliwaonyesha wabunge wa Roma tini ili kuwashawishi wakubali kuanzishwa kwa Vita vya Tatu dhidi ya Carthage. Tini bora zilizokaushwa ambazo zilipatikana Roma zilitoka Caria, huko Asia Ndogo. Hivyo, carica likawa jina la Kilatini la tini zilizokaushwa. Eneo hilo ambalo sasa ni Uturuki bado huzalisha tini bora zilizokaushwa.
Mara nyingi wakulima Waisraeli walipanda mitini katika mashamba ya mizabibu, lakini mitini isiyozaa ilikatwa. Walifanya hivyo kwa kuwa sehemu zilizokuwa na udongo wenye rutuba zilikuwa chache. Katika mfano wa Yesu kuhusu mtini usiozaa, mkulima alimwambia mtunza-mizabibu hivi: “Sasa ni miaka mitatu ambayo nimekuja nikitafuta matunda juu ya mtini huu, lakini sijapata yoyote. Ukate! Kwa kweli kwa nini huo uiweke nchi bila mafaa?” (Luka 13:6, 7) Kwa kuwa wakati wa Yesu miti ya matunda ililipiwa kodi, mti wowote usiozaa ungekuwa mzigo kifedha.
Tini zilikuwa sehemu muhimu sana ya chakula cha Waisraeli. Kwa hiyo, mavuno mabaya ya tini—ambayo yamkini yalisababishwa na hukumu kali ya Yehova—yangeleta msiba. (Hosea 2:12; Amosi 4:9) Nabii Habakuki alisema: “Maana mtini hautachanua maua, wala mizabibuni hamtakuwa na matunda; taabu ya mzeituni itakuwa bure, na mashamba hayatatoa chakula . . walakini nitamfurahia BWANA nitamshangilia Mungu wa wokovu wangu.”—Habakuki 3:17, 18.
Mfano wa Taifa Lisilo na Imani
Nyakati nyingine, Biblia hutumia tini au mitini kwa njia ya mfano. Kwa mfano, Yeremia aliwalinganisha Wayahudi waaminifu waliohamishwa kutoka Yuda, na kikapu cha tini nzuri. Hizo zilikuwa tini za mapema ambazo kwa kawaida zililiwa kabla ya kukaushwa. Hata hivyo, Wayahudi wasio waaminifu ambao walihamishwa walilinganishwa na tini mbovu, ambazo hazingeweza kuliwa ila kutupwa.—Yeremia 24:2, 5, 8, 10.
Katika mfano wake wa mtini usiozaa, Yesu alionyesha jinsi Mungu alivyoonyesha taifa la Wayahudi subira. Kama ilivyotajwa, Yesu alizungumza kuhusu mtu fulani aliyekuwa na mtini katika shamba lake la mizabibu. Mti huo haukuwa umezaa kwa miaka mitatu, na mwenye shamba alitaka ukatwe. Lakini mtunza-mizabibu akasema: “Bwana-mkubwa, Luka 13:8, 9.
uuache mwaka huu pia, mpaka nilime kuuzunguka na kuweka mbolea; na ndipo ukitokeza matunda wakati ujao, basi ni vema; lakini ikiwa sivyo, hakika utaukata.”—Yesu alipotoa mfano huo, alikuwa amehubiri kwa miaka mitatu, akijitahidi kulisaidia taifa la Wayahudi lisitawishe imani. Yesu alizidisha juhudi zake, “akiweka mbolea” kwenye mti huo wa mfano, yaani, taifa la Wayahudi—na kulipatia fursa ya kuzaa matunda. Hata hivyo, juma moja kabla ya kifo cha Yesu, ilionekana wazi kwamba taifa hilo kwa jumla lilikuwa limemkataa Mesiya.—Mathayo 23:37, 38.
Yesu alitumia tena mfano wa mtini ili kuonyesha hali mbaya ya kiroho ya taifa hilo. Alipokuwa akisafiri kutoka Bethania kwenda Yerusalemu, siku nne kabla ya kifo chake, aliona mtini uliokuwa na majani mengi lakini haukuwa na matunda yoyote. Kwa kuwa tini za mapema hutokea wakati mmoja na majani—nyakati nyingine hata kabla ya majani kutokea—mti huo haukuwa na faida yoyote kwa sababu haukuwa na matunda.—Marko 11:13, 14. *
Kama vile mtini usiozaa ulivyoonekana kuwa unasitawi, taifa la Wayahudi lilionekana tofauti na lilivyokuwa. Lakini taifa hilo halikuwa limezaa matunda yanayompendeza Mungu, na hatimaye likamkataa Mwana wa Yehova mwenyewe. Yesu aliulaani mtini huo usiozaa, na siku iliyofuata wanafunzi wake wakaona kwamba ulikuwa umenyauka. Mti huo uliokauka ulifananisha ifaavyo jinsi ambavyo Mungu angekuja kuwakataa Wayahudi waliokuwa watu wake wateule.—Marko 11:20, 21.
‘Jifunzeni Kutokana na Mtini’
Yesu pia alitumia mtini kufundisha jambo muhimu kuhusu kuwapo kwake. Alisema: “Jifunzeni jambo hili kutokana na mtini kama kielezi: Mara tu tawi lao changa likuapo kuwa jororo na kutoa majani, mwajua kwamba kiangazi kiko karibu. Hivyohivyo nyinyi pia, mwonapo mambo yote hayo, jueni kwamba yuko karibu milangoni.” (Mathayo 24:32, 33) Majani ya mtini yenye rangi nyangavu ya kijani kibichi huonekana kwa urahisi na ni ishara wazi ya kuanza kwa majira ya kiangazi. Vivyo hivyo, unabii muhimu wa Yesu kwenye kitabu cha Mathayo sura ya 24, Marko sura ya 13, na Luka sura ya 21 hutoa uthibitisho wa kuwapo kwake sasa akiwa mtawala wa Ufalme wa mbinguni.—Luka 21:29-31.
Kwa kuwa tunaishi katika wakati huu muhimu katika historia, bila shaka tungependa kujifunza kutokana na mtini. Tukifanya hivyo na kuendelea kuwa macho kiroho, tunakuwa na tumaini la kuona utimizo wa ahadi hii tukufu: “Wataketi kila mtu chini ya mzabibu wake, na chini ya mtini wake; wala hapana mtu atakayewatia hofu; kwa kuwa kinywa cha BWANA wa majeshi kimesema hivi.”—Mika 4:4.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 8 H. B. Tristram, mtaalamu wa mimea na viumbe ambaye alizuru nchi zinazotajwa katika Biblia katikati ya karne ya 19, alisema kwamba watu wa huko bado hutumia tini zilizoshinikizwa na kufanywa laini kutibu majipu.
^ fu. 16 Kisa hiki kilitukia karibu na kijiji cha Bethfage. Jina la kijiji hicho linamaanisha “Nyumba ya Tini za Mapema.” Huenda jambo hilo likaonyesha kwamba kijiji hicho kilikuwa maarufu kwa mavuno mazuri ya tini za mapema.