Maandishi Yenye Kuvutia Sana
Maandishi Yenye Kuvutia Sana
KUANZIA mwaka wa 1928 hadi 1956 mvumbuzi Richard E. Byrd alisafiri barani Antaktika mara tano. Kwa kuwa aliandika habari sahihi kuhusu safari zake, yeye na wenzake waliweza kujua mkondo wa upepo, wakachora ramani, na kukusanya habari nyingi kuhusu bara la Antaktika.
Safari za Byrd zinaonyesha umuhimu wa kuhifadhi maandishi kuhusu safari. Kwa kweli, marubani wanapaswa kuandika kuhusu safari za ndege, ilhali manahodha wanapaswa kuandika kuhusu safari za meli. Baadaye, habari hizo zinaweza kutumiwa kuchunguza mambo yaliyotukia au kuchanganua habari zinazoweza kutumiwa wakati ujao.
Maandiko yana masimulizi yenye kuvutia kuhusu Gharika ya siku za Noa. Gharika hiyo ilichukua muda unaozidi mwaka mmoja. Ili kujitayarisha kwa ajili ya Gharika hiyo, Noa, mke wake, na watoto wake watatu wa kiume, pamoja na wake zao, walijenga safina kwa muda wa miaka 50 au 60. Safina hiyo ilikuwa na ukubwa wa meta 133.5 x 22.3 x 13.4. Ilikuwa ya kazi gani? Ya kuhifadhi wanadamu na wanyama wasiharibiwe na Gharika.—Mwanzo 7:1-3.
Kitabu cha Biblia cha Mwanzo kina maandishi ya Noa kuhusu mambo yaliyotukia tangu Gharika ilipoanza hadi yeye na familia yake walipotoka ndani ya safina. Je, maandishi hayo yana maana yoyote kwetu leo?