Yale Ambayo Ndege Wanaweza Kutufunza
Yale Ambayo Ndege Wanaweza Kutufunza
“WAANGALIENI kwa mkazo ndege wa mbinguni, kwa sababu hawapandi mbegu au kuvuna au kukusanya ghalani; na bado Baba yenu wa kimbingu huwalisha wao. Je, nyinyi si bora kuliko wao?” (Mathayo 6:26) Yesu Kristo alisema maneno hayo katika mahubiri yake yenye kujulikana sana kando ya mlima karibu na Bahari ya Galilaya. Zaidi ya wafuasi wake, kulikuwa na wasikilizaji wengine. Umati mkubwa wa watu ambao wangeweza kuwa wafuasi wake walikuwapo kutoka sehemu zote za nchi. Wengi wao walikuwa maskini waliomletea Yesu wagonjwa wao ili awaponye.—Mathayo 4:23–5:2; Luka 6:17-20.
Baada ya kuwatibu wagonjwa wote, Yesu alikazia fikira mahitaji muhimu zaidi ya kiroho. Kati ya mambo aliyowafundisha moja limetajwa hapo juu.
Ndege wa mbinguni wamekuwapo kwa muda mrefu. Baadhi yao hula wadudu na wengine hula matunda na mbegu. Ikiwa Mungu amewapa ndege chakula kingi hivyo, bila shaka anaweza kuwasaidia watumishi wake wapate chakula cha kila siku. Anaweza kufanya hivyo kwa kuwasaidia kupata kazi ili wapate pesa za kununua chakula. Au anaweza kuwasaidia wafanikiwe kupata mavuno mazuri. Hali za dharura zinapotokea, Mungu anaweza kuwachochea majirani na marafiki wenye fadhili wawagawie chakula wenye uhitaji.
Tunaweza kujifunza mengi zaidi kwa kuwatazama ndege kwa makini. Mungu amewaumba ndege wakiwa na silika yenye kustaajabisha inayowawezesha kujenga viota vya kuwalea watoto wao. Ona aina mbili za viota. Upande wa kushoto kuna picha ya kiota cha ndege anayeitwa kinegwa-mwekundu. Kiota hicho kimejengwa kwenye ukingo wa mwamba au juu ya ukuta wa nyumba. Paa ya viota hivyo huwa ni sehemu iliyochomoza ya mwamba au kama inavyoonyeshwa katika picha hii, pembe za paa la nyumba. Sakafu ya kiota imetengenezwa kwa vipande vidogo vya matope vilivyounganishwa pamoja na kufanya kiota kiwe na umbo la kikombe. Ndege wa kiume na wa kike hufanya kazi kwa bidii kukusanya vipande vidogo vya matope na huenda ikawachukua mwezi mmoja hivi kukamilisha kujenga kiota chao. Kisha wanafunika sehemu ya ndani kwa nyasi na manyoya. Wote wawili hushiriki kuwalisha watoto wao. Hapa chini kuna kiota cha ndege anayeitwa nguya wa jamii ya nyomvi. Ndege huyo mwenye bidii wa Afrika hujenga kiota chake kwa kutumia nyasi au magamba ya mimea mingine. Ndege huyo anaweza kukamilisha kujenga kiota chake kwa muda wa siku moja na anaweza kusokota viota zaidi ya 30 kwa kipindi fulani cha mwaka!
Tunajifunza nini? Ikiwa Mungu huwapa ndege ustadi na vifaa vingi vya kujenga viota, bila shaka anaweza kuwasaidia watumishi wake kupata makao wanayohitaji. Hata hivyo, Yesu alionyesha kwamba kuna kitu kingine cha lazima iwapo tunataka Yehova Mungu atusaidie kupata mahitaji yetu ya kimwili. Yesu aliahidi hivi: “Basi, fulizeni kutafuta kwanza ufalme na uadilifu wake, na vitu vingine vyote hivi mtaongezewa.” (Mathayo 6:33) Huenda ukajiuliza, ‘Ni nini kinachohusika katika kutafuta kwanza Ufalme wa Mungu?’ Mashahidi wa Yehova ambao hugawa gazeti hili watafurahi kujibu swali hilo.