Kuwatumikia Wengine Hupunguza Mateso
Simulizi la Maisha
Kuwatumikia Wengine Hupunguza Mateso
LIMESIMULIWA NA JULIÁN ARIAS
Katika mwaka wa 1988, nilipokuwa na umri wa miaka 40, kazi yangu ilionekana kuwa ya kudumu. Nilikuwa mkurugenzi wa mkoa wa kampuni moja ya kimataifa ambayo ilinipa gari, mshahara mnono, na ofisi maridadi katikati ya jiji la Madrid, nchini Hispania. Kampuni hiyo hata ilidokeza kwamba ingenipandisha cheo kuwa mkurugenzi wao wa kitaifa. Sikujua kamwe kwamba maisha yangu yangebadilika ghafula.
SIKU moja mwaka huohuo, daktari wangu aliniambia kwamba nina ugonjwa wa neva usio na tiba. Nilifadhaika na baadaye niliposoma namna ugonjwa huo unavyoweza kumwathiri mtu, niliogopa. * Ilionekana kwamba ningelazimika kuishi maisha yangu yote kwa woga. Nitamtunzaje mke wangu Milagros, na mwana wangu Ismael mwenye umri wa miaka mitatu? Tutakabilianaje na hali hii? Kabla ya kupata majibu kwa maswali hayo, nilipata pigo lingine baya.
Mwezi mmoja baada ya daktari kuniambia kuhusu ugonjwa wangu, msimamizi wangu kazini aliniita ofisini mwake na kuniambia kwamba kampuni ilihitaji watu wenye “sura ya kuvutia.” Na mtu aliye na ugonjwa wenye kudhoofisha—hata unapoanza tu—hawezi kuvutia. Basi, papo hapo msimamizi wangu akanifuta kazi. Ghafula, nikapoteza kazi yangu!
Nikiwa na familia yangu, nilijitahidi nionekane jasiri, lakini nilitamani sana kuwa peke yangu, nifikirie hali yangu mpya na wakati wangu ujao.
Nilijitahidi sana kuepuka hisia za kushuka moyo. Kilichoniumiza hata zaidi ni kwamba, kwa ghafula kampuni yangu iliniona kuwa sifai kitu.Nina Nguvu Nijapokuwa Dhaifu
Ninashukuru kwamba wakati huu wa shida, kuna mambo mengi yanayonitia nguvu. Nilikuwa nimekuwa Shahidi wa Yehova kwa miaka 20. Kwa hiyo nilisali kwa Yehova kwa unyofu kuhusu hisia zangu na mahangaiko yangu ya wakati ujao. Mke wangu ambaye pia ni Shahidi wa Yehova, alinitegemeza sana, nao marafiki wangu wa karibu wenye fadhili na huruma walinitegemeza na kunitia moyo sana.—Mithali 17:17.
Kuhisi kwamba nina daraka la kuwasaidia wengine kulinisaidia pia. Nilitaka kumlea mwana wangu vizuri, kumfundisha, kucheza naye, na kumzoeza kuhubiri. Kwa hiyo, singekata tamaa. Isitoshe, nilikuwa mzee katika kutaniko moja la Mashahidi wa Yehova, na ndugu na dada zangu Wakristo kutanikoni walihitaji msaada wangu. Ningewawekea wengine kielelezo gani kama ningeruhusu matatizo yadhoofishe imani yangu?
Bila shaka maisha yangu yalibadilika kimwili na kiuchumi—kwa njia moja mabadiliko hayo yalifanya maisha yangu kuwa mabaya na kwa njia nyingine yakayaboresha. Wakati mmoja nilimsikia daktari akisema: “Ugonjwa haumharibu mtu; bali, humbadili.” Na nimejifunza kwamba si mabadiliko yote huwa mabaya.
Kwanza kabisa, “mwiba katika mwili” wangu ulinisaidia kuelewa vizuri matatizo ya kiafya ya wengine na kuwahurumia. (2 Wakorintho 12:7) Nilielewa vizuri zaidi maneno haya ya Mithali 3:5: “Mtumaini BWANA kwa moyo wako wote, wala usizitegemee akili zako mwenyewe.” Zaidi ya hayo, hali yangu mpya ilinisaidia kujua mambo ambayo ni muhimu maishani na yanayoleta uradhi wa kweli na kufanya tujiheshimu. Bado ningeweza kufanya mengi katika tengenezo la Yehova. Nilielewa maana halisi ya maneno haya ya Yesu: “Kuna furaha zaidi katika kutoa kuliko kulivyo katika kupokea.”—Matendo 20:35.
Maisha Mapya
Punde baada ya ugonjwa wangu kugunduliwa, nilialikwa kuhudhuria semina moja iliyofanywa Madrid ambapo wajitoleaji Wakristo walifundishwa kukuza ushirikiano kati ya madaktari na wagonjwa ambao ni Mashahidi. Baadaye, wajitoleaji hao walipangwa kuwa vikundi vya Halmashauri ya Uhusiano na Hospitali. Kwangu mimi, semina hiyo ilikuwa ya wakati unaofaa. Nilipata kazi bora ambayo ingeniridhisha zaidi kuliko kazi yoyote ya kuajiriwa.
Katika semina hiyo tulijifunza kwamba washiriki hao wapya wa Halmashauri ya Uhusiano na Hospitali wangetembelea hospitali, wawahoji madaktari, na kuzungumza na wafanyakazi wa hospitali, ili kukuza uhusiano mzuri na kuepuka kutoelewana. Halmashauri hizo huwasaidia Mashahidi wenzao kupata madaktari wanaoweza kuwatibu bila kutumia damu. Kwa kuwa mimi si mtaalamu wa kitiba, nilikuwa na mengi ya kujifunza kuhusu lugha ya kitiba, kanuni za kitiba, na utaratibu wa hospitali. Hata hivyo, semina hiyo ilibadili maoni yangu na kunitayarisha kwa ajili ya mgawo mpya nilioufurahia sana.
Kutembelea Watu Hospitalini Kunaridhisha
Madaraka yangu nikiwa mshiriki wa Halmashauri ya Uhusiano na Hospitali yaliongezeka ijapokuwa ugonjwa wangu uliendelea tu kunilemaza. Kwa kuwa nilikuwa nikipokea malipo ya walemavu, nilikuwa na fursa ya kutembe
lea hospitali mbalimbali. Licha ya mambo yenye kuvunja moyo, wakati mwingine ziara hizo zilikuwa rahisi na zenye kuthawabisha kuliko nilivyotazamia. Ijapokuwa sasa ninalazimika kutumia kiti cha magurudumu, sijapata tatizo kubwa. Kila wakati mimi huandamana na mshiriki mwenzangu wa halmashauri. Isitoshe, madaktari wamezoea kuzungumza na watu wanaotumia viti vya magurudumu, na wakati mwingine wao husikiliza kwa heshima wanapoona jinsi ninavyojitahidi kuwatembelea.Kwa zaidi ya miaka kumi sasa, nimewatembelea madaktari wengi sana. Baadhi yao walikuwa tayari kutusaidia. Dakt. Juan Duarte, mpasuaji wa moyo huko Madrid anayependa kuheshimu dhamiri ya wagonjwa, alijitolea mara moja kutuhudumia. Tangu wakati huo amefanya upasuaji bila kutumia damu zaidi ya mara 200, upasuaji ambao unahusisha wagonjwa walio Mashahidi kutoka sehemu mbalimbali za Hispania. Kwa miaka kadhaa sasa madaktari wengi wameanza kufanya upasuaji bila kutumia damu. Ziara zetu za kawaida zimechangia sana, na pia kumekuwa na mafanikio kwa sababu ya maendeleo ya kitiba na matokeo mazuri ya upasuaji bila kutumia damu. Na tuna hakika kwamba Yehova amebariki jitihada zetu.
Nimetiwa moyo sana hasa na itikio la madaktari fulani wanaopasua moyo ambao ni wataalamu wa kutibu watoto. Kwa miaka miwili tulitembelea kikundi cha madaktari wawili na wataalamu wao wa dawa za kumfanya mgonjwa apoteze fahamu wakati wa upasuaji. Tuliwapa vitabu vya kitiba vilivyoonyesha yale ambayo madaktari wengine wanafanya kuhusiana na suala hilo. Mwaka wa 1999, jitihada zetu zilithawabishwa wakati wa Mkutano wa Kitiba Kuhusu Upasuaji wa Moyo kwa Watoto. Madaktari hao wawili wakielekezwa na daktari-mpasuaji kutoka Uingereza, walifanya upasuaji mgumu sana kwa mtoto wa Shahidi ambaye mshipa wake mkubwa wa kupeleka damu moyoni ulihitaji kufanyiwa marekebisho. * Nilifurahi pamoja na wazazi wa mtoto huyo wakati daktari alipotoka katika chumba cha upasuaji na kusema kwamba upasuaji umefaulu na uamuzi wa familia hiyo umeheshimiwa. Sasa madaktari hao huwakubali kwa ukawaida wagonjwa ambao ni Mashahidi kutoka kotekote Hispania.
Jambo linaloniridhisha kikweli kuhusu visa kama hivyo ni kujua kwamba ninaweza kuwasaidia ndugu zangu Wakristo. Kwa kawaida, wao huwasiliana na Halmashauri ya Uhusiano na Hospitali wanapokabiliana na hali ngumu sana maishani. Wao huhitaji kupasuliwa, nao madaktari katika maeneo yao hukataa au hawawezi kuwatibu bila kutumia damu. Hata hivyo, ndugu wanapojua kwamba hapa Madrid kuna madaktari-wapasuaji katika nyanja mbalimbali za kitiba na ambao wako tayari kusaidia, wanafurahi sana. Nimeona ndugu akiacha kuwa na hangaiko na kuanza kutulia, kwa kuwa tu tulikuwa kando yake hospitalini.
Mahakimu na Maadili ya Kitiba
Katika miaka ya karibuni, washiriki wa Halmashauri ya Uhusiano na Hospitali wamewatembelea mahakimu pia. Katika ziara hizo
tunawapa kichapo Family Care and Medical Management for Jehovah’s Witnesses, ambacho kilitayarishwa hasa ili kuwaarifu wataalamu hao kuhusu msimamo wetu juu ya matumizi ya damu na kuwapo kwa matibabu mengine yasiyohusisha damu. Ziara hizo zilihitajiwa sana, kwa kuwa wakati mmoja lilikuwa jambo la kawaida nchini Hispania kwa mahakimu kuwaidhinisha madaktari wamtie mgonjwa damu kinyume cha mapenzi yake.Kumbi za mahakimu ni kubwa, na katika ziara yangu ya kwanza, nilijiona kuwa mtu asiye na maana nikipita kwenye vijia nikiwa katika kiti changu cha magurudumu. Isitoshe, tulipata aksidenti ndogo, nikaanguka kutoka kitini na kuangukia magoti yangu. Mahakimu na wanasheria wachache walioona hali yangu walikuja kunisaidia kwa fadhili, lakini niliaibika sana mbele yao.
Ingawa mahakimu hawakujua kusudi letu la kuwatembelea, wengi walitutendea kwa fadhili. Hakimu wa kwanza niliyemtembelea alikuwa tayari anatafakari msimamo wetu, na alisema kwamba angependa kuzungumza zaidi pamoja nasi. Katika ziara yetu iliyofuata, yeye alinisukuma nikiwa katika kiti changu cha magurudumu hadi kwenye ukumbi wake na akatusikiliza kwa makini. Matokeo mazuri ya ziara hiyo ya kwanza yalinitia moyo mimi na wenzangu kushinda woga wetu, na punde tukaanza kuona matokeo zaidi mazuri.
Mwaka huohuo, tulimpa nakala ya Family care hakimu mwingine aliyetupokea kwa fadhili naye akaahidi kuisoma. Nilimpa namba yangu ya simu iwapo angehitaji kuwasiliana nasi wakati wa dharura. Majuma mawili baadaye alipiga simu kusema kwamba daktari mmoja mpasuaji amemwomba atoe idhini ya kumtia damu Shahidi mmoja aliyehitaji upasuaji. Hakimu huyo alituambia kwamba alitaka tumsaidie kupata suluhisho ambalo lingeheshimu ombi la Shahidi huyo la kuepuka kutumia damu. Haikuwa vigumu kupata hospitali nyingine, ambapo madaktari walifanya upasuaji huo kwa mafanikio bila kutumia damu. Hakimu huyo alifurahi aliposikia matokeo hayo, naye akatuahidi kwamba atatafuta suluhisho kama hilo wakati ujao.
Katika ziara zangu hospitalini, mara nyingi swali la maadili ya kitiba lilizuka kwa kuwa tulitaka madaktari wafikirie haki na dhamiri ya mgonjwa. Hospitali moja huko Madrid ilinialika kuhudhuria masomo ya maadili ya kitiba.
Masomo hayo yaliniwezesha kutoa hotuba mbele ya wataalamu wengi wa kitiba kuhusu maoni yetu yanayotegemea Biblia. Yalinisaidia pia kuelewa maamuzi mengi magumu ambayo madaktari hulazimika kufanya.Mwalimu mmoja wa masomo hayo, Profesa Diego Gracia, ambaye kwa kawaida huwapangia madaktari wa Hispania masomo ya hali ya juu kuhusu maadili ya kitiba, amekuwa mtetezi imara wa haki yetu ya kutaka kuarifiwa kuhusu masuala ya utiaji damu. * Kwa sababu ya mawasiliano yetu ya kawaida pamoja naye, wawakilishi wa ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova ya Hispania walialikwa ili kuwaeleza msimamo wetu wanafunzi wa Profesa Gracia wa shahada ya juu, ambao baadhi yao wanaonwa kuwa madaktari bora nchini.
Kukabili Hali Halisi
Ni kweli kwamba kazi hii yenye kuridhisha kwa niaba ya waamini wenzangu haijasuluhisha matatizo yangu yote. Ugonjwa wangu unaendelea tu kunidhoofisha. Lakini ninafurahi kwamba akili yangu ni timamu. Bado ninaweza kushughulikia madaraka yangu na ninamshukuru mke wangu na mwana wangu ambao hawalalamiki kamwe. Bila wao kunisaidia na kuniunga mkono singetimiza mambo hayo. Hata siwezi kufunga suruali au kujivisha koti. Hasa ninafurahia kuhubiri kila Jumamosi pamoja na mwana wangu Ismael, ambaye hunisukuma ili niweze kuzungumza na watu mbalimbali. Na bado ninaweza kushughulikia madaraka yangu nikiwa mzee wa kutaniko.
Katika kipindi cha miaka 12 hivi iliyopita, nimepatwa na pindi zenye kutaabisha sana. Wakati mwingine kuona namna ugonjwa wangu umeathiri familia yangu, kunaniumiza zaidi kuliko ugonjwa wenyewe. Ijapokuwa hawasemi, ninajua kwamba wanateseka. Hivi karibuni, katika kipindi cha mwaka mmoja, mama-mkwe wangu na baba yangu walikufa. Mwaka huohuo, singeweza kwenda popote bila kutumia kiti cha magurudumu. Baba yangu aliyekuwa anaishi nasi, aliugua ugonjwa mwingine wenye kudhoofisha na akafa. Milagros, ambaye alikuwa akimtunza alihisi kana kwamba anashuhudia yale ambayo yatanipata wakati ujao.
Hata hivyo, familia yetu ina umoja na tunakabiliana na magumu hayo pamoja. Badala ya kuwa na kiti cha cheo kazini, sasa ninatumia kiti cha magurudumu, lakini maisha yangu ni bora sasa kwa kuwa nimejitolea kuwatumikia wengine. Kutumia wakati na jitihada kwa niaba ya wengine kunaweza kupunguza mateso, na kulingana na ahadi yake, Yehova hutuimarisha wakati tunapokuwa na uhitaji. Kwa kweli ninaweza kusema hivi kama Paulo: “Kwa mambo yote ninayo nguvu kwa njia ya yeye anipaye nguvu.”—Wafilipi 4:13.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 5 Ugonjwa wa neva hudhuru ubongo na uti wa mgongo. Hatua kwa hatua ugonjwa huo hudhoofisha usawaziko wa mwili, miguu na mikono, na wakati mwingine hudhoofisha uwezo wa kuona, wa usemi, au ufahamu.
^ fu. 19 Upasuaji huu unaitwa utaratibu wa Ross.
^ fu. 27 Ona gazeti la Mnara wa Mlinzi, la Februari 15, 1997, ukurasa wa 19-20.
[Sanduku katika ukurasa wa 24]
Maoni ya Mke
Kuishi na mwenzi anayeugua ugonjwa wa neva ni jambo linaloumiza mke kiakili, kihisia, na kimwili. Ni lazima nipange mambo ninayotaka kufanya kwa busara na niepuke mahangaiko yasiyo ya lazima kuhusu wakati ujao. (Mathayo 6:34) Hata hivyo mateso yanaweza kufunua sifa bora za mtu. Ndoa yetu imeimarika kuliko zamani, nami nina uhusiano wa karibu zaidi na Yehova. Nimeimarishwa sana pia na masimulizi ya maisha ya wengine walio katika hali kama hii yenye kufadhaisha. Kama Julián, ninahisi nikiwa nimeridhika kwa sababu ya utumishi wake wenye thamani kwa niaba ya akina ndugu, na nimeona kwamba Yehova hatuachi kamwe, ijapokuwa huenda kila siku ikawa na magumu yake.
[Sanduku katika ukurasa wa 24]
Maoni ya Mwana
Uvumilivu wa baba yangu na mtazamo wake unaofaa umeniwekea kielelezo bora, nami ninahisi ninatoa msaada ninapomsukuma akiwa katika kiti chake cha magurudumu. Ninajua kwamba wakati wote siwezi kufanya nipendavyo. Sasa mimi ni tineja, lakini nitakapokuwa mkubwa, ningependa kuwa mshiriki wa Halmashauri ya Uhusiano na Hospitali. Kulingana na ahadi ya Biblia ninajua kwamba mateso ni ya muda tu na kwamba ndugu na dada wengi wanateseka zaidi kuliko sisi.
[Picha katika ukurasa wa 22]
Mke wangu huniimarisha
[Picha katika ukurasa wa 23]
Nikizungumza na Dakt. Juan Duarte, mpasuaji wa moyo
[Picha katika ukurasa wa 25]
Mimi na mwana wangu hufurahia kuhubiri pamoja