Ni Nini Kilichoyapata Majiji ya Nofu na No?
Ni Nini Kilichoyapata Majiji ya Nofu na No?
NOFU na No ni majina ya majiji ya Memfisi na Thebesi yanayopatikana katika Biblia, ambayo yalikuwa maarufu sana nchini Misri. Nofu (Memfisi) lilikuwa kilometa 23 hivi kusini ya Cairo, upande wa kaskazini ya Mto Nile. Hata hivyo, mwishowe, Memfisi likakoma kuwa jiji kuu la Misri. Mwanzoni mwa karne ya 15 K.W.K., No (Thebesi) jiji lililokuwa karibu kilometa 500 kusini ya Nofu likawa jiji kuu la Misri. Miongoni mwa magofu mengi ya mahekalu ya Thebesi ni yale ya hekalu la Karnak, ambalo linadhaniwa kuwa jengo kubwa zaidi lililowahi kujengwa kwa nguzo. Thebesi na hekalu lake Karnak liliwekwa wakfu kwa ibada ya Amoni, mungu mkuu wa Wamisri.
Unabii wa Biblia ulitabiri nini kuhusu Memfisi na Thebesi? Ulitabiri kuhukumiwa kwa Farao wa Misri na miungu yake, hasa mungu wake mkuu, “Amoni na No.” (Yeremia 46:25, 26) Umati wa waabudu waliomiminika huko ‘wangekatiliwa mbali.’ (Ezekieli 30:14, 15) Na hivyo ndivyo ilivyokuwa. Hakuna chochote kinachosalia kuhusiana na ibada ya Amoni isipokuwa magofu ya hekalu lake. Mji wa kisasa wa Luxor upo upande mmoja wa lililokuwa jiji la Thebesi la kale, na vijiji vingine vidogo vinapatikana miongoni mwa magofu yake.
Kwa habari ya Memfisi, hakuna kilichosalia ila tu makaburi yake. Msomi wa Biblia Louis Golding anasema: “Kwa karne nyingi Waarabu washindi kutoka Misri walichimba mawe kutoka magofu makubwa ya Memfisi ili kujenga jiji kuu la [Cairo] ng’ambo ya mto. Wajenzi hao Waarabu walichimba sana na baadaye mchanga wa Nile ukalifunika jiji hilo la zamani hivi kwamba hakuna jiwe linalotokeza juu ya udongo mweusi kilometa nyingi kulizunguka.” Kwa hakika kama vile Biblia ilivyotabiri, Memfisi likawa ‘ukiwa . . . lisilokaliwa na watu.’—Yeremia 46:19.
Hii ni mifano miwili tu kati ya mifano mingi inayoonyesha kwamba unabii wa Biblia ni sahihi. Uharibifu wa Thebesi na Memfisi unatuchochea kuweka tumaini katika unabii wa Biblia ambao haujatimizwa bado.—Zaburi 37:10, 11, 29; Luka 23:43; Ufunuo 21:3-5.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 32]
Photograph taken by courtesy of the British Museum