Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Maskini Wanazidi Kuwa Maskini

Maskini Wanazidi Kuwa Maskini

Maskini Wanazidi Kuwa Maskini

“Hakuna jamii inayoweza kusitawi na kuwa na furaha iwapo idadi kubwa ya raia zake ni maskini na hawana furaha.”

MANENO hayo yalisemwa na mtaalamu wa uchumi, Adam Smith katika karne ya 18. Wengi wanasadiki kwamba ukweli wa yale aliyosema unaonekana wazi zaidi leo. Tofauti kati ya matajiri na maskini inaonekana wazi zaidi. Huko Ufilipino, theluthi moja ya watu hujitegemeza kwa kiasi kinachopungua dola moja ya Marekani kwa siku, kiasi ambacho mara nyingi huchumwa kwa dakika chache katika mataifa tajiri. Kichapo cha Umoja wa Mataifa, Human Development Report 2002 kinasema kwamba “mapato ya asilimia 5 ya watu matajiri sana ulimwenguni ni mara 114 zaidi ya asilimia 5 ya wale walio maskini sana.”

Ingawa watu fulani wanaishi maisha ya starehe, mamilioni huishi wakiwa maskwota, wakijenga nyumba za mabanda mahali popote. Hali ya wengine ni mbaya zaidi; wanaishi barabarani, wakiwa wamelalia na kujifunika tu makaratasi. Wengi wao hujitegemeza kwa njia yoyote ile—huchakura takataka, hubeba mizigo mizito, au hutumia mikokoteni kuokota takataka wanazoweza kuuza kama vile makaratasi, mikebe na chupa.

Ukosefu wa usawa kati ya matajiri na maskini hauko tu katika nchi zinazositawi, bali kama vile Benki ya Dunia inavyosema ‘kuna maskini katika nchi zote.’ Hata kama wengine ni matajiri sana, iwe ni huko Bangladesh au Marekani, kuna wale ambao wanashindwa kujipatia chakula cha kutosha na makao. Likinukuu ripoti ya Shirika la Marekani la Sensa ya 2001, gazeti The New York Times lilionyesha kwamba pengo kati ya matajiri na maskini huko Marekani linazidi kupanuka. Lilisema hivi: “Asilimia 20 ya watu walio matajiri sana ilipokea nusu ya mapato ya familia zote mwaka jana . . . Asilimia 20 ya walio maskini sana ilipokea asilimia 3.5.” Hali iko hivyo au ni mbaya hata zaidi katika nchi nyingine nyingi. Ripoti moja ya Benki ya Dunia inaonyesha kwamba asilimia 57 ya watu ulimwenguni hujitegemeza kwa kiasi kinachopungua dola mbili kwa siku.

Kufanya hali iwe mbaya hata zaidi, katika mwaka wa 2002, watu wengi walikerwa na ripoti kuhusu wasimamizi wa makampuni ambao walitajirika kwa njia zenye kutiliwa shaka. Hata kama utajiri huo ulipatikana kwa njia halali, wengi wamehisi kwamba wasimamizi hao wa makampuni “walikuwa matajiri kupita kiasi, bila kujali wengine,” kama lilivyosema gazeti Fortune. Kwa kufikiria yale yanayotukia ulimwenguni, wengine hujiuliza kama kweli ni haki kwa watu fulani kuwa na pesa nyingi mno, ambazo zinakadiriwa kuwa mamilioni ya dola, huku wengine wakiishi katika umaskini.

Je, Umaskini Utakuwapo Milele?

Hii haimaanishi kwamba hakuna mtu anayefikiria kuwasaidia maskini. Bila shaka, maofisa wa serikali wenye nia nzuri na mashirika ya kutoa misaada yametoa mapendekezo ya kuleta mabadiliko. Hata hivyo, hali bado inasikitisha. Kichapo Human Development Report 2002 kinasema kwamba “nchi nyingi ni maskini kuliko zilivyokuwa miaka 10, 20 na katika visa vingine, miaka 30 iliyopita,” licha ya jitihada nzuri za kuboresha mambo.

Je, hii inamaanisha kwamba maskini hawana tumaini lolote? Tunakukaribisha usome makala inayofuata ili uone jinsi kuwa na hekima kunavyoweza kuwasaidia maskini sasa na pia suluhisho ambalo labda hujawahi kulifikiria.