Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

“Miti ya Yehova Imeshiba”

“Miti ya Yehova Imeshiba”

Fahari ya Uumbaji wa Yehova

Miti ya Yehova Imeshiba”

JE, UMEWAHI kusimama msituni huku miale ya jua ikipenyeza katikati ya miti mirefu? Je, ungeweza kusikia upepo ukivuma katikati ya majani?—Isaya 7:2.

Katika kipindi fulani cha mwaka, majani ya miti mbalimbali katika maeneo fulani duniani hubadilika rangi na kuwa mekundu, ya rangi ya machungwa, manjano, na kadhalika. Ni kana kwamba misitu imewashwa moto! Hali hiyo inapatana na wazo hili: “Changamkeni, ninyi milima, kwa vigelegele vya shangwe, Ee msitu nanyi miti yote mlio ndani yake!”—Isaya 44:23. *

Karibu sehemu moja ya tatu ya nchi kavu ya sayari ina misitu. Misitu na viumbe wengi walio hai ambao wanaishi humo humtukuza Yehova Mungu, aliye Mbuni na Muumba kwa njia nzuri sana. Mtunga-zaburi aliongozwa na roho ya Mungu kuimba: “Msifuni Yehova . . . enyi miti ya matunda, nanyi mierezi yote.”—Zaburi 148:7-9.

Kitabu The Trees Around Us kinasema, “Miti ni muhimu kwa ajili ya mahitaji ya kimwili ya mwanadamu na tamaa yake ya kuona umaridadi wa vitu.” Misitu hulinda, hutegemeza, na kusafisha maji kwa ajili ya mwanadamu. Miti pia husafisha hewa. Kupitia utaratibu mzuri wa usanidimwanga, chembe za majani hugeuza kaboni dioksidi, maji, madini, na nuru ya jua kuwa virutubisho na oksijeni.

Msitu huonyesha umaridadi na ubuni wa hali ya juu. Kwa kawaida miti mikubwa ndiyo huvutia zaidi katika msitu. Katikati ya miti hiyo kuna mimea mingine mingi midogo-midogo. Mimea hiyo hutegemea mazingira yanayotokezwa na miti hiyo, huku ikikua chini ya kivuli chake na kufyonza unyevu-nyevu unaotokana na msitu.

Katika misitu fulani yenye miti inayopukutisha majani, majani yapatayo milioni kumi yanaweza kuanguka katika eneo la msitu la ekari moja mwishoni mwa mwaka. Majani hayo huenda wapi? Wadudu, kuvu, minyoo, na viumbe wengine hai huyageuza kuwa mbolea inayorutubisha udongo. Naam, hakuna chochote kinachopotea wakati wafanyakazi hawa wasioonekana wanapotayarisha udongo kwa ajili ya mimea mipya.

Chini ya majani hayo makavu, udongo wa msitu una viumbe hai wengi sana. Kitabu The Forest, kinasema kwamba “huenda kukawa na viumbe 1,350 . . . katika eneo lenye ukubwa wa sentimeta 30 za mraba na lenye kina cha sentimeta 2.5, na hiyo haitii ndani mabilioni ya viumbe hai wasioonekana kwa macho ambao wamo katika kila konzi moja ya udongo.” Isitoshe, misitu ina wanyama watambaazi, ndege, wadudu, na wanyama wanyonyeshao. Ni nani anayepaswa kusifiwa kwa ajili ya viumbe hao maridadi na wa namna mbalimbali? Kwa kufaa, Muumba wao anasema: “Kila mnyama wa mwituni ni wangu, wanyama walio juu ya milima elfu moja.”—Zaburi 50:10.

Wanyama fulani waliumbwa wakiwa na uwezo wa ajabu wa kulala ili kupisha majira ya baridi kali na vipindi virefu vyenye uhaba wa chakula. Hata hivyo, si wanyama wote hufanya hivyo. Hata katikati ya majira ya baridi kali, huenda ukaona kundi la paa wakiruka-ruka kondeni. Paa hawalali ili kupisha majira ya baridi kali wala hawahifadhi chakula, bali wao hutafuta-tafuta chakula, wakiguguna-guguna majani laini na chipukizi kama unavyoona kwenye picha iliyo katika makala hii ambayo ilipigwa Ujerumani.

Mimea imezungumziwa sana katika Biblia. Kulingana na hesabu fulani, Biblia inataja mimea mbalimbali ipatayo 130, kutia ndani miti tofauti-tofauti 30 hivi. Mtaalamu wa mimea, Michael Zohary, anasema hivi kuhusu umuhimu wa kutajwa kwa miti na mimea hiyo katika Biblia: “Vitabu vya kawaida havitaji miti na mimea mingi inayohusiana na uhai kama vile Biblia.”

Miti na misitu ni zawadi bora kutoka kwa Muumba mwenye upendo.Kama umewahi kutembea msituni hakika utakubaliana na maneno haya ya mtunga-zaburi: “Miti ya Yehova imeshiba, mierezi ya Lebanoni ambayo alipanda. Ambamo ndege hutengeneza viota.”—Zaburi 104:16, 17.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 4 Ona Kalenda ya Mwaka wa 2004 ya Mashahidi wa Yehova, Januari/Februari.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 9]

Mlozi ni mojawapo ya miti yenye kuvutia zaidi huko Mashariki ya Kati. Mlozi huamka kutoka usingizini mwanzoni mwa mwaka, hata kabla ya miti mingine. Waebrania wa kale waliuita mlozi mti unaoamka, wakirejelea kule kuchanua maua kwake mapema. Mti huo huonekana kana kwamba unaamka kwa kuchanua maua yenye kupendeza ya rangi nyeupe au ya waridi.—Mhubiri 12:5.

Kati ya aina za ndege zipatazo 9,000 zinazojulikana, 5,000 hivi ni aina ya ndege waimbaji. Nyimbo zao husikika msituni. (Zaburi 104:12) Kwa mfano, shomoro mwimbaji hutoa sauti nzuri sana. Naye ndege huyu mdogo mwimbaji kwenye picha hii ana manyoya maridadi ya rangi ya kijivujivu, manjano, na kijani-kibichi.—Zaburi 148:1, 10.

[Picha katika ukurasa wa 9]

Msitu wa Normandy, Ufaransa