“Mojawapo ya Kazi Kuu Zaidi za Uhandisi”
“Mojawapo ya Kazi Kuu Zaidi za Uhandisi”
HEKALU la Yehova lilipojengwa Yerusalemu wakati wa utawala wa Mfalme Sulemani miaka 3,000 hivi iliyopita, beseni nzuri ya maji iliyotengenezwa kwa shaba iliwekwa nje ya kiingilio cha hekalu. Ilikuwa na uzito wa tani zaidi ya 30 na ingeweza kuwekwa lita 40,000 za maji. Beseni hiyo kubwa iliitwa bahari ya kuyeyushwa. (1 Wafalme 7:23-26) “Bila shaka, beseni hiyo ilikuwa mojawapo ya kazi kuu zaidi za uhandisi kuwahi kufanywa katika taifa la Waebrania,” asema Albert Zuidhof, aliyekuwa ofisa wa kiufundi kwenye Baraza la Kitaifa la Utafiti la Kanada, katika gazeti Biblical Archeologist.
Beseni hiyo ilitengenezwaje? Biblia inasema, “Katika Wilaya ya Yordani ndipo Mfalme alipoyeyusha [vyombo vya shaba] katika kalibu ya udongo wa mfinyanzi.” (1 Wafalme 7:45, 46) Zuidhof anasema, “Bila shaka, njia hiyo ya kuyeyusha inafanana na ile ambayo wayeyushaji hutumia nta kutengeneza kengele kubwa za shaba nyekundu.” Anaeleza kwamba katika njia hii, kwa kawaida wayeyushaji walitumia beseni mbili za udongo zilizokauka, moja ndogo ya ndani na nyingine kubwa ya nje, kisha wakamwaga shaba nyekundu iliyoyeyushwa katikati ya beseni hizo. Hatua ya mwisho ilikuwa kuvunja beseni hizo mbili za udongo.
Kwa kuwa beseni hiyo ya hekalu ilikuwa kubwa na nzito sana ilihitaji ustadi mkubwa kuitengeneza. Beseni ya udongo ya nje na ya ndani ilipaswa kuwa ngumu kuweza kustahimili tani 30 za shaba iliyoyeyushwa, na uyeyushaji huo ulipaswa kufanywa kwa kuendelea ili beseni ya shaba inayotengenezwa isiwe na nyufa au kasoro fulani. Yaelekea kazi hiyo ilihitaji tanuri kadhaa zilizounganishwa pamoja kwa ajili ya kumwaga shaba iliyoyeyushwa katikati ya zile beseni mbili za udongo. Hiyo ilikuwa kazi nyingi wee!
Katika sala yake wakati wa kuzinduliwa kwa hekalu, Mfalme Sulemani alimsifu Yehova Mungu kwa ajili ya kazi yote ya hekalu akisema: ‘Ulitoa hiyo ahadi kwa kinywa chako mwenyewe, na kwa mkono wako mwenyewe umetimiza, kama ilivyo leo hii.’—1 Wafalme 8:24.