Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Makanisa Yanaweza Kuokolewa?

Je, Makanisa Yanaweza Kuokolewa?

Je, Makanisa Yanaweza Kuokolewa?

“WATU huko Uingereza bado wanamwamini Mungu lakini hawataki kujitoa kwa Kristo,” asema Stephen Tirwomwe, kasisi Mganda. Miaka 20 hivi iliyopita kasisi huyo aliokoka kule kuuawa kikatili kwa washiriki fulani wa kanisa la Anglikana la Uganda. Leo yeye huhubiri kwenye vilabu vya wanaume huko Leeds, Uingereza, naye hutoa hotuba yake ya dakika kumi kabla wanaume hao hawajaanza kucheza kamari.

Huko Marekani, shirika la Mishonari la Kanisa la Anglikana lililoanzishwa hivi karibuni, linakabili tatizo hilohilo la kiroho. “Kati ya nchi zinazozungumza Kiingereza ulimwenguni, sasa Marekani ndiyo yenye watu wengi zaidi wasioenda kanisani na wasiopendezwa na mambo ya kiroho,” chasema kituo rasmi cha Internet cha shirika hilo. “Marekani imekuwa eneo ambalo mishonari wanahitaji kutumwa.” Kwa kukata tamaa baada ya kushindwa kuleta mabadiliko katika kanisa lao, shirika hilo jipya la mishonari lilikiuka desturi na kujiunga na viongozi wa Asia na Afrika ili kuanza “kupeleka mishonari wakahubiri huko Marekani.”

Hata hivyo, kwa nini mishonari kutoka Afrika, Asia, na Amerika Kusini ‘wanaokoa nafsi’ katika nchi za Ulaya na Amerika Kaskazini zinazodai kuwa za Kikristo?

Ni Nani Anayeokoa Mwingine?

Kwa miaka zaidi ya mia nne, mishonari wengi wenye bidii kutoka Ulaya waliendelea kumiminika katika maeneo mapya yaliyotawaliwa na wakoloni huko Afrika, Asia, Pasifiki, na Amerika Kusini. Lengo lao lilikuwa kupeleka dini yao kwa watu waliosemekana kuwa wapagani katika nchi hizo. Baada ya muda, nchi za Amerika zilizokuwa chini ya ukoloni, ambazo ilisemekana zilianzishwa kwa kutegemea kanuni za Kikristo, ziliungana na mwishowe zikatuma mishonari wengi zaidi ulimwenguni kushinda nchi za Ulaya. Sasa mambo yamebadilika.

“Kitovu [cha ule unaoitwa Ukristo] kimebadilika,” asema Andrew Walls, mwanzilishi na mkurugenzi wa Kituo cha Uchunguzi wa Ukristo katika nchi ambazo si za Magharibi. Katika mwaka wa 1900, asilimia 80 ya wale waliodai kuwa Wakristo walikuwa ama watu wa Ulaya au wa Amerika Kaskazini. Hata hivyo, leo zaidi ya asilimia 60 ya watu wanaodai kuwa Wakristo huishi Afrika, Asia, na Amerika Kusini. Ripoti moja ya hivi karibuni inasema: “Makanisa ya Katoliki huko Ulaya yanategemea makasisi kutoka Ufilipino na India,” na “mmoja kati ya makasisi sita wanaotumika katika parokia za Katoliki huko Marekani, anatoka nchi za ng’ambo.” Wahubiri Waafrika nchini Uholanzi, ambao wengi wao wanatoka Ghana, hujiona kuwa “mishonari katika bara lisilojishughulisha na dini.” Na sasa wahubiri kutoka Brazili hufanya mikutano ya injili katika maeneo mbalimbali nchini Uingereza. Mwandikaji mmoja anasema: “Nchi zilizotuma mishonari hapo kwanza sasa ndizo zinapokea mishonari.”

Mapambano Yatazamiwa

Yaelekea mishonari wanahitajika katika nchi za Ulaya na Amerika ya Kaskazini ambazo zinazidi kutojishughulisha na dini. “Huko Scotland Wakristo wanaoenda kanisani kwa ukawaida hawafiki asilimia 10,” lasema gazeti moja. Nchini Ufaransa na Ujerumani, Wakristo wanaoenda kanisani ni wachache hata zaidi. Walipohojiwa, “asilimia 40 hivi ya Wamarekani na asilimia 20 hivi ya Wakanada walisema kwamba wao huenda kanisani kwa ukawaida,” ripoti nyingine inasema. Tofauti na nchi hizo, inasemekana kwamba nchini Ufilipino, watu asilimia 70 hivi huenda kanisani, na hali iko hivyo katika nchi nyingine zinazositawi.

Jambo linalostahili kufikiriwa hata zaidi ni kwamba, watu wanaoenda makanisani katika nchi zilizo Kusini mwa Ikweta hushikilia zaidi mapokeo ya kanisa kuliko wenzao katika nchi zilizo Kaskazini mwa Ikweta. Kwa mfano, Wakatoliki huko Marekani na Ulaya wanapohojiwa, sikuzote wao husema kwamba hawaamini makasisi nao husisitiza kwamba watu wa kawaida wahusishwe zaidi katika shughuli za kanisa, na wanawake watendewe kwa usawa. Kwa upande mwingine, Wakatoliki katika nchi zilizo Kusini mwa Ikweta huunga mkono kabisa mapokeo ya kanisa kuhusu masuala hayo. Kwa kuwa nchi zilizo Kusini mwa Ikweta ndizo zina washiriki wengi katika dini, hilo litatokeza mapambano wakati ujao. Philip Jenkins, msomi wa historia na dini anatabiri hivi: “Inaonekana kwamba baada ya miaka kumi au ishirini hivi washiriki wa dini za Kikristo zilizo Kaskazini mwa Ikweta na zile zilizo Kusini mwa Ikweta, hawatawatambua wenzao kuwa Wakristo wa kweli.”

Kwa kufikiria hali hiyo, Walls anasema kwamba suala muhimu ni “jinsi Wakristo wa Afrika, Asia, Amerika Kusini, Amerika Kaskazini, na Ulaya wanavyoweza kuishi pamoja katika kanisa moja, na kudumisha imani ileile.” Unaonaje? Je, makanisa yanaweza kuokoka katika ulimwengu uliogawanyika? Msingi wa umoja wa Ukristo wa kweli ni nini? Makala inayofuata itatoa majibu ya Kimaandiko, pamoja na uthibitisho ulio wazi kwamba tayari kuna kikundi chenye kusitawi cha Wakristo walioungana ulimwenguni pote.

[Picha katika ukurasa wa 4]

Jengo hili lililokuwa kanisa sasa ni mkahawa ambapo muziki hupigwa

[Hisani]

AP Photo/Nancy Palmieri