Mwadhimisho Unaokuhusu
Mwadhimisho Unaokuhusu
YESU KRISTO alipokuwa duniani, alianzisha mwadhimisho unaomtukuza Mungu. Hii ndiyo sherehe pekee ya kidini ambayo aliwaagiza wafuasi wake moja kwa moja waiadhimishe, nayo ni Mlo wa Jioni wa Bwana.
Wazia kwamba wewe ni mtazamaji asiyeonekana wa matukio yaliyoongoza kwenye sherehe hiyo. Yesu na mitume wake wamekutanika pamoja katika chumba cha juu huko Yerusalemu ili waadhimishe Pasaka ya Wayahudi. Wamemaliza kula chakula kilicholiwa wakati wa Pasaka, yaani, mwana-kondoo aliyechomwa, mboga chungu, mkate usiotiwa chachu, na divai nyekundu. Mtume Yuda Iskariote, asiye mwaminifu, amefukuzwa na baada ya muda mfupi atamsaliti Bwana wake. (Mathayo 26:17-25; Yohana 13:21, 26-30) Yesu yuko peke yake pamoja na mitume wake waaminifu 11. Mathayo ni mmoja wao.
Kulingana na masimulizi ya Mathayo aliyejionea tukio hilo, hivi ndivyo Yesu anavyoanzisha Mlo wa Jioni wa Bwana: “Yesu alichukua mkate [usiotiwa chachu] na, baada ya kutoa baraka, akaumega, akawapa wanafunzi, akasema: ‘Chukueni, mle. Huu unamaanisha mwili wangu.’ Pia, akachukua kikombe na, akiisha kushukuru, akawapa, akisema: ‘Kinyweeni, ninyi nyote; kwa maana hii inamaanisha ‘damu yangu ya agano,’ ambayo itamwagwa kwa ajili ya wengi kwa msamaha wa dhambi.’”—Mathayo 26:26-28.
Kwa nini Yesu alianzisha Mlo wa Jioni wa Bwana? Alipoanzisha mlo huo, kwa nini alitumia mkate usiotiwa chachu na divai nyekundu? Je, wafuasi wote wa Kristo wangekula na kunywa mifano hiyo? Mlo huo ulipaswa kuadhimishwa mara ngapi? Je, kweli una maana kwako?