Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Makasisi Wanapaswa Kujiingiza Katika Siasa?

Je, Makasisi Wanapaswa Kujiingiza Katika Siasa?

Je, Makasisi Wanapaswa Kujiingiza Katika Siasa?

“ASKOFU mmoja mkuu Mkanada aliwaambia watu wanaotembelea sehemu zinazoonwa kuwa takatifu kwamba kujiingiza katika siasa kunaweza kuwasaidia maskini . . . Hata kama mfumo wa kisiasa hauonekani kuwa unapatana na mapenzi ya Mungu, ‘tunahitaji kujiingiza katika siasa ili tuweze kuwatendea maskini kwa haki.’”—Catholic News.

Ni kawaida kusikia ripoti kuhusu viongozi wa dini wakiunga mkono hatua ya kujiingiza katika siasa; na viongozi wengi wa dini wana vyeo vya kisiasa. Baadhi yao wamejaribu kubadili siasa ziwe bora. Nao wengine wanaheshimiwa na kukumbukwa kwa kampeni zao kuhusu masuala kama vile usawa wa kijamii na kukomeshwa kwa utumwa.

Hata hivyo, waumini wengi huhisi vibaya wahubiri wao wanapounga mkono upande fulani katika masuala ya kisiasa. Makala moja kuhusu theolojia ya kisiasa katika Christian Century ilisema: “Waumini Waprotestanti ndio nyakati nyingine waliotilia shaka kujiingiza kwa viongozi wao wa dini katika siasa.” Watu wengi wa dini huona kanisa kuwa takatifu na halipaswi kujiingiza katika siasa.

Jambo hilo hutokeza maswali mengi yenye kuvutia ambayo huwahangaisha wote wanaotaka kuishi katika ulimwengu bora. Je, wahubiri wa Ukristo wanaweza kuzibadili siasa ziwe bora? * Je, kuhubiri siasa ndiyo njia ya Mungu ya kuleta serikali na ulimwengu bora? Je, kusudi la awali la Ukristo lilikuwa kuanzisha njia mpya ya kushiriki katika siasa?

Jinsi Wahubiri Walivyoanza Kujiingiza Katika Siasa

Katika kitabu The Early Church, mwanahistoria Henry Chadwick anasema kwamba kutaniko la mapema la Kikristo lilijulikana kwa “kutojishughulisha kupata mamlaka katika ulimwengu huu.” Lilikuwa “lenye utulivu, lenye kupenda amani, na lisilojiingiza katika siasa.” Kitabu A History of Christianity kinasema: “Wakristo wengi walisadiki kwamba hakuna yeyote kati yao aliyepaswa kuwa na cheo serikalini . . . Baadaye, mwanzoni mwa karne ya tatu, Hippolytus alisema kwamba kulingana na desturi ya Kikristo ya zamani, hakimu alipaswa kujiuzulu kabla ya kujiunga na Kanisa.” Hata hivyo, pole kwa pole, watu waliotamani mamlaka walianza kuongoza makutaniko na kujipatia majina makubwa ya vyeo. (Matendo 20:29, 30) Baadhi yao walitaka kuwa viongozi wa dini na pia wa kisiasa. Badiliko la ghafula katika serikali ya Roma liliwawezesha viongozi hao wafanye walilotaka.

Katika mwaka wa 312 W.K., Maliki Mroma Konstantino alianza kupendelea Ukristo wa jina. Inashangaza kwamba maaskofu walikuwa tayari kukubaliana na maliki huyo mpagani ili awape mapendeleo fulani. Henry Chadwick aliandika: “Kanisa lilizidi kuhusika katika maamuzi muhimu ya kisiasa.” Viongozi wa dini waliathiriwaje na kujiingiza katika siasa?

Jinsi Siasa Zilivyowaathiri Wahubiri

Wazo la kwamba Mungu angewatumia viongozi wa dini kama wanasiasa liliungwa mkono hasa na Augustine, Mwanatheolojia Mkatoliki wa karne ya tano, aliyekuwa maarufu. Aliwazia kwamba kanisa lingetawala mataifa na kuwaletea wanadamu amani. Lakini mwanahistoria H. G. Wells aliandika: “Masimulizi kuhusu mambo yaliyotukia Ulaya kuanzia karne ya tano hadi ya kumi na tano yanafafanua hasa kushindwa kwa jaribio la kuwa na serikali ya kimungu.” Dini zinazojiita za Kikristo hazikuleta amani duniani, hata Ulaya kwenyewe. Hivyo, wengi wakapoteza imani katika jaribio hilo lililofikiriwa kuwa la Kikristo. Shida ilikuwa nini?

Wengi waliodai kuhubiri Ukristo walijiingiza katika siasa wakiwa na nia nzuri, lakini wakaanza kushiriki katika vitendo viovu. Martin Luther, aliyekuwa mhubiri na mtafsiri wa Biblia, ni maarufu sana kwa juhudi zake za kuleta mabadiliko katika Kanisa Katoliki. Hata hivyo, msimamo wake imara dhidi ya mafundisho ya kanisa ulifanya apendwe na wale waliotaka kuasi kwa sababu za kisiasa. Watu wengi waliacha kumheshimu pale yeye pia alipoanza kuzungumzia masuala ya kisiasa. Mwanzoni, aliwaunga mkono wakulima walioasi wakuu wenye kukandamiza. Kisha, uasi huo ulipoanza kuwa wenye jeuri, akawatia moyo wakuu hao kuukomesha, nao wakafanya hivyo kwa kuua watu wengi sana. Haishangazi kwamba wakulima walimwona kuwa msaliti. Luther pia aliwatia moyo wakuu hao katika uasi wao dhidi ya maliki Mkatoliki. Kwa kweli, Waprotestanti, kama wafuasi wa Luther wanavyoitwa, walianzisha harakati ya kisiasa tangu mwanzo. Luther aliathiriwaje na mamlaka? Yalimpotosha. Kwa mfano, ingawa mwanzoni alipinga kuwalazimisha watu waliompinga wakubaliane naye, baadaye aliwahimiza marafiki wake wa kisiasa wawaue kwa kuwachoma moto wale waliopinga ubatizo wa watoto.

John Calvin alikuwa kasisi maarufu huko Geneva, lakini yeye pia akawa na uwezo mkubwa kisiasa. Michael Servetus alipoonyesha kwamba Maandiko hayaungi mkono Utatu, Calvin alitumia uwezo wake wa kisiasa kuunga mkono kuuawa kwa Servetus ambaye alichomwa kwenye mti. Calvin alikuwa ameachilia mbali kabisa mafundisho ya Yesu.

Labda watu hao walisahau vile Biblia inavyosema katika 1 Yohana 5:19: “Ulimwengu mzima unakaa katika nguvu za yule mwovu.” Je, walitamani kwa unyoofu kubadili siasa za wakati wao ziwe bora, au walivutiwa na taraja la kupata uwezo na marafiki wenye vyeo vikubwa? Vyovyote vile, walipaswa kukumbuka maneno ambayo Yakobo, mwanafunzi wa Yesu, aliongozwa na roho ya Mungu kuandika: “Hamjui kwamba urafiki na ulimwengu ni uadui na Mungu? Kwa hiyo, yeyote anayetaka kuwa rafiki ya ulimwengu anajifanya kuwa adui ya Mungu.” (Yakobo 4:4) Yakobo alijua kwamba Yesu alikuwa amesema hivi kuhusu wafuasi wake: “Wao si sehemu ya ulimwengu, kama vile ambavyo mimi si sehemu ya ulimwengu.”—Yohana 17:14.

Hata hivyo, wengi hukataa kuchukua msimamo wa kutokuwamo, yaani, ‘kutokuwa sehemu ya ulimwengu’ ingawa wanajua kwamba Wakristo hapaswi kushiriki katika maovu ya ulimwengu. Wanadai kwamba msimamo huo huwazuia Wakristo wasiwaonyeshe wengine upendo. Wanaamini kwamba viongozi wa makanisa wanapaswa kuzungumza waziwazi na kushiriki katika kupambana na ufisadi na ukosefu wa haki. Lakini, je, kwa kweli msimamo wa kutokuwamo ambao Yesu alifundisha unaweza kumfanya mtu asionyeshe anawajali wengine? Je, Mkristo anaweza kujitenga na masuala ya kisiasa yenye kugawanya na wakati huohuo awasaidie wengine? Makala inayofuata inachanganua maswali hayo.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 5 Siasa zimefafanuliwa kuwa “shughuli zinazohusiana na utawala wa nchi au eneo, hasa majadiliano au mapambano kati ya watu au vyama vyenye mamlaka au vinavyotumaini kuyapata.”—The New Oxford Dictionary of English.

[Picha katika ukurasa wa 4]

Ili kupata uwezo wa kisiasa, viongozi wa makanisa walijitiisha kwa watawala kama Maliki Konstantino

[Hisani]

Musée du Louvre, Paris

[Picha katika ukurasa wa 5]

Kwa nini viongozi maarufu wa dini walijiingiza katika siasa?

Augustine

Luther

Calvin

[Hisani]

Augustine: ICCD Photo; Calvin: Portrait by Holbein, from the book The History of Protestantism (Vol. II)