Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Michezo ya Zamani na Umuhimu wa Kushinda

Michezo ya Zamani na Umuhimu wa Kushinda

Michezo ya Zamani na Umuhimu wa Kushinda

“KILA mtu anayeshiriki katika shindano hujizuia katika mambo yote.” “Kama yeyote akishindana . . . katika michezo, havikwi taji isipokuwa awe ameshindana kulingana na sheria.”—1 Wakorintho 9:25; 2 Timotheo 2:5.

Michezo ambayo mtume Paulo alirejelea ilikuwa sehemu muhimu katika utamaduni wa Ugiriki. Historia inatuambia nini kuhusu mashindano hayo na uvutano wake?

Hivi karibuni, maonyesho fulani kuhusu michezo ya Wagiriki, Nike—Il gioco e la vittoria (“Nike—Michezo na Ushindi”), yalifanywa katika Uwanja wa Duara wa Roma. * Maonyesho hayo yalitoa majibu fulani kwa swali hilo nayo hutusaidia tufikirie maoni ya Mkristo kuhusu michezo.

Michezo Ni Utamaduni wa Zamani

Ugiriki haikuwa nchi ya kwanza kushiriki katika michezo. Hata hivyo, yapata karne ya nane K.W.K., Homer, mshairi Mgiriki, alitaja jamii iliyosisimuliwa na mashujaa waliokuwa mifano bora na roho ya ushindani, na ambayo ilithamini sana uwezo wa kijeshi na riadha. Maonyesho hayo yalieleza kwamba sherehe za zamani kabisa za Wagiriki zilianza kama sherehe za kidini za kutukuza miungu kwenye mazishi ya mashujaa. Kwa mfano, Iliad, kitabu cha zamani zaidi cha fasihi ya Kigiriki, kilichoandikwa na Homer kinaeleza jinsi mashujaa wa tabaka la juu, waliokuwa pamoja na Achilles, walivyoweka silaha zao chini kwenye mazishi ya Patroclus na kushindana ili kuonyesha ushujaa wao katika kupigana ngumi, mieleka, kutupa kisahani na mkuki, na mashindano ya magari ya farasi.

Sherehe nyingine kama hizo zilianza kusherehekewa kotekote Ugiriki. Kijitabu kuhusu maonyesho hayo kinasema: “Sherehe hizo ziliandaa nafasi muhimu ambayo Wagiriki, kwa kuitukuza miungu yao, waliacha kwa muda mizozano yao isiyokoma na ambayo mara nyingi ilikuwa yenye jeuri. Walifanikiwa kubadili roho yao ya ushindani na badala yake wakaanzisha mashindano ya riadha yenye amani na yenye unyoofu.”

Vikundi vya majiji yenye kujitawala vilianza zoea la kukutana kwenye vituo vya pamoja vya ibada ili kuitukuza miungu yao kupitia mashindano ya riadha. Baadaye, sherehe nne kama hizo—Michezo ya Olimpiki na ya Nimea, iliyofanywa kwa heshima ya Zeu, na Michezo ya Pythia na Isthmus, iliyofanywa kwa heshima ya Apollo na Poseidon—ilizidi kupata umuhimu na kufikia kiwango cha kusherehekewa Ugiriki yote. Yaani, Wagiriki wote wangeweza kushiriki katika michezo hiyo. Sherehe hizo zilitia ndani dhabihu na sala, na pia zilitukuza miungu kupitia mashindano ya michezo au sanaa iliyo bora.

Mojawapo ya sherehe za zamani na maarufu zaidi inayosemekana kuwa ilianza mwaka wa 776 K.W.K., ilifanywa kila baada ya miaka minne huko Olympia ili kumtukuza Zeu. Sherehe ya pili kwa umuhimu ni ile ya Pythia. Sherehe hiyo iliyofanywa karibu na hekalu la uaguzi lililokuwa maarufu zaidi huko Delphi, ilitia ndani pia michezo ya riadha. Lakini nyimbo na dansi ndizo zilizokuwa muhimu katika sherehe ya kumtukuza Apollo, mfadhili wa mashairi na muziki.

Mashindano Mbalimbali ya Michezo

Tofauti na michezo ya sasa, idadi ya michezo ambayo watu wangeshiriki ilikuwa michache, na ni wanaume peke yao walioshiriki. Michezo ya zamani ya Olimpiki haikuzidi kumi. Sanamu, vinyago, nakshi, na michoro iliyokuwa kwenye vyombo vya udongo uliochomwa ambavyo vilikuwa kwenye Uwanja wa Duara vilionyesha kwa kiwango kidogo jinsi michezo hiyo ilivyokuwa.

Kulikuwa na mashindano ya kukimbia ya aina tatu—yenye urefu wa meta 200; yenye urefu maradufu unaolingana na mbio za sasa za meta 400; na mbio za masafa marefu za meta 4,500 hivi. Wanamichezo walikimbia na kufanya mazoezi wakiwa uchi wa mnyama. Washindani walioshiriki katika michezo mitano tofauti walishindana katika: kukimbia, kuruka chini, kupigana mweleka, kutupa kisahani na mkuki. Mashindano mengine yalitia ndani kupigana ngumi na pancratium, shindano linalofafanuliwa kuwa “mchezo wenye ukatili uliohusisha mieleka na kupigana ngumi bila kuvaa glavu.” Kisha kulikuwa na mashindano ya urefu wa meta zaidi ya 1,600 ya magari mepesi yenye magurudumu madogo yaliyokuwa wazi nyuma. Magari hayo yalikokotwa na farasi wadogo wawili au wanne, au na farasi wakubwa.

Mashindano ya ngumi yalikuwa yenye jeuri sana na wakati mwingine yalisababisha kifo. Kwenye ngumi zao, washindani walivaa mikanda ya ngozi ngumu iliyopigiliwa vipande vya chuma vyenye kuumiza. Unaweza kuwazia ni kwa nini mshindani aitwaye Stratofonte hangeweza kujitambua kwenye kioo baada ya kupigana ngumi kwa muda wa saa nne. Sanamu na nakshi za zamani zinaonyesha kwamba wapiganaji ngumi waliharibiwa sura vibaya sana.

Katika mieleka, washindani hawakuruhusiwa kushika sehemu ya juu ya mwili, na mshindi alipaswa kumwangusha mpinzani wake mara tatu. Lakini katika shindano la pancratium washindani waliruhusiwa kushikana. Wangeweza kupigana mateke, ngumi, na kutegua maungio. Walikatazwa tu kung’oana macho, kukwaruzana, na kuumana. Lengo la mshindani lilikuwa kumwangusha mpinzani wake na kumlazimisha asalimu amri. Wengine waliona shindano hilo kuwa “bora zaidi katika Olympia yote.”

Inasemekana kwamba shindano maarufu na la zamani zaidi la pancratium lilifanywa mwaka wa 564 K.W.K. kwenye fainali za Olimpiki. Arrhachion, aliyekuwa akinyongwa, alikuwa macho vya kutosha kutegua kidole cha mguu cha mpinzani wake. Kwa kulemewa na uchungu, mpinzani huyo alisalimu amri kabla tu ya Arrhachion kufa. Waamuzi walitangaza maiti ya Arrhachion kuwa imeshinda!

Mashindano ya magari ya farasi ndiyo yaliyokuwa maarufu na yenye kupendwa zaidi na watu wa tabaka la juu, kwa kuwa mwenye gari na farasi ndiye aliyeshinda wala si mwendeshaji. Mwanzo wa mashindano hayo ulikuwa mgumu kwa kuwa waendeshaji walipaswa kubaki kwenye mistari yao. Isitoshe, walipaswa kubaki kwenye mistari hiyo walipopiga kona kuzunguka nguzo mbili zilizokuwa kwenye sehemu ya mwisho ya uwanja. Kuvunja sheria za michezo kungeweza kusababisha aksidenti zilizofanya shindano hilo maarufu livutie hata zaidi.

Tuzo

Mtume Paulo alisema: “Wakimbiaji katika mbio wote hukimbia, lakini ni mmoja tu anayepokea tuzo.” (1 Wakorintho 9:24) Ushindi ndio uliokuwa jambo muhimu zaidi. Hakukuwa na nishani ya fedha au shaba wala hakukuwa na mshindi wa pili au wa tatu. Maonyesho hayo yanaeleza, “Ushindi, ‘Nike,’ ndio uliokuwa lengo kuu zaidi kwa mshindani.” Yeye “alitaka tu kushinda kwa sababu ushindi ndio ulioonyesha kikweli sifa zake za kimwili na kiadili, na kuuletea fahari mji wake wa nyumbani.” Mtazamo huo unaelezwa hivi katika mstari mmoja tu wa kitabu cha Homer: “Sikuzote nimejifunza kufanya vizuri kuliko wengine.”

Tuzo alilopewa mshindi katika Michezo iliyohusisha Wagiriki wote lilikuwa tu mfano—taji la majani. Paulo aliliita “taji linaloharibika.” (1 Wakorintho 9:25) Hata hivyo, tuzo hilo lilikuwa na maana kubwa. Liliwakilisha nguvu za asili zilizomsaidia mshindi kushinda. Ushindi uliopatikana kwa kujitoa kabisa, ulimaanisha kwamba mtu alikuwa na kibali cha miungu. Kwenye maonyesho hayo kulikuwa pia na maandishi kuhusu maoni ya watengeneza-vinyago na wachoraji wa zamani kuhusu Nike, mungu-mke wa ushindi wa Ugiriki mwenye mabawa, akimpa mshindi taji. Mchezaji alifikia upeo wa ustadi wake aliposhinda katika michezo ya Olympia.

Mataji ya Olimpiki yalitengenezwa kwa majani ya mzeituni-mwitu—taji kwenye michezo ya Isthmus lilitengenezwa kwa msindano, la Pythia likatengenezwa kwa mdalasini, nalo la Nemea likatengenezwa kwa figili-mwitu. Waliopanga michezo hiyo kwingineko walitoa pesa au tuzo nyingine ili kuvutia washindani walio bora zaidi. Vyombo kadhaa vya maua vilivyokuwa kwenye maonyesho hayo ni tuzo zilizotolewa kwenye Michezo iliyohusisha Waathene wote, ambayo ilifanywa Athene ili kumtukuza mungu wa kike Athena. Mwanzoni, vyombo hivyo vyenye mikono miwili vilikuwa na mafuta yenye thamani ya mzeituni kutoka Attica. Mchoro ulio upande mmoja wa mojawapo ya vyombo hivyo unaonyesha Athena na una maneno “tuzo kwa mashindano ya Athena.” Upande ule mwingine una picha ya shindano fulani, yaelekea lile ambalo mshindani alipata ushindi.

Majiji ya Ugiriki yalifurahia umaarufu yaliyopata kwa sababu ya wanamichezo wao, ambao ushindi wao uliwafanya kuwa mashujaa sehemu walikotoka. Washindi waliporudi nyumbani walikaribishwa kwa maandamano yenye shangwe ya ushindi. Sanamu zao zilichongwa ili kutoa shukrani kwa miungu—heshima ambayo kwa kawaida haikupewa wanadamu—nao washairi waliimba kuhusu ushujaa wa washindi hao. Baadaye, washindi walikuwa wakiketi viti vya mbele kwenye sherehe za umma na walipokea malipo ya uzeeni kutoka hazina ya umma.

Kumbi za Mazoezi ya Viungo na Walioshiriki

Mashindano ya riadha yalionwa kuwa muhimu katika ukuzi wa raia waliokuwa askari. Majiji yote ya Ugiriki yalikuwa na kumbi ambako vijana walifanya mazoezi ya viungo na pia kufundishwa mambo ya usomi na ya kiroho. Kumbi hizo zilijengwa kuzunguka sehemu kubwa zilizo wazi zilizotumiwa kwa mazoezi, na ambazo zilizungukwa na varanda yenye nguzo na sehemu nyingine zenye paa ambazo zilitumiwa kama maktaba na madarasa. Majengo hayo yalitembelewa hasa na vijana kutoka familia tajiri ambao wangeweza kutumia wakati kujifunza badala ya kufanya kazi. Huko, wanamichezo walifanya mazoezi makali na ya muda mrefu ili kujitayarishia michezo. Walisaidiwa na wakufunzi ambao waliwaeleza chakula walichopaswa kula na kuhakikisha kwamba walijiepusha na ngono.

Maonyesho kwenye Uwanja wa Duara yaliwapa wageni nafasi ya kufurahia miigizo bora ya vinyago vya awali vya wanamichezo wa zamani ambavyo Waroma waliiga hasa kutoka kwa Wagiriki. Kulingana na itikadi ya kale ya Wagiriki, ubora wa kimwili ulikuwa sawa na ubora wa kiadili nao ungeweza kupatikana tu na watu wa tabaka la juu, hivyo miili iliyoumbika vizuri ya wanamichezo hao wenye kushinda iliwakilisha falsafa bora. Waroma walithamini vinyago hivyo kuwa kazi ya usanii, navyo vilipamba viwanja vya michezo, bafu, nyumba za kifahari, na majumba ya wafalme.

Waroma walipenda sana michezo yenye jeuri, kwa hiyo kati ya michezo yote ya Wagiriki iliyofanyiwa Roma, walivutiwa zaidi na mapigano ya ngumi, mieleka, na pancratium. Waroma waliiona michezo hiyo kuwa vitumbuizo tu wala si mashindano ya kutambua mshindani bora kati ya washindani wawili wenye uwezo sawa. Yale maoni ya awali kwamba michezo ilihusisha kuelimishwa kwa pamoja kwa wanamichezo mashujaa yaliachwa. Badala yake, Waroma walipunguza heshima ya michezo ya Wagiriki kuwa tu mazoezi ya kuboresha afya au michezo ya watazamaji iliyofanywa na wachezaji wa hali ya chini, kama vile michezo ya kupigana ya Waroma.

Wakristo na Michezo Hiyo

Wakristo wa karne ya kwanza waliepuka michezo hiyo kwa sababu ilihusisha mambo ya kidini, kwa kuwa “hekalu la Mungu lina upatano gani na sanamu?” (2 Wakorintho 6:14, 16) Namna gani michezo leo?

Bila shaka, michezo ya siku hizi haitukuzi miungu ya kipagani. Lakini, je, si kweli kwamba bidii ya watu fulani katika michezo inakuwa karibu sawa na bidii yao katika mambo ya kidini, ambayo inaweza kulinganishwa na ile ya wanamichezo wa zamani? Isitoshe, kama vile ambavyo ripoti za miaka michache iliyopita zimeonyesha, ili kushinda, wanamichezo fulani wamekubali kutumia dawa za kuongeza nguvu mwilini ambazo huhatarisha afya yao na hata maisha yao.

Wakristo hawathamini sana mafanikio ya kimwili. Sifa za kiroho za “yule mtu wa siri wa moyoni” ndizo hutufanya tupendeze machoni pa Mungu. (1 Petro 3:3, 4) Tunatambua kwamba leo si wanamichezo wote ambao wana roho ya ushindani mkali, lakini wengi wanayo. Je, kushirikiana nao kutatusaidia kufuata himizo la Biblia la ‘kutofanya jambo lolote kwa ugomvi au kwa kujisifu, bali kwa unyenyekevu wa akili?’ Au kushirikiana nao hakutatokeza ‘uadui, mizozo, wivu, milipuko ya hasira, magomvi, na migawanyiko’?—Wafilipi 2:3; Wagalatia 5:19-21.

Michezo mingi ya siku hizi ambayo washindani hugusana inaweza kutokeza jeuri. Yeyote anayevutiwa na michezo hiyo anapaswa kukumbuka maneno ya Zaburi 11:5: “Yehova humchunguza mwadilifu na pia mwovu, na mtu yeyote anayependa jeuri nafsi Yake hakika inamchukia.”

Mazoezi yanaweza kufurahisha yasipofanywa kupita kiasi, naye mtume Paulo alisema kwamba “mazoezi ya kimwili ni yenye faida kidogo.” (1 Timotheo 4:7-10) Hata hivyo, alipozungumza kuhusu michezo ya Wagiriki, kwa kufaa Paulo aliirejelea ili kuonyesha umuhimu wa Wakristo kuwa na sifa kama vile kujizuia na uvumilivu. Lengo kuu la Paulo lilikuwa kujitahidi kupokea “taji” la uzima wa milele kutoka kwa Mungu. (1 Wakorintho 9:24-27; 1 Timotheo 6:12) Kwa kufanya hivyo, alituwekea kielelezo.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 4 Nike ni neno la Kigiriki linalomaanisha “ushindi.”

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 31]

Mpiganaji-Ngumi Baada ya Pigano Lingine

Medali hii ya shaba ya karne ya nne K.W.K. inaonyesha madhara yaliyosababishwa na mapigano ya zamani ya ngumi, na kulingana na kitabu kuhusu maonyesho ya Roma, “upinzani wa mpiganaji-ngumi . . . aliyeshiriki katika mapigano yenye kuchosha ambapo mpiganaji alirudisha ‘jeraha kwa jeraha,’ ulionwa kuwa kielelezo kizuri.” Kitabu hicho kinaendelea kusema, “Mtu alipata majeraha zaidi mbali na majeraha aliyopata katika pigano lililopita.”

[Picha katika ukurasa wa 29]

Mashindano ya magari ya farasi ndiyo yaliyokuwa maarufu zaidi zamani

[Picha katika ukurasa wa 30]

Wachoraji wa zamani walimchora Nike, mungu-mke wa ushindi wa Ugiriki mwenye mabawa, akimpa mshindi taji