Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

“Mito na Ipige Makofi”

“Mito na Ipige Makofi”

Fahari ya Uumbaji wa Yehova

“Mito na Ipige Makofi”

ANGALIA ramani ya dunia, na katika sehemu nyingi utaona mistari yenye kujipindapinda inayopita kutoka upande mmoja wa ramani hadi ule mwingine. Mistari hiyo inapita nchi tambarare, majangwa, na kanda za mbuga. Inajipindapinda kupitia mabonde, korongo za mito, na misitu. (Habakuki 3:9) Mistari hiyo kwenye ramani ni mito ya sayari yetu ambayo ni kama mishipa ya uhai. Mito hiyo inashuhudia hekima na nguvu za Yehova, Muumba wa dunia. Tunapoichunguza, tunakubaliana na maoni ya mtunga-zaburi aliyeimba: “Mito na ipige makofi; milima yote pamoja na ipige vigelegele kwa shangwe mbele za Yehova.”—Zaburi 98:8, 9. *

Kuna uhusiano wa karibu sana kati ya mito na historia ya mwanadamu. Biblia huzungumza kuhusu mito minne muhimu iliyogawanyika kutoka katika mto mmoja uliotoka Edeni. (Mwanzo 2:10-14) Moja kati ya staarabu za kale ulianzia katika mabonde yenye rutuba ya mito Tigri na Efrati huko Mashariki ya Kati. Mito Hwang huko China, Ganges na Indus kusini mwa Asia, na Nile huko Misri, ilichangia kuwepo kwa staarabu kubwa.

Basi haishangazi kwamba sikuzote mwanadamu hustaajabia sana nguvu, wingi, na umaridadi wa mito. Mto Nile wa Misri unatiririka kwa umbali wa kilometa 6,670. Mto Amazon huko Amerika ya Kusini ndio mpana zaidi. Ingawa baadhi ya mito ni mikubwa, mingine ni maridadi sana, kama vile Mto Tone huko Japani, ambao ni mdogo zaidi, lakini unatiririka kwa haraka.

Ni nini hufanya mto utiririke? Kwa ufupi, ni nguvu za uvutano. Nguvu hizo ndizo huvuta maji kutoka juu hadi chini. Wakati mwingine kunakuwa na maporomoko ya maji yenye kelele. Ikizungumzia wonyesho huu wa nguvu na ukuu, Biblia inasema: “Mito imepaaza, Ee Yehova, mito imepaaza sauti yake; mito inaendelea kupaaza mivumo yake.”—Zaburi 93:3.

Yehova alimuuliza Ayubu, mwanamume mwenye kumwogopa Mungu hivi: “Nani aliyechora angani njia kwa ajili ya mvua?” (Ayubu 38:25, Biblia Habari Njema) Naam, maji yote hayo hutoka wapi? Jibu linahusiana na ule mfumo tata unaoitwa mzunguko wa maji. Maji duniani huzunguka daima huku yakivutwa na nishati ya jua na nguvu za uvutano. Maji hupanda angani baada ya kugeuka kuwa mvuke. Mwishowe, yanakuwa baridi na mazito ili kufanyiza mawingu. Hatimaye, mvuke huo hurudi duniani ukiwa theluji au mvua. Kiasi kikubwa cha maji hayo huhifadhiwa katika bahari, maziwa, mito, mito ya barafu, zile ncha za dunia zenye barafu, na chini ya ardhi.

Kuhusu mzunguko huu wa ajabu wa maji, Biblia inasema hivi: “Mito yote ya wakati wa majira ya baridi kali inaenda baharini, hata hivyo bahari haijai. Mahali inapoenda mito hiyo ya majira ya baridi kali, hapo ndipo inarudi ili iende tena.” (Mhubiri 1:7) Ni Yehova tu, Mungu mwenye upendo na hekima isiyo na kikomo, ambaye angeweza kuanzisha mzunguko kama huo. Nao mzunguko huo uliotayarishwa kwa njia ya akili hutuonyesha nini kuhusu utu wa Mungu? Kwamba Yeye ni mwenye hekima nyingi na upendo.—Zaburi 104:13-15, 24, 25; Methali 3:19, 20.

Licha ya ukubwa na idadi yake, mito ina kiasi kidogo sana cha maji ya dunia yasiyo na chumvi. Hata hivyo, maji hayo ni muhimu kwa uhai. ‘Mwanadamu hawezi kuishi bila maji na bila kuyadhibiti kwa kadiri fulani,’ chasema kitabu Water. “Hatua ambayo mwanadamu amechukua ili kupata maji na kuyadhibiti imechangia sana ustaarabu.”

Kwa miaka mingi, mito imetoa maji ya kunywa kwa ajili ya mwanadamu na kwa matumizi ya mabustani yake. Udongo wenye rutuba kando ya mito mingi ni muhimu kwa ukuzi wa mazao. Ona jinsi wazo hilo linavyoonyeshwa katika maneno haya ya kuwabariki watumishi wa Yehova: “Ni yenye kupendeza kama nini mahema yako, Ee Yakobo, maskani zako, Ee Israeli! Yameenea mbali kama mabonde ya mto, kama bustani kando ya mto. Kama mimea ya udi ambayo Yehova amepanda, kama mierezi kando ya maji.” (Hesabu 24:5, 6) Pia mito husaidia kutegemeza viumbe kama mabata na mbweha unayemwona hapa. Kwa kweli, kadiri tunavyoendelea kujifunza kuhusu mito, ndivyo tunavyochochewa zaidi kumtukuza Yehova.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 3 Ona Kalenda ya 2004 ya Mashahidi wa Yehova, Mei/Juni.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]

Maporomoko ya Iguaçú, kwenye mpaka kati ya Argentina na Brazili, ni kati ya maporomoko makubwa zaidi ya maji. Yana upana unaozidi kilometa 3. Maporomoko hayo ambayo yako kwenye msitu wa kitropiki wenye kuvutia yamefanyizwa kwa maporomoko madogo-madogo yapatayo 300. Wakati wa mvua, karibu meta 10,000 za mchemraba za maji huporomoka chini kila sekunde.

[Picha katika ukurasa wa 9]

Mto Tone, Japani