Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Wanabaptisti Walikuwa Akina Nani?

Wanabaptisti Walikuwa Akina Nani?

Wanabaptisti Walikuwa Akina Nani?

WATU wanaotembelea mara ya kwanza sehemu ya katikati ya jiji la Münster huko Westphalia, Ujerumani, karibu sikuzote husimama ili kutazama yale masanduku matatu ya chuma ambayo yananing’inia kwenye mnara wa kanisa. Isipokuwa kwa vipindi fulani tu, masanduku hayo yamekuwa mahali hapo kwa miaka 500 hivi. Mwanzoni, yalikuwa na miili ya wanaume watatu ambao waliteswa na kuuawa hadharani. Wanaume hao walikuwa Wanabaptisti, nayo masanduku hayo ni mabaki ya ufalme wao.

Wanabaptisti walikuwa akina nani? Kikundi chao kilianzaje? Kilikuwa na mafundisho gani ya msingi? Kwa nini waliuawa? Nayo masanduku hayo matatu yana uhusiano gani na ufalme?

Kanisa Linapaswa Kurekebishwaje?

Mwishoni mwa karne ya 15 na mwanzoni mwa karne ya 16, lawama dhidi ya Kanisa Katoliki la Roma na makasisi iliongezeka. Upotovu wa maadili na uasherati viliathiri sana kanisa; hivyo, wengi wakahisi kwamba mabadiliko makubwa yalihitajiwa. Mwaka wa 1517, Martin Luther aliomba hadharani mabadiliko yafanyike, na kwa kuwa wengine walijiunga na majadiliano hayo, Marekebisho Makubwa ya Dini ya Kiprostestanti yalikuwa karibu kutokea.

Lakini waleta-marekebisho hao hawakuwa na maoni sawa kuhusu marekebisho yaliyopaswa kufanywa na kwa kadiri gani. Wengi walitambua uhitaji wa kushikamana na Biblia katika mambo yanayohusu ibada. Hata hivyo, waleta-marekebisho hao hawakukubaliana hata katika ufafanuzi wa pamoja wa mafundisho ya Biblia. Wengine walihisi kwamba Marekebisho hayo Makubwa ya Kidini yalifanyika polepole sana. Kikundi cha Wanabaptisti kilianzishwa na baadhi ya waleta-marekebisho hao.

“Kwa kweli, hapakuwa na kikundi kimoja tu cha Wanabaptisti; bali vilikuwa vingi,” anaandika Hans-Jürgen Goertz katika kitabu chake Die Täufer—Geschichte und Deutung. Kwa mfano, mnamo mwaka wa 1521 wanaume wanne walioitwa manabii wa Zwickau walisababisha vurugu kwa kuhubiri mafundisho ya Wanabaptisti huko Wittenberg. Na katika mwaka wa 1525, kikundi tofauti cha Wanabaptisti kiliundwa huko Zurich, Uswisi. Jamii za Wanabaptisti zilianzishwa huko Uholanzi na pia Moravia—ambayo kwa sasa inajulikana kuwa Jamhuri ya Cheki.

Je, Ubatizo Ni kwa Watoto au kwa Watu Wazima?

Kwa kawaida jamii za Wanabaptisti zilikuwa ndogo, na kwa ujumla washiriki walijiendesha kwa amani. Waumini hawakuficha imani yao, waliwahubiria wengine. Mafundisho ya msingi ya Wanabaptisti yalielezwa katika Tangazo lao la Imani la Schleitheim mwaka wa 1527. Mafundisho yao ya msingi yalitia ndani kukataa utumishi wa kijeshi, kujitenga na ulimwengu, na kuwafukuza wakosaji. Lakini kilichofanya imani yao iwe hasa tofauti na dini nyingine ni kwamba Wanabaptisti waliamini kwa uhakika kwamba watu wazima ndio walistahili kubatizwa wala si watoto. *

Ubatizo wa watoto haukuwa tu suala la fundisho la kidini; bali la mamlaka. Ikiwa ubatizo ungeahirishwa hadi mtu afikie umri mkubwa ili kumruhusu afanye uamuzi unaotegemea imani, huenda wengine hawangebatizwa kamwe. Na kwa kadiri fulani, watu wasiobatizwa hawangekuwa chini ya uongozi wa kanisa. Kwa makanisa kadhaa, ubatizo wa mtu mzima ulimaanisha kupoteza uwezo.

Hivyo, Wakatoliki na pia wafuasi wa Luther walitaka kuzuia zoea la kubatiza watu wazima. Baada ya mwaka wa 1529, angalau katika maeneo fulani, wale waliobatiza watu wazima au wale waliobatizwa wakiwa watu wazima yaelekea walipaswa kuhukumiwa kifo. Mwandishi wa habari Thomas Seifert anaeleza kwamba Wanabaptisti “waliteswa vikali katika Milki Takatifu yote ya Roma ya taifa la Ujerumani.” Mateso yalikuwa makali zaidi huko Münster.

Jiji la Münster la Enzi za Kati Latafuta Mabadiliko

Katika enzi za kati jiji la Münster lilikuwa na wakaaji wapatao 10,000 nalo lilizingirwa kwa mfumo wa ulinzi usioweza kupenywa wenye upana wa meta 90 hivi na mzunguko wa kilometa 5. Hata hivyo, hali ndani ya jiji haikuwa tulivu kama ulinzi wake ulivyoonyesha. Kichapo The Kingdom of the Anabaptists, (Ufalme wa Wanabaptisti) kilichochapishwa na Jumba la Makumbusho la Jiji la Münster, kinataja “mabishano ya ndani ya kisiasa kati ya washiriki wa Baraza la Usimamizi la Jiji na Ushirika wa Wafanyabiashara na Mafundi.” Isitoshe, wakaaji walikasirishwa na mwenendo wa makasisi. Jiji la Münster lilikubali Marekebisho Makubwa ya Kidini na mnamo 1533 likaacha kuwa jiji la Kikatoliki na kuwa la Kilutheri.

Bernhard Rothmann, mtu mgumu zaidi, ndiye aliyekuwa mhubiri mleta-marekebisho mkuu huko Münster. Friedrich Oehninger anaeleza kwamba Rothmann “alianza kufuata kwa dhati maoni ya Wanabaptisti; yeye na wenzake wengine walikataa kuwabatiza watoto wachanga.” Aliungwa mkono na watu wengi huko Münster, ingawa wengine walimwona kuwa mwenye msimamo mkali. “Watu zaidi na zaidi waliopenda maoni ya zamani waliondoka katika jiji hilo lililojawa na wasiwasi na hisia za kwamba jambo baya lingetukia. Wanabaptisti walimiminika jijini Münster kutoka kila mahali, wakitarajia kwamba matazamio yao yangetimizwa.” Idadi hiyo kubwa ya Wanabaptisti huko Münster iliongoza kwenye tukio baya sana.

Yerusalemu Jipya Lazingirwa

Wahamiaji wawili wa Kiholanzi huko Münster, yaani, Jan Mathys, mwokaji mikate kutoka Haarlem, na Jan Beuckelson, anayejulikana kama John wa Leiden—walitimiza daraka muhimu katika maendeleo ya jiji hilo. Mathys alidai kuwa nabii na alitangaza Aprili 1534 kuwa wakati wa kurudi kwa Kristo kwa mara ya pili. Jiji la Münster lilitangazwa kuwa Yerusalemu Jipya linalotajwa katika Biblia nao watu wakaanza kufikiri kwamba mwisho ulikuwa umekaribia. Rothmann akaamua kwamba mali yote imilikiwe na watu wote. Wakaaji ambao walikuwa watu wazima walipaswa kuamua: Kubatizwa au kuondoka. Ubatizo wa watu wengi ulitia ndani baadhi ya wale waliobatizwa ili tu kuepuka kuacha nyumba na mali zao.

Jamii nyingine zilitazama kwa mshangao jinsi Münster lilivyokuja kuwa jiji la kwanza ambamo Wanabaptisti walikuwa wenye nguvu zaidi kidini na kisiasa. Kulingana na kitabu Die Täufer zu Münster, hali hiyo ilililetea jiji la “Münster uadui na Milki Takatifu ya Roma yote ya taifa la Ujerumani.” Askofu Count Franz von Waldeck, mkuu wa mahali hapo, alikusanya jeshi ili kuzingira Münster. Jeshi hilo liliundwa na Wakatoliki na wafuasi wa Luther. Dini hizo mbili, ambazo mapema zilipingana kuhusu Marekebisho Makubwa ya Kidini na ambazo karibuni zingepambana katika Vita vya Miaka 30, ziliungana kupigana na Wanabaptisti.

Kuharibiwa kwa Ufalme wa Wanabaptisti

Kuzingirwa kwa jiji na majeshi hayo hakukuwaogopesha wale waliojihisi salama ndani ya kuta za jiji hilo. Mnamo Aprili 1534, wakati ilipodhaniwa kwamba Kristo atarudi mara ya pili, Mathys alitoka nje ya jiji akiwa amepanda farasi mweupe, huku akitarajia kupata ulinzi wa kimungu. Fikiria woga wa wafuasi wa Mathys wakati walipotazama toka juu ya kuta na kuona jinsi majeshi yaliyolizingira jiji, yalivyomkata Mathys vipande-vipande, na kutundika kichwa chake.

John wa Leiden ndiye aliyechukua nafasi ya Mathys naye akaitwa Mfalme Jan wa Wanabaptisti huko Münster. Alijaribu kusawazisha idadi ya wanaume na wanawake kwa kuwa jiji lilikuwa na wanawake wengi zaidi kuliko wanaume. Hivyo, akawatia wanaume moyo kuchukua wanawake wengi zaidi kadiri walivyotaka. Kwa mfano, katika ufalme wa Wanabaptisti huko Münster, wazinzi na waasherati walihukumiwa adhabu ya kifo, bali kuoa wake wengi kuliruhusiwa, na hata wanaume walitiwa moyo kufanya hivyo. Mfalme Jan mwenyewe alioa wake 16. Wakati mmoja wa wake zake, Elisabeth Wandscherer, alipoomba ruhusu ya kuondoka katika jiji, aliuawa kwa kukatwa kichwa hadharani.

Kuzingirwa kwa jiji kulidumu miezi 14, hadi Juni 1535 wakati mwishowe jiji lilipotekwa. Jiji la Münster lilipata uharibifu ambao halikuwahi kuuona tena hadi Vita vya Pili vya Ulimwengu. Rothmann aliponyoka, lakini Mfalme Jan na viongozi wengine wawili wa Wanabaptisti walinaswa, wakateswa, na kuuawa. Miili yao iliwekwa ndani ya masanduku nayo yakainuliwa kwa kuning’inizwa kwenye mnara wa Kanisa la Mtakatifu Lambert. Hilo “lilifanyika ili kutoa onyo lenye kutisha kwa wakorofi wowote ambao wangejitokeza,” anasema Seifert. Naam, kujiingiza katika siasa kulileta matokeo mabaya.

Ni nini kilichotokea kwa jamii nyingine za Wanabaptisti? Mateso yaliendelea kwa miaka mingi katika Ulaya yote. Wanabaptisti wengi walishikamana na kanuni zao za kutojiunga na vita, ingawa baadhi yao walikuwa wapiganaji. Baada ya muda, kasisi wa zamani Menno Simons akawa kiongozi wa Wanabaptisti, nacho kikundi hicho kikaja kujulikana kuwa wafuasi wa Menno au kwa majina mengine.

Yale Masanduku Matatu

Kwa kweli, Wanabaptisti walikuwa watu wa kidini ambao walijaribu kushikamana na kanuni za Biblia. Lakini watu wenye msimamo mkali kuhusu masuala ya kisiasa, kiuchumi, au kijamii huko Münster walifanya Wanabaptisti waache kushikamana na kanuni za Biblia, na kujiingiza katika siasa. Hilo lilipotukia, kikundi hicho kilijiingiza katika harakati za mapinduzi ya kutumia nguvu. Hilo lilimaanisha hasara kwa kikundi cha Wanabaptisti na kwa jiji la Münster la enzi ya kati.

Watu wanapotembelea sehemu ya katikati ya jiji hilo bado hukumbuka matukio yenye kutisha yaliyotukia yapata miaka 500 iliyopita. Jinsi gani? Kwa kuona yale masanduku matatu ya chuma yanayoning’inia kwenye mnara wa kanisa.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 9 Makala hii haishughulikii hoja mbalimbali ili kuunga mkono au kupinga ubatizo wa watoto. Ili kupata maelezo zaidi kuhusu habari hiyo, ona makala “Je, Watoto Wachanga Wabatizwe?” katika gazeti Mnara wa Mlinzi, la Machi 15, 1986.

[Picha katika ukurasa wa 13]

Mfalme Jan aliteswa, akauawa, na kuning’inizwa kwenye mnara wa Kanisa la Mtakatifu Lambert