Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

‘Majira ya Kiangazi na Majira ya Baridi Kali Hayatakoma Kamwe’

‘Majira ya Kiangazi na Majira ya Baridi Kali Hayatakoma Kamwe’

Fahari ya Uumbaji wa Yehova

‘Majira ya Kiangazi na Majira ya Baridi Kali Hayatakoma Kamwe’

JUA kali sana linaangaza jangwani. Katika sehemu nyingine za dunia, linaleta joto baada ya majira ya baridi kali. Kwa kweli, joto la jua ni baadhi ya mambo ya msingi ambayo huchangia kubadilika kwa halihewa na majira.

Kunakuwa na majira tofauti-tofauti duniani pote. Lakini majira hukuathirije? Je, wewe hufurahia upepo mtulivu wa jioni wenye kuburudisha unapotembea kandokando ya ufuo wakati wa majira ya joto? Wewe huhisije mvua inapoanza kunyesha na kufanya udongo mkavu uwe na unyevunyevu? Je, wewe hufurahia kuona maeneo yaliyofunikwa na ukungu wakati wa majira ya baridi?

Ni nini hutokeza majira? Kwa ufupi, ni mwinamo wa dunia. Dunia huzunguka jua ikiwa imeinama kwa nyuzi 23.5 kwenye mhimili wake. Ikiwa dunia haingekuwa imeinama kwenye mhimili wake, hakungekuwa na majira. Kungekuwa na majira yaleyale daima. Hiyo ingeathiri mimea na ukuzaji wa mazao.

Mtu anaweza kuona uthibitisho wa kwamba Muumba alibuni majira yawe yakifuatana. Akizungumza na Yehova Mungu, mtunga-zaburi alisema hivi kwa kufaa: “Ni wewe uliyeweka mipaka yote ya dunia; majira ya kiangazi na majira ya baridi kali—wewe mwenyewe uliyafanyiza.”Zaburi 74:17. *

Vitu vinavyoonekana angani huashiria majira kwa usahihi. Alipokuwa akiumba mfumo wetu wa jua, Mungu aliagiza hivi: “Kuwe na mianga katika anga la mbingu . . . , nayo iwe ishara na kwa ajili ya majira na kwa ajili ya siku na miaka.” (Mwanzo 1:14) Kila mwaka, dunia hupitia sehemu mbili katika mzunguko wake ambapo jua huangaza juu ya mstari wa ikweta saa sita mchana. Matukio hayo yanaitwa ikwinoksi, na katika nchi nyingi huonyesha kwamba kipindi cha masika na vuli kimeanza. Wakati wa ikwinoksi, saa za mchana na usiku huwa karibu kulingana duniani pote.

Kuwepo na pia kuanza kwa majira hakuhusishi tu mwendo wa magimba ya mbinguni. Misimu, tabia ya nchi, na halihewa vinahusiana sana katika mfumo tata ambao hutegemeza uhai. Akizungumza na watu walioishi Asia Ndogo, ambao wengi wao walifahamu ukulima na uzalishaji wa chakula, mtume Mkristo Paulo na mwenzake Barnaba walisema kwamba Mungu ndiye ‘anayewapa ninyi mvua kutoka mbinguni na majira yenye kuzaa matunda, akijaza mioyo yenu kikamili kwa chakula na uchangamfu.’—Matendo 14:14-17.

Mfumo wa kustaajabisha wa usanidimwanga huendeleza mimea iliyo kwenye ardhi na ile ya baharini. Kwa kuwa mimea hutumia nuru kutengeneza chakula ambacho mimea na wanyama wengine hutegemea, mabadiliko ya halihewa husababisha mabadiliko tata ya vitu vilivyo hai na mazingira yake. Paulo alitaja kwamba mkono wa Yehova unahusika katika mambo hayo yote aliposema: “Udongo unaokunywa mvua ambayo huja mara nyingi juu yake, na kisha unazaa mimea inayofaa kwa wale ambao huo hulimwa kwa ajili yao, hupokea malipo ya baraka kutoka kwa Mungu.”—Waebrania 6:7.

Neno “baraka” huwa na maana nyingine unapofikiria mambo yanayotukia katika sehemu ambazo masika hutokeza halijoto la kadiri, siku ndefu zaidi, mwanga zaidi wa jua, na mvua za kutosha. Maua huchanua nao wadudu hutoka mahali walipokuwa wakati wa majira ya baridi kali, wakiwa tayari kuchavusha mimea. Ndege, kama vile blue jay unayemwona hapa, hufanya misitu ivutie kwa sababu ya rangi yake na nyimbo zake, nayo nchi huchangamka. Viumbe mbalimbali hukua haraka zaidi, navyo vijiumbe huendelea na maisha yao ya kawaida, kuzaliwa, kuzaliwa-upya, na kukua. (Wimbo wa Sulemani 2:12, 13) Utendaji huo hutangulia mavuno mwishoni mwa majira ya kiangazi au ya vuli.—Kutoka 23:16.

Kazi za Yehova zinadhihirishwa kwa njia ya ajabu na jinsi alivyoiinamisha dunia, akitupa usiku na mchana, majira, na wakati wa kupanda na kuvuna. Sisi huwa na hakika kwamba baada ya majira ya kiangazi kutakuwa na majira ya baridi kali. Kwa kweli, Mungu ndiye aliyeahidi: “Siku zote ambazo dunia inaendelea kuwapo, kupanda mbegu na kuvuna, baridi na joto, majira ya kiangazi na majira ya baridi kali, mchana na usiku, havitakoma kamwe.”—Mwanzo 8:22.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 6 Ona Kalenda ya Mashahidi wa Yehova ya 2004, Julai/Agosti.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 9]

Mwezi Ni Muhimu kwa Uhai

Kwa muda mrefu, wanadamu wameshangazwa na kusisimuliwa na mwezi. Lakini je, unajua kwamba mwezi huathiri majira? Mwezi husaidia dunia iweze kuinama kwenye mhimili wake. Jambo hilo “ni muhimu sana katika kutokeza hali Duniani zinazoweza kutegemeza uhai,” asema Andrew Hill, mwandishi mmoja wa sayansi. Kama mwezi haungekuweko ili kuisaidia dunia iiname kwenye mhimili wake, kungekuwa na joto kali sana ambalo yaelekea lingefanya kusiwe na uhai duniani. Hivyo, kikundi cha wanaanga kilimalizia kwa kusema hivi: “Mtu anaweza kuuona Mwezi kuwa ndio unaodhibiti mabadiliko ya halihewa Duniani.”—Zaburi 104:19.

[Hisani]

Moon: U.S. Fish & Wildlife Service, Washington, D.C./Bart O’Gara

[Picha katika ukurasa wa 9]

Ngamia, Afrika Kaskazini na Peninsula ya Arabia