Kuchunguza Hazina ya Chester Beatty
Kuchunguza Hazina ya Chester Beatty
ALIYEKUWA msimamizi wa Maktaba ya Chester Beatty huko Dublin, Ireland, R. J. Hayes, alitoa maelezo haya mafupi kuhusu maktaba hiyo: “Ina vitu vingi sana vyenye thamani vya staarabu nyingi sana zilizotoweka, . . . michoro yake midogo na mikubwa inavutia sana.” Maktaba hiyo ina mkusanyo wa vitu vya kale vyenye thamani kubwa, sanaa yenye kuvutia, vitabu na hati zisizopatikana kwa urahisi ambazo thamani yake haikadiriki. Kwa hiyo, Chester Beatty alikuwa nani? Naye alikusanya vitu gani vyenye thamani?
Mababu wa Alfred Chester Beatty, aliyezaliwa mwaka wa 1875 huko New York, Marekani, walitoka Scotland, Ireland, na Uingereza. Kufikia wakati alipokuwa na umri wa miaka 32, Beatty alikuwa tajiri sana kwa kuwa alifanya kazi kama injinia na mshauri wa mambo ya migodi. Katika maisha yake yote, alitumia mali yake nyingi kukusanya vitu bora na vyenye kuvutia. Alipokufa mwaka wa 1968 akiwa na umri wa miaka 92, Beatty aliwaachia watu wa Ireland vitu vyote alivyokusanya.
Alikusanya Nini?
Beatty alikusanya vitu vingi tofauti-tofauti. Asilimia 1 tu ya vitu hivyo ndiyo huonyeshwa kwa wakati mmoja. Alikusanya vitu visivyopatikana kwa urahisi na vyenye thamani katika wakati na tamaduni tofauti-tofauti zinazohusisha maelfu ya miaka. Kutoka Ulaya alikusanya vitu vya enzi za kati na kile kipindi cha Mwamko wa Elimu na Maarifa, na pia akakusanya vingine kutoka nchi nyingi za Asia na Afrika. Kwa mfano, picha zilizochongwa kwenye mbao ambazo alikusanya kutoka Japani, ndizo hufikiriwa kuwa bora zaidi ulimwenguni.
Tofauti kabisa na mkusanyo wa vitu vya sanaa, kuna mkusanyo mwingine wenye kuvutia wa mabamba ya udongo kutoka Babiloni na Sumeria, ambayo yana maandishi ya zamani ya kikabari. Watu walioishi Mesopotamia miaka zaidi ya 4,000 iliyopita waliandika habari nyingi sana kuhusu maisha yao kwenye mabamba ya udongo mbichi, ambayo yalikaushwa baadaye. Mabamba mengi kama hayo yapo hata leo, nayo huthibitisha kwamba sanaa ya uandishi ni ya zamani sana.
Alivutiwa na Vitabu
Inaonekana kwamba Chester Beatty alivutiwa na ustadi wa kutengeneza vitabu bora. Alikusanya maelfu ya mabuku ya kidini na ya kilimwengu, kutia ndani nakala fulani za Kurani ambazo zilikuwa zimerembeshwa kwa ustadi sana. Mwandishi mmoja anasema kwamba, Beatty “alivutiwa sana na ukubwa wa herufi za maandishi ya Kiarabu, . . . na upendezi wake wa rangi ulichochewa na maandishi yaliyorembeshwa kwa dhahabu, fedha, na madini mengine yaliyong’aa.”
Mawe ya yashefi yalimvutia Chester Beatty kama yalivyowavutia watawala wa China wa karne zilizopita. Waliyaona mawe mazuri ya yashefi kuwa yenye thamani zaidi kuliko madini yote, hata kuliko dhahabu. Watawala hao waliwaagiza wasanii stadi kugeuza vipande vya mawe hayo kuwa karatasi nyembamba na laini. Kisha wasanii wenye vipawa wakajaza kurasa hizo kwa maandishi na michoro ya dhahabu, na hivyo kutengeneza vitabu vyenye kustaajabisha zaidi kuwahi kutengenezwa. Mkusanyo wa Beatty wa vitu hivyo ni maarufu sana ulimwenguni.
Hati za Biblia Zenye Thamani Kubwa
Watu wanaoipenda Biblia huuona mkusanyo mkubwa wa Chester Beatty wa hati za Biblia za kale na za enzi za kati, kuwa wenye thamani zaidi kuliko vitu
vingine vyote alivyokusanya. Hati zilizorembeshwa huonyesha kwamba waandishi waliozinakili kwa mkono walikuwa wasanii wenye subira. Vitabu vilivyochapwa vinaonyesha ustadi na usanii wa wajalidi na wachapaji wa vitabu wa zamani. Kwa mfano, Biblia Latina ilichapwa huko Nuremberg mwaka wa 1479 na Anton Koberger, ambaye aliishi wakati mmoja na Johannes Gutenberg, naye anatajwa kuwa “mmojawapo wa wachapaji muhimu zaidi na wenye bidii zaidi wa zamani.”Hati moja ya ngozi iliyoandikwa zamani katika karne ya nne na Ephraem, msomi Msiria, ni kati ya vitu vya kipekee ambavyo vimeonyeshwa kwenye Maktaba ya Chester Beatty. Ephraem ananukuu sana kitabu cha karne ya pili kiitwacho Diatessaron. Tatian, ambaye aliandika kitabu hicho, aliunganisha masimulizi ya Injili zote nne kuhusu maisha ya Yesu Kristo kuwa kitabu kimoja. Waandishi wa baadaye walirejelea kitabu Diatessaron, lakini sasa nakala za kitabu hicho hazipatikani tena. Wasomi fulani wa karne ya 19 hata walitilia shaka kama kulikuwa na kitabu kama hicho. Hata hivyo, mnamo 1956 Beatty alipata ufafanuzi wa Ephraem kuhusu kitabu hicho cha Tatian, Diatessaron. Kupatikana kwa ufafanuzi huo kulikuwa uthibitisho zaidi kwamba Biblia ni ya kweli kabisa.
Hati za Mafunjo Zenye Thamani Kubwa
Beatty pia alikusanya hati nyingi sana za mafunjo, za kidini na za kilimwengu. Zaidi ya kodeksi (vitabu vya kale vilivyoandikwa kwa mkono) 50 za mafunjo ni za kabla ya karne ya nne W.K. Baadhi ya mafunjo hayo yaliokolewa katika marundo makubwa ya mafunjo—hasa katika jaa la kutupia taka za karatasi—ambayo yalibaki bila kugunduliwa kwa karne nyingi katika jangwa la Misri. Mafunjo mengi yalikuwa yamechakaa sana yalipotolewa ili kuuzwa. Wauzaji walileta masanduku yaliyojaa vipande vya mafunjo. “Wale waliotaka kununua waliingiza mkono tu na kutoa kipande kilichokuwa kikubwa zaidi na chenye maandishi mengi zaidi,” asema Charles Horton, msimamizi wa sehemu ya Maktaba ya Chester Beatty yenye sanaa kutoka nchi za Magharibi.
Horton anasema, “Ugunduzi wenye kutokeza zaidi” wa Beatty ulitia ndani kodeksi za Biblia zenye thamani ambazo zilitia ndani “baadhi ya nakala za Agano la Kale na Jipya za Kikristo zilizojulikana kuwa za zamani zaidi.” Wauzaji wa kodeksi waliojua thamani yake walizirarua ili kuziuza zikiwa vipande-vipande kwa wanunuzi mmoja-mmoja. Hata hivyo, Beatty alikuwa na uwezo wa kununua nyingi za kodeksi hizo. Lakini, kodeksi hizo zina umuhimu gani? Bwana Frederic Kenyon anaeleza kugunduliwa kwa kodeksi hizo kuwa “ugunduzi muhimu zaidi” tangu Tischendorf agundue Kodeksi ya Sinai mwaka wa 1844.
Kodeksi hizi ni za kati ya karne ya pili na ya nne W.K. Kati ya vitabu vya Maandiko ya Kiebrania katika tafsiri ya Septuajinti ya Kigiriki, kuna nakala mbili za kitabu cha Mwanzo. Kenyon anasema kwamba vitabu hivyo vina thamani ya kipekee “kwa sababu karibu kitabu chote [cha Mwanzo] kinakosekana katika kodeksi za Vatikani na Sinai,” ambazo ni kodeksi za ngozi za karne ya nne. Kodeksi tatu zina vitabu vya Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo. Moja ina sehemu kubwa ya zile Injili nne na pia sehemu kubwa ya kitabu cha Matendo. Kodeksi ya pili, yenye kurasa za ziada ambazo Beatty alipata baadaye, ina karibu barua zote za mtume Paulo, kutia ndani ile aliyowaandikia Waebrania. Kodeksi ya tatu ina theluthi tatu za kitabu cha Ufunuo. Kenyon anasema kwamba mafunjo hayo
“yameimarisha uhakika wetu hata zaidi katika maandishi ya Agano Jipya tuliyo nayo sasa.”Maandishi ya Biblia kwenye mafunjo katika Maktaba ya Chester Beatty yanaonyesha kwamba, Wakristo walianza mapema sana kutumia kodeksi, au vitabu vyenye kurasa badala ya zile hati nzito za kukunjwa, yaelekea kabla ya mwisho wa karne ya kwanza W.K. Pia mafunjo hayo yanaonyesha kwamba, kwa sababu ya uhaba wa vifaa vya kuandikia, mara nyingi wanakili walitumia mafunjo ya zamani yaliyokuwa tayari yametumiwa. Kwa mfano, kodeksi moja ya Koptiki yenye sehemu ya Injili ya Yohana imeandikwa “katika kile kinachoonekana kuwa kitabu cha shule chenye hesabu za Kigiriki.”
Maandishi hayo ya mafunjo hayavutii, lakini yana thamani kubwa sana. Mafunjo hayo yanatusaidia kuelewa mwanzo wa Ukristo. “Hapa mbele yenu,” asema Charles Horton, “mnaweza kuona aina ya vitabu vilivyotumiwa na baadhi ya jamii za kale zaidi za Wakristo—vitabu ambavyo walivithamini sana.” (Methali 2:4, 5) Ikiwa utakuwa na nafasi ya kuchunguza baadhi ya hazina hizo katika Maktaba ya Chester Beatty, utafurahi.
[Picha katika ukurasa wa 31]
Picha kutoka Japani zilizochongwa kwenye mbao na Katsushika Hokusai
[Picha katika ukurasa wa 31]
“Biblia Latina” ilikuwa mojawapo ya nakala za Biblia za zamani zaidi zilizochapwa
[Picha katika ukurasa wa 31]
Ufafanuzi wa Ephraem kuhusu kitabu “Diatessaron” cha Titian unatoa uthibitisho zaidi kwamba Biblia ni ya kweli
[Picha katika ukurasa wa 31]
Kodeksi ya Chester Beatty P45 ambayo ndiyo mojawapo ya kodeksi za zamani zaidi ulimwenguni, ina sehemu kubwa ya zile Injili nne na pia sehemu kubwa ya kitabu cha Matendo katika buku moja
[Picha katika ukurasa wa 31]
All images: Reproduced by kind permission of The Trustees of the Chester Beatty Library, Dublin
[Picha katika ukurasa wa 29]
All images: Reproduced by kind permission of The Trustees of the Chester Beatty Library, Dublin