Urithi Unaoweza Kuutumaini
Urithi Unaoweza Kuutumaini
“UKIPOKEA taarifa kutoka kwa mtu fulani kwamba kuna mali fulani unayoweza kurithi, jihadhari. Labda unadanganywa.”
Hilo ni onyo ambalo Shirika la Kukagua Barua la Marekani liliweka kwenye kituo chake cha Intaneti. Kwa nini? Kwa sababu watu wengi sana walipata taarifa kupitia barua iliyosema, ‘Mtu fulani wa ukoo wako amekufa naye amekuachia urithi.’ Kwa sababu hiyo, wengi walituma kwa njia ya posta malipo ya dola 30 au zaidi za Marekani, ili wapate ‘ripoti ya urithi’ ambayo ingeeleza mahali ulipo urithi huo na jinsi ya kuudai. Walikatishwa tamaa sana. Wote waliojibu barua hizo walikuwa wamepata taarifa ileile, lakini hapakuwa na uwezekano wa kurithi chochote.
Njama hizo huvutia watu kwa kuwa wana ile tamaa ya asili ya kupokea urithi. Lakini, Biblia husema kwa njia ifaayo kuhusu wale wanaoacha urithi inaposema: “Mtu mwema atawaachia urithi wana wa wanawe.” (Methali 13:22) Bila shaka, Yesu Kristo mwenyewe ndiye aliyesema maneno haya maarufu na yanayopendwa sana katika Mahubiri yake ya Mlimani: “Heri wenye upole; maana watairithi nchi.”—Mathayo 5:5, Union Version.
Maneno ya Yesu hutukumbusha jambo hili ambalo Mfalme Daudi wa Israeli la kale aliongozwa na roho ya Mungu kuandika karne nyingi awali: “Wenye upole watairithi nchi, watajifurahisha kwa wingi wa amani.”—Zaburi 37:11, UV.
Ni tarajio zuri kama nini ‘kuirithi nchi’! Lakini je, tunaweza kuwa na hakika kwamba hii si njama nyingine yenye hila kama ile iliyotangulia kutajwa? Ndiyo tunaweza kuwa na hakika. Kwa kuwa dunia ni sehemu ya uumbaji wa Yehova wenye kustaajabisha, yeye akiwa Mfanyi na Mmiliki wa uumbaji huo ana haki kisheria kumpa yeyote atakaye. Kupitia Mfalme Daudi, Yehova alitoa ahadi hii ya kinabii kwa Mwanaye mpendwa, Yesu Kristo: “Niombe, ili nikupe mataifa yawe urithi wako na miisho ya dunia iwe miliki yako mwenyewe.” (Zaburi 2:8) Kwa sababu hiyo, mtume Paulo alimtaja Yesu kuwa yule ‘ambaye Mungu alimweka rasmi kuwa mrithi wa vitu vyote.’ (Waebrania 1:2) Kwa hiyo, tunaweza kuwa na uhakika kamili kwamba Yesu aliposema wapole “watairithi nchi,” alifanya hivyo kwa nia nzuri, naye alikuwa na mamlaka yafaayo kutimiza ahadi yake.—Mathayo 28:18.
Hivyo basi, ni muhimu kuuliza, Ahadi hiyo itatimizwa jinsi gani? Kila mahali tunapotazama leo, inaonekana kwamba watu wenye ugomvi na wenye msimamo mkali ndio hufanikiwa zaidi, nao hupata wanachotaka.
Hivyo, wapole watarithi nini? Isitoshe, dunia imejaa matatizo yanayotokana na uchafuzi wa hewa, nazo mali zake za asili zinatumiwa isivyofaa na watu wenye pupa na wasiojali hali ya baadaye. Je, kweli kutakuwa na dunia inayofaa kurithiwa? Tunakualika usome makala ifuatayo ili upate jibu kwa maswali haya na mengine muhimu.[Picha katika ukurasa wa 3]
Je, utapata urithi halisi?