Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Maswali Kutoka kwa Wasomaji

Maswali Kutoka kwa Wasomaji

Maswali Kutoka kwa Wasomaji

Kwa nini Yesu aliyefufuliwa alimwambia Tomaso amguse na hali alikuwa amemkataza Maria Magdalene kufanya hivyo hapo awali?

Tafsiri nyingine za zamani za Biblia hutoa wazo la kwamba Yesu alimwambia Maria Magdalene asimguse. Kwa mfano, Zaire Swahili Bible inafasiri hivi maneno ya Yesu: “Usiniguse, kwa sababu sijapanda kwa Baba yangu.” (Yohana 20:17) Hata hivyo, kitenzi cha awali cha Kigiriki ambacho nyakati nyingine hutafsiriwa “gusa,” humaanisha “ng’ang’ania, ning’inia, shikilia, shika, kamata.” Kwa kufaa, Yesu hakuwa akimkataza Maria Magdalene asimguse, kwa kuwa muda mfupi baada ya hapo aliwaruhusu wanawake wengine waliokuwa kwenye kaburi lake ‘wamshike miguu.’—Mathayo 28:9.

Tafsiri nyingi za kisasa kama vile Biblia Takatifu—Tafsiri ya Ulimwengu Mpya, The New Jerusalem Bible, na The New English Bible, hutusaidia kuelewa maana halisi ya maneno ya Yesu: “Acha kuning’ang’ania.” Kwa nini Yesu alimwambia hivyo Maria Magdalene ambaye alikuwa rafiki yake wa karibu?—Luka 8:1-3.

Yaelekea Maria Magdalene alihofia kwamba Yesu alikuwa karibu kuondoka na kupaa mbinguni. Akitamani sana kuwa na Bwana wake, alimshikilia Yesu kwa nguvu ili asiende. Ili kumhakikishia kwamba hakuwa anaondoka wakati huo, Yesu alimwambia Maria aache kumng’ang’ania na badala yake aende kuwaambia wanafunzi wake habari za kufufuliwa kwake.—Yohana 20:17.

Mazungumzo kati ya Yesu na Tomaso yalikuwa tofauti. Yesu alipowatokea wanafunzi fulani, Tomaso hakuwepo. Baadaye, Tomaso alitilia shaka kufufuliwa kwa Yesu, akisema kwamba hangeamini mpaka aone majeraha ya Yesu yaliyosababishwa na misumari na kutia mkono wake ndani ya upande ambao Yesu alidungwa kwa mkuki. Siku nane baadaye, Yesu aliwatokea tena wanafunzi wake. Wakati huu Tomaso alikuwepo, naye Yesu alimwambia aguse majeraha yake.—Yohana 20:24-27.

Hivyo, kwa habari ya Maria Magdalene, Yesu alikuwa akishughulika na mtu aliyetaka kumzuia isivyofaa asiondoke; kwa habari ya Tomaso, Yesu alikuwa akimsaidia mtu mwenye shaka. Katika visa vyote viwili, Yesu alikuwa na sababu nzuri ya kutenda alivyotenda.