Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Sifa Inayopatikana Tu Katika Wanadamu

Sifa Inayopatikana Tu Katika Wanadamu

Sifa Inayopatikana Tu Katika Wanadamu

Jodie hukagua thamani ya mali zilizoachwa kama urithi. Anamsaidia mwanamke mmoja kuuza vifaa vya nyumbani vya dada yake aliyekufa. Anapoangalia mahali pa kuwashia moto, anaona masanduku mawili ya zamani yanayotumiwa kuweka vifaa vya uvuvi. Anapotazama ndani ya mojawapo ya masanduku hayo, haamini macho yake. Kuna mabunda ya noti za dola 100 zilizofungwa kwa karatasi ya alumini—jumla ya dola 82,000 pesa taslimu! Jodie yuko peke yake chumbani. Anapaswa kufanya nini? Je, atachukua sanduku hilo kimya-kimya au atamwambia mteja wake kwamba amepata pesa hizo?

HALI yenye kutatanisha inayomkabili Jodie inakazia mojawapo ya sifa ambazo hututofautisha na wanyama. Kichapo The World Book Encyclopedia kinasema: “Mojawapo ya sifa za pekee za wanadamu ni uwezo wa kufikiria yale tunayopaswa kufanya na yale tusiyopaswa kufanya.” Mbwa mwenye njaa anapopata kipande cha nyama mezani hatafikiria kama anapaswa kula nyama hiyo au hapaswi. Hata hivyo, Jodie ana uwezo wa kuchanganua kama uamuzi wake unapatana na maadili. Akichukua pesa hizo, atakuwa ameiba, lakini huenda asijulikane. Pesa hizo si zake; lakini mteja wake hana habari yoyote kuzihusu. Mbali na hilo, watu wengi katika jamii ya Jodie watamwona kuwa mjinga ikiwa atampa mteja wake pesa hizo.

Ungefanya nini iwapo ungejikuta katika hali kama hiyo? Jibu lako litategemea viwango vya maadili ambavyo umeamua kufuata.

Maadili Ni Nini?

Maadili yamefafanuliwa kuwa “uchunguzi wa maswali kuhusu mambo yanayofaa na yasiyofaa.” (Collins Cobuild English Dictionary) Mwandishi Eric J. Easton anasema: “Maneno ya Kigiriki na Kilatini yanayotafsiriwa ‘maadili’ yana maana moja na yote hurejelea jinsi watu wanavyoishi.”

Kwa muda mrefu, watu wamekuwa wakiishi kwa kufuata viwango vya maadili vilivyowekwa na dini. Neno la Mungu, Biblia, limekuwa na uvutano wenye nguvu katika jamii nyingi. Hata hivyo, watu wengi ulimwenguni wamepuuza viwango mbalimbali vya kidini kuwa visivyofaa na kwamba kanuni za maadili za Biblia zimepitwa na wakati. Pengo hilo limejazwa na nini? Kitabu Ethics in Business Life kinasema kwamba “maoni ya kilimwengu . . . yamechukua mahali pa mamlaka ya kidini ambayo yalifuatwa zamani.” Badala ya kutegemea dini iwawekee viwango vya maadili, wengi hutafuta mwongozo kutoka kwa wataalamu wa kilimwengu wa masuala ya maadili. Mtaalamu wa masuala ya maadili Paul McNeill anasema: “Nafikiri wataalamu wa maadili wamechukua daraka la makasisi. . . . Leo watu wanaongozwa na maadili badala ya kuongozwa na dini kama ilivyokuwa hapo zamani.”

Unapokabili maamuzi mazito, wewe hutofautishaje yaliyo sawa na yaliyo makosa? Je, Mungu ndiye huamua viwango vya maadili utakavyofuata au wewe hujiamulia mwenyewe?