Kwa Nini Vita Vya Maneno Huumiza?
Kwa Nini Vita Vya Maneno Huumiza?
“Vita vinatoka chanzo gani na mapigano yanatoka chanzo gani katikati yenu?”—YAKOBO 4:1.
MWANDIKAJI wa Biblia Yakobo hakuelekeza swali hilo kwa askari-jeshi wa vikosi vya Roma, ambao wakati huo walikuwa wakipigana vita vya ushindi; wala hakuwa akichunguza nia ya wanamgambo Wayahudi wa Wasikarii, au wanaume waliokuwa wakipigana kwa kutumia visu, wa karne ya kwanza W.K. Yakobo alikuwa akizungumzia ugomvi ambao ulihusisha angalau watu wawili. Kwa nini? Kwa sababu sawa na vita halisi, vita vya maneno huleta madhara. Ona masimulizi yafuatayo ya Biblia.
Wana wa mzee wa ukoo Yakobo walimchukia sana ndugu yao Yosefu hivi kwamba wakamuuza utumwani. (Mwanzo 37:4-28) Baadaye, Mfalme Sauli wa Israeli alijaribu kumuua Daudi. Kwa nini? Kwa sababu alimwonea Daudi wivu. (1 Samweli 18:7-11; 23:14, 15) Katika karne ya kwanza, wanawake wawili Wakristo, Euodia na Sintike, walivuruga amani ya kutaniko zima kwa sababu ya ugomvi wao.—Wafilipi 4:2.
Katika nyakati za hivi karibuni, wanaume walisuluhisha tofauti zao kwa kupigana huku wakipambana kwa visu au bastola. Mara nyingi mmoja wa wapiganaji hao aliuawa au kulemazwa kabisa. Leo, watu wenye uadui hupigana kwa kutumia maneno makali na yenye kuumiza. Ingawa huenda damu isimwagike, kushambulia kwa maneno huumiza hisia na kumharibia mtu sifa. Katika “vita” hivyo, mara nyingi watu wasio na hatia ndio huumia.
Fikiria yale yaliyotukia miaka kadhaa iliyopita kasisi mmoja Mwanglikana alipomshutumu kasisi mwingine kwamba alikuwa akitumia vibaya pesa za kanisa. Ugomvi wao ulijulikana na kila mtu, na kutaniko walilokuwa wakitumikia likagawanyika mara mbili. Baadhi ya washiriki walikataa kuhudhuria ibada ikiwa kasisi waliyempinga ndiye aliyekuwa akiongoza ibada. Washiriki wa kanisa walichukiana sana hivi kwamba hawangeweza kuzungumziana walipokuwa wakiabudu
kanisani. Kasisi aliyemshutumu mwenzake yeye pia aliposhutumiwa kwa sababu ya mwenendo wake mpotovu wa kingono, ugomvi huo uliongezeka.Askofu Mkuu wa kanisa la Canterbury aliwasihi makasisi hao wawili waache ugomvi wao, na kuutaja kuwa “kansa” na “aibu inayofanya jina la Bwana Wetu lisiheshimiwe.” Mnamo mwaka wa 1997, mmoja wa makasisi hao alikubali kustaafu. Yule mwingine aliendelea na kazi hadi alipolazimika kustaafu kwa sababu ya umri wake. Hata hivyo, aliendelea na kazi hadi dakika ya mwisho, naye akastaafu Agosti 7, 2001, alipofikisha umri wa miaka 70. Gazeti The Church of England Newspaper lilisema kwamba siku ambayo alistaafu ilikuwa sikukuu ya “Mtakatifu” Victricius. “Mtakatifu” Victricius alikuwa nani? Alikuwa askofu wa karne ya nne ambaye inaripotiwa kwamba alipigwa kwa sababu ya kukataa kupigana jeshini. Likionyesha tofauti katika mitazamo ya watu hao wawili, gazeti hilo lilisema: “Akionyesha mtazamo uliokuwa tofauti na ule wa “Mtakatifu” Victricius, [Kasisi aliyestaafu] alikuwa tayari kupambana na kasisi mwingine.”
Makasisi hao wangeweza kuepuka kuumizana na kuwaumiza wengine ikiwa wangefuata shauri linalopatikana kwenye Waroma 12:17, 18: “Msimlipe yeyote uovu kwa uovu. Fanyeni mambo mema machoni pa watu wote. Ikiwezekana, kwa kadiri inavyowategemea ninyi, iweni wenye kufanya amani na watu wote.”
Namna gani wewe? Mtu fulani akikukosea, je, wewe huchochewa na hasira na kuanzisha vita vya maneno? Au je, wewe huepuka maneno makali na hivyo kuwa tayari kufanya amani? Ukimkosea mtu mwingine, je, wewe humwepuka na kutarajia kwamba baada ya muda mtu huyo atasahau jambo hilo? Au je, wewe hufanya haraka kuomba msamaha? Iwe wewe ndiye unayeomba msamaha au wewe ndiye unayemsamehe mtu mwingine, kujaribu kufanya amani kutakusaidia uwe mwenye furaha zaidi. Shauri la Biblia linaweza kutusaidia kusuluhisha hata mizozo ya muda mrefu kama makala inayofuata inavyoonyesha.