Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Alipata Ushindi wa Pekee

Alipata Ushindi wa Pekee

Alipata Ushindi wa Pekee

JE, WEWE hupingwa kwa sababu ya imani yako ukiwa kazini, shuleni, nyumbani, au kwa sababu ya vizuizi vilivyowekwa na serikali? Ikiwa ndivyo, usivunjike moyo. Mashahidi wengi wa Yehova wamekabili majaribu kama hayo, nao wameyashinda. Hebu ona mfano wa Erna Ludolph.

Erna alizaliwa Lübeck, Ujerumani, mwaka wa 1908. Kati ya washiriki wote wa familia yao, yeye tu ndiye aliyemtumikia Yehova. Wakati serikali ya Hitler ilipoanza kutawala mwaka wa 1933, Mashahidi wa Yehova walikabili hali ngumu. Watu waliofanya kazi na Erna walimshutumu hadharani kwa kukataa kumpigia Hitler saluti. Hivyo, Erna akakamatwa na Wanazi. Kwa muda wa miaka minane, alifungwa katika magereza na kambi mbalimbali za mateso huko Hamburg-Fuhlsbüttel, Moringen, Lichtenburg, na Ravensbrück. Alipokuwa Ravensbrück, jambo fulani lilitokea ambalo lilimwezesha kupata ushindi.

Mfanyakazi wa Pekee

Profesa Friedrich Holtz na mke wake, Alice, waliishi Berlin. Hawakuwa wanachama wa Nazi wala hawakuunga mkono sera zake. Hata hivyo, walikuwa na uhusiano wa kiukoo na ofisa mmoja wa cheo cha juu kati ya walinzi wa Hitler, ambaye alisimamia baadhi ya wafungwa wa kambi za mateso. Hivyo, profesa huyo na mke wake walipokuwa wakitafuta mfanyakazi wa nyumbani, ofisa huyo aliwaruhusu kujichagulia mfungwa mwanamke. Mnamo Machi 1943, Alice alienda Ravensbrück kuchagua mfanyakazi. Unajua alimchagua nani? Si mwingine ila Erna Ludolph. Erna alianza kuishi na familia ya Holtz, nao walimtendea vizuri. Baada ya vita kumalizika, alihama pamoja na familia hiyo hadi eneo la Halle kwenye Mto Saale. Akiwa huko, Erna alikabili upinzani tena, wakati huu kutoka kwa Wasoshalisti wa Ujerumani Mashariki. Mwaka wa 1957, familia ya Holtz ililazimishwa kuhamia Ujerumani Magharibi, na Erna akahama pamoja nao. Hatimaye, Erna aliweza kuabudu kwa uhuru.

Erna alipataje ushindi wa pekee? Alice Holtz na watoto wake watano walibatizwa wakawa Mashahidi wa Yehova kwa sababu ya mwenendo mzuri wa Erna na ustadi wake wa kuhubiri ujumbe wa Biblia. Isitoshe, wajukuu 11 wa Alice ni Mashahidi pia. Kwa sasa, wawili kati yao wanatumika katika ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova huko Selters, Ujerumani. Susanne, mmoja wa binti za Alice, anasema: “Familia yetu imepata kweli hasa kwa sababu ya mfano mzuri wa Erna.” Erna alipata thawabu kubwa kwa kuvumilia. Namna gani wewe? Wewe pia unaweza kupata thawabu kubwa kwa kuvumilia hali ngumu kwa uaminifu. Naam, ukiwa na mwenendo mzuri na ukihubiri kwa ustadi, unaweza kupata ushindi wa pekee. *

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 6 Makala hii ilipokuwa ikitayarishwa, Erna Ludolph alikufa akiwa na umri wa miaka 96. Alikuwa mwaminifu hadi kifo.

[Picha katika ukurasa wa 31]

Erna Ludolph (ameketi) pamoja na washiriki wa familia ya Holtz