Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ujasiri Licha ya Upinzani

Ujasiri Licha ya Upinzani

Ujasiri Licha ya Upinzani

GAYO na Aristarko, marafiki wawili wa mtume Paulo, walilazimishwa na umati wenye hasira kuingia ndani ya jumba la maonyesho la Efeso. Humo, umati huo ulipaaza sauti hivi kwa muda wa saa mbili: “Artemi wa Waefeso ni mkuu!” (Matendo 19:28, 29, 34) Je, marafiki hao wa Paulo walisimama imara walipokabili upinzani huo? Na ni nini kilichosababisha hali hiyo?

Paulo alikuwa amepata mafanikio alipohubiri katika jiji la Efeso kwa miaka mitatu hivi. Hivyo, Waefeso wengi walikuwa wameacha kuabudu sanamu. (Matendo 19:26; 20:31) Sanamu iliyotumiwa katika Efeso ilikuwa hekalu ndogo la fedha la Artemi, mungu wa kike wa uzazi, ambaye hekalu lake kubwa lilikuwa katika jiji hilo. Sanamu hizo ndogo za hekalu zilivaliwa kama hirizi au ziliwekwa ndani ya nyumba. Bila shaka, Wakristo hawangenunua sanamu hizo.—1 Yohana 5:21.

Demetrio, mmoja wa mafundi wa fedha, aliamini kwamba huduma ya Paulo ilihatarisha biashara yao yenye faida kubwa. Kwa kutia maneno yake chumvi, Demetrio aliwasadikisha mafundi wengine wa fedha kwamba watu katika maeneo yote ya Asia Ndogo wataacha kumwabudu Artemi. Mafundi hao wa fedha walipoanza kupaaza sauti na kumsifu Artemi, fujo zilizuka na jiji lote likajaa mvurugo.—Matendo 19:24-29.

Maelfu ya watu walikusanyika katika jumba la maonyesho, ambalo lilikuwa na viti vya kutosha kukaliwa na watazamaji 25,000. Paulo alitaka kuuhutubia umati huo wenye hasira, lakini maofisa wenye urafiki wakamsadikisha asifanye hivyo. Hatimaye, karani wa jiji alifaulu kuunyamazisha umati huo, na Gayo na Aristarko wakanusurika.—Matendo 19:35-41.

Leo, huenda watu wa Mungu wakakabili upinzani na ghasia wanapohubiri. Mara nyingi wao huhubiri habari njema katika majiji yaliyojaa ibada ya sanamu, ukosefu wa adili, na uhalifu. Hata hivyo, wao huiga ujasiri wa mtume Paulo, ambaye ‘hakuepuka kufundisha hadharani na nyumba kwa nyumba’ katika jiji la Efeso. (Matendo 20:20) Pia, wao hushangilia wanapoona kwamba ‘neno la Yehova linazidi kukua na kusitawi.’—Matendo 19:20.

[Picha katika ukurasa wa 30]

Mabaki ya jumba la maonyesho la Efeso