Je, Mwanadamu Anaweza Kuukomesha Umaskini?
Je, Mwanadamu Anaweza Kuukomesha Umaskini?
MAMILIONI ya watu wamelelewa bila kukabili umaskini. Hakuna wakati ambapo wamelala njaa au kupigwa na baridi wanapolala. Lakini wengi wao huwahurumia maskini nao hujitahidi sana kuwasaidia.
Hata hivyo, umaskini ni shida kubwa kwa watu wanaokumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe, mafuriko, ukame, na matatizo mengine. Mambo hayo huwahangaisha wakulima wa Afrika wanaokuza mazao ili kupata riziki. Baadhi yao wamelazimika kuondoka makwao na kwenda katika miji mikuu au kukimbilia nchi nyingine. Wakaaji wengine wa mashambani huhamia mjini wanapoambiwa kwamba maisha yatakuwa bora huko.
Mara nyingi msongamano wa watu katika miji huchangia umaskini. Nafasi ya kukuza mazao huwa ndogo au hukosekana kabisa. Inakuwa vigumu kupata kazi. Wengi huwa wahalifu wanapokata tamaa kabisa. Wakaaji wa mijini huomba msaada, lakini serikali za wanadamu haziwezi kutatua tatizo la umaskini ambalo linaongezeka. Gazeti The Independent la London lilisema hivi kuhusu ripoti moja ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa mnamo Novemba 2003: “Njaa inaongezeka ulimwenguni.” Kisha likasema: “Ulimwenguni pote, watu wapatao milioni 842 hawapati chakula cha kutosha, na idadi hiyo inaongezeka, huku watu wengine milioni 5 wakikumbwa na njaa kila mwaka.”
Nyakati nyingine, watu wanaokumbwa na umaskini huiandikia ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova nchini Afrika Kusini. Kwa mfano, mtu mmoja anayeishi Bloemfontein aliandika hivi: “Sina kazi, nami huiba mjini ninapopata nafasi. Nisipofanya hivyo, sisi hulala njaa kwa siku kadhaa na hata kupigwa na baridi kali. Hakuna kazi kabisa. Wengi wanazunguka mitaani wakitafuta kazi na chakula. Ninawajua wengine ambao huchokora-chokora takataka wakitafuta chakula. Wengine hujiua. Wengi wameshuka moyo na kukata tamaa kama mimi. Inaonekana hali hazitabadilika. Je, Mungu aliyetuumba na uhitaji wa kula na kuvaa haoni mambo hayo?”
Kuna majibu yenye kufariji kwa maswali ya mtu huyo. Kama makala inayofuata inavyoonyesha, majibu hayo yanapatikana katika Neno la Mungu, Biblia.