Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mari—Jiji Maarufu la Kale la Jangwani

Mari—Jiji Maarufu la Kale la Jangwani

Mari—Jiji Maarufu la Kale la Jangwani

“NILIKUWA nimesisimuka sana usiku nilipoingia katika chumba changu cha kulala baada ya kusherehekea pamoja na wenzangu uvumbuzi wetu usiotarajiwa,” asema André Parrot, mchunguzi wa vitu vya kale kutoka Ufaransa. Mnamo Januari 1934, katika eneo la Tell Hariri, karibu na mji mdogo wa Abu Kemal, kwenye Mto Efrati huko Siria, Parrot na wenzake walivumbua sanamu yenye maandishi haya: “Lamgi-Mari, mfalme wa Mari, kuhani mkuu wa Enlil.” Walifurahia sana uvumbuzi huo.

Hatimaye, jiji la Mari lilikuwa limepatikana! Kwa nini wanafunzi wa Biblia wapendezwe na uvumbuzi huo?

Kwa Nini Wapendezwe na Jiji la Mari?

Ingawa maandishi ya zamani yanaonyesha kwamba jiji la Mari lilikuwako, haikujulikana mahali lilipokuwa. Waandishi wa Sumeria wanasema kwamba jiji la Mari lilikuwa makao ya familia ya kifalme ambayo huenda pindi moja ilitawala Mesopotamia yote. Kwa kuwa lilijengwa kwenye kingo za Mto Efrati, jiji hilo lilikuwa mahali panapofaa, kwenye makutano ya njia za wafanyabiashara, zilizounganisha Ghuba ya Uajemi na Ashuru, Mesopotamia, Anatolia, na Pwani ya Mediterania. Bidhaa zilizotia ndani mbao, vyuma, na mawe, ambazo hazikupatikana Mesopotamia, zilisafirishwa kupitia jiji la Mari. Ushuru uliotozwa bidhaa hizo ulilitajirisha sana jiji hilo, na kuliwezesha kulitawala eneo hilo. Hata hivyo, mamlaka yake yaliisha wakati Sargoni wa Akkad alipoishinda Siria.

Miaka 300 hivi baada ya ushindi wa Sargoni, jiji la Mari lilitawaliwa mfululizo na magavana wa kijeshi. Wakati huo, jiji hilo lilipata ufanisi wa kadiri fulani. Hata hivyo, wakati wa mtawala wake wa mwisho, Zimri-Lim, umaarufu wake ulikuwa umeanza kudidimia. Zimri-Lim alijaribu kuuimarisha utawala wake kupitia uvamizi mbalimbali wa kijeshi, mikataba, na mapatano ya ndoa. Lakini yapata mwaka wa 1760 K.W.K., Mfalme Hammurabi wa Babiloni alishinda jiji hilo na kuliharibu, na hivyo akakomesha kile ambacho Parrot alikiita “ustaarabu wa hali ya juu wa kale.”

Yalipoliharibu jiji la Mari, majeshi ya Hammurabi yaliwasaidia, bila kujua, wanahistoria na wachunguzi wa vitu vya kale wa siku hizi. Majeshi hayo yalipobomoa kuta za matofali yasiyochomwa, vifusi vilifunika majengo fulani ambayo katika sehemu nyingine yako meta tano chini ya vifusi hivyo. Hivyo, majengo hayo yakahifadhiwa. Wachunguzi hao wamevumbua mabomoko ya mahekalu, majumba ya wafalme, vitu mbalimbali vya kale, na maandishi mengi yanayoeleza kuhusu eneo hilo la kale lenye ustaarabu.

Kwa nini tupendezwe na mabomoko ya Mari? Fikiria wakati ambapo Abrahamu, mzee wa ukoo, aliishi. Abrahamu alizaliwa mwaka wa 2018 K.W.K., miaka 352 baada ya ile Gharika kuu. Kizazi chake kilikuwa cha kumi kuanzia Noa. Kwa kutii amri ya Mungu, Abrahamu aliondoka Uru, jiji la kwao, na kwenda Harani. Katika mwaka wa 1943 K.W.K., Abrahamu aliondoka Harani akaenda Kanaani, akiwa na umri wa miaka 75. “Wakati Abrahamu alipohama Uru kwenda Yerusalemu [huko Kanaani], jiji la Mari lilikuwako,” asema Paolo Matthiae, mchunguzi wa vitu vya kale wa Italia. Kwa hiyo, uvumbuzi wa jiji la Mari ni muhimu kwa sababu unaweza kutusaidia kuelewa jinsi hali zilivyokuwa wakati ambapo Abrahamu, mtumishi mwaminifu wa Mungu, aliishi. *Mwanzo 11:10–12:4.

Mabomoko Hayo Yanafunua Nini?

Watu wa Mari, sawa na watu wa sehemu nyingine za Mesopotamia, walipenda dini sana. Waliona kwamba watu wana wajibu wa kuitumikia miungu. Walitafuta kujua maoni ya miungu kabla ya kufanya maamuzi yoyote muhimu. Wachunguzi wa vitu vya kale wamepata magofu ya mahekalu sita. Mahekalu hayo yanatia ndani Hekalu la Simba (ambalo wengine hufikiri ni la Dagan, yaani, Dagoni, mungu anayetajwa katika Biblia), Ishtar, mungu wa kike wa uzazi, na pia Shamash, mungu wa jua. Mwanzoni, mahekalu hayo yalikuwa na sanamu ya mungu ambaye waabudu walimtolea sala na matoleo. Waabudu hao walitengeneza sanamu zenye kutabasamu zilizofanana nao ambazo zilionyesha jinsi walivyokaa walipotoa sala, kisha wakaziweka juu ya viti kwenye madhabahu. Waliamini kwamba sanamu hizo ziliwawakilisha na kurefusha ibada yao. Parrot anasema: “Sanamu [hizo], sawa na mshumaa unaotumiwa sana katika ibada ya Wakatoliki leo, zilimwakilisha muumini.”

Uvumbuzi wa pekee uliofanywa kwenye mabomoko ya Tell Hariri ni kugunduliwa kwa mabaki ya jumba la mfalme, ambalo limepewa jina la Mfalme Zimri-Lim, aliyekuwa mfalme wa mwisho kuishi humo. Louis-Hugues Vincent, mchunguzi wa vitu vya kale kutoka Ufaransa, alisema jumba hilo “ndilo jengo la kale la Mashariki lililojengwa kwa ustadi mkubwa sana.” Jumba hilo lililojengwa kwenye eneo la ekari sita, lilikuwa na vyumba 300 na nyua. Hata zamani, jumba hilo lilionwa kuwa mojawapo ya maajabu ya ulimwengu. Katika kitabu chake Ancient Iraq, Georges Roux anasema: “Jumba hilo lilikuwa maarufu sana hivi kwamba Mfalme wa Ugarit, aliyeishi kwenye pwani ya Siria, alikuwa tayari kumtuma mwanawe umbali wa kilometa 600 ndani ya nchi, kusudi tu aitembelee ‘nyumba ya Zimri-Lim.’”

Kabla ya kufika kwenye ua mkubwa, wageni waliingia katika jumba hilo la mfalme lenye ngome kupitia lango moja lenye minara. Zimri-Lim, mfalme wa mwisho wa Mari, aliketi kwenye kiti cha enzi kilichokuwa juu ya jukwaa aliposhughulikia mambo ya kijeshi, kibiashara, na kibalozi, na pia alipotoa hukumu na kupokea wageni na mabalozi. Kulikuwa na vyumba vya wageni, ambao walikaribishwa na mfalme kula na kunywa katika karamu zake kubwa. Walikula nyama ya ng’ombe iliyochomwa au kuchemshwa, nyama ya kondoo, swala, samaki, na kuku, ambazo ziliandaliwa pamoja na mchuzi uliotengenezwa kwa kitunguu saumu. Walikula pia mboga za aina mbalimbali na jibini. Baada ya mlo mkuu, wageni walikula matunda yaliyotoka tu kuchumwa, matunda yaliyokaushwa au kugandishwa kwa sukari, na keki zilizookwa katika miundo mbalimbali. Ili kukata kiu, wageni waliandaliwa pombe au divai.

Kulikuwa na mfumo wa kudumisha usafi katika jumba la mfalme. Bafu zilizovumbuliwa zina vyoo na beseni za kuogea zilizotengenezwa kwa udongo wa mfinyanzi uliochomwa. Sakafu na sehemu za chini za kuta za bafu hizo zilipakwa lami ili kuzuia maji yasipenye. Maji machafu yaliondolewa kupitia mifereji iliyotengenezwa kwa matofali, nayo mabomba ya udongo yaliyopakwa lami ili maji yasipenye bado yanatumika sasa, miaka 3,500 hivi baadaye. Wakati wake watatu wa mfalme waliposhikwa na ugonjwa unaoweza kusababisha kifo, maagizo makali yalitolewa. Mwanamke mwenye ugonjwa huo alipaswa kutengwa kabisa na wengine. “Hakuna mtu anayepaswa kutumia kikombe chake, kula pamoja naye, au kuketi kwenye kiti chake.”

Tunayoweza Kujifunza Kutokana na Mabamba ya Kale

Parrot na wenzake walivumbua mabamba ya kikabari 20,000 hivi yaliyoandikwa katika lugha ya Akkad. Mabamba hayo yalitumiwa kuandika barua na mambo ya uchumi na utawala. Ni theluthi moja tu ya habari zinazopatikana kwenye mabamba hayo ambazo zimechapishwa, nazo zimechapishwa katika mabuku 28! Mabuku hayo yana umuhimu gani? Jean-Claude Margueron, msimamizi wa Tume ya Kuchunguza Vitu vya Kale vya Mari, alisema: “Kabla ya mabamba ya Mari kuvumbuliwa, tulijua mambo machache sana kuhusu historia, utamaduni, na jinsi watu walivyoishi huko Mesopotamia na Siria muda mfupi baada ya mwaka wa 2000 K.W.K. Mabamba hayo yametusaidia kuandika habari nyingi zaidi na sahihi kuhusu kipindi hicho.” Kama Parrot alivyosema, kuna “ufanani wenye kushangaza kati ya watu wanaotajwa katika mabamba hayo na yale ambayo Agano la Kale linasema kuhusu kipindi cha Wazee wa Ukoo.”

Mabamba hayo yaliyovumbuliwa Mari pia hufafanua habari fulani katika Biblia. Kwa mfano, yanaonyesha kwamba “wakati huo lilikuwa jambo la kawaida kwa mfalme” kuchukua wake au masuria wa adui yake. Hivyo, shauri la msaliti Ahithofeli kwa Absalomu, mwana wa Mfalme Daudi kwamba alale na masuria wa babake, halikuwa jambo jipya.—2 Samweli 16:21, 22.

Eneo la Tell Hariri limechimbuliwa mara 41 tangu mwaka wa 1933. Hata hivyo, kwa sasa ni ekari 20 tu kati ya ekari 270 za jiji la Mari ambazo zimechimbuliwa. Yaelekea vitu vingi vyenye kuvutia vitavumbuliwa huko Mari, jiji maarufu la kale la jangwani.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 8 Pia, yaelekea kwamba Wayahudi waliohamishwa kwenda Babiloni baada ya Yerusalemu kuharibiwa mwaka wa 607 K.W.K., walipita karibu na mabomoko ya Mari.

[Ramani katika ukurasa wa 10]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Ghuba ya Uajemi

Uru

MESOPOTAMIA

Efrati

MARI

ASHURU

Harani

ANATOLIA

KANAANI

Yerusalemu

Bahari ya Mediterania (Bahari Kuu)

[Picha katika ukurasa wa 11]

Katika maandishi haya, Mfalme Iahdun-Lim wa Mari anajigamba kuhusu kazi yake ya ujenzi

[Picha katika ukurasa wa 11]

Kuvumbuliwa kwa sanamu hii ya Lamgi-Mari kulisaidia kutambua mahali jiji la Mari lilipokuwa

[Picha katika ukurasa wa 12]

Ebih-Il, ofisa wa Mari, akisali

[Picha katika ukurasa wa 12]

Jukwaa katika jumba la mfalme ambapo huenda sanamu fulani ya mungu wa kike ilisimama

[Picha katika ukurasa wa 12]

Mabomoko ya Mari yanayoonyesha jengo la matofali yasiyochomwa

[Picha katika ukurasa wa 12]

Bafu katika jumba la mfalme

[Picha katika ukurasa wa 13]

Bamba linaloonyesha ushindi wa Naram-Sin dhidi ya Mari

[Picha katika ukurasa wa 13]

Mabamba ya kikabari 20,000 hivi yalipatikana katika mabomoko ya jumba la mfalme

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 10]

◀ © Mission archéologique française de Tell Hariri - Mari (Syrie)

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 11]

Document: Musée du Louvre, Paris; statue: © Mission archéologique française de Tell Hariri - Mari (Syrie)

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 12]

Statue: Musée du Louvre, Paris; podium and bathroom: © Mission archéologique française de Tell Hariri - Mari (Syrie)

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 13]

Victory stele: Musée du Louvre, Paris; palace ruins: © Mission archéologique française de Tell Hariri - Mari (Syrie)