Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Watu Wanyoofu Humletea Yehova Sifa

Watu Wanyoofu Humletea Yehova Sifa

Ripoti ya Watangazaji wa Ufalme

Watu Wanyoofu Humletea Yehova Sifa

MASHAHIDI wa Yehova, vijana kwa wazee, wanajulikana duniani pote kwa unyoofu wao. Ona mifano inayofuata kutoka mabara matatu.

Msichana mmoja huko Nigeria mwenye umri wa miaka 17, anayeitwa Olusola, aliona mfuko mdogo uliokuwa umeanguka chini alipokuwa akirudi nyumbani baada ya shule. Aliuokota na kumpelekea mwalimu mkuu ambaye alihesabu pesa zilizokuwemo na kupata kwamba zilikuwa naira 6,200 (dola 45 hivi za Marekani). Mwalimu mkuu alirudisha mfuko huo kwa mwalimu aliyekuwa ameupoteza. Mwalimu huyo alimshukuru Olusola na kumpa naira 1,000 (dola 7 hivi za Marekani) na kumwambia azitumie kulipa karo ya shule. Wanafunzi wengine waliposikia kisa hicho walimdhihaki Olusola. Majuma machache baadaye, mwanafunzi mmoja alisema kwamba pesa zake zimeibwa, kwa hiyo walimu wakaombwa wawapekue wanafunzi. Yule mwalimu alimwambia Olusola hivi: “Wewe simama hapa. Najua kwamba wewe ni Shahidi wa Yehova na huwezi kuiba.” Wavulana wawili kati ya wale waliokuwa wamemdhihaki Olusola walipatikana na pesa hizo, nao wakaadhibiwa vikali. Olusola aliandika hivi: “Ninafurahi sana kwamba ninajulikana kuwa Shahidi wa Yehova, ambaye hawezi kamwe kuiba. Hivyo, ninamletea Yehova utukufu.”

Siku moja, Marcelo, ambaye ni mwenyeji wa Argentina, aliokota mkoba, meta chache tu kutoka kwenye mlango wa nyuma wa nyumba yake. Aliingiza mkoba huo ndani ya nyumba yake, kisha yeye na mke wake wakaufungua kwa uangalifu. Walishangaa sana kupata pesa nyingi, kadi za mikopo, na hundi kadhaa zilizotiwa sahihi, moja ikiwa ya peso milioni moja (dola 190,000 za Marekani). Ndani ya mkoba huo, walipata hati ya kibiashara iliyokuwa na namba ya simu. Walimpigia simu mwenyewe na kupanga kukutana naye mahali ambapo Marcelo anafanya kazi ili kumrudishia mkoba huo pamoja na vitu vilivyokuwemo. Mtu huyo alipofika, alionekana mwenye wasiwasi. Mwajiri wa Marcelo alimwambia mtu huyo atulie kwa kuwa Marcelo ni Shahidi wa Yehova. Mtu huyo alimpa Marcelo peso 20 tu (dola 6 hivi za Marekani) kama zawadi ya kumrudishia mkoba huo. Kwa kuwa mwajiri wa Marcelo alivutiwa sana na unyoofu wake, alikasirika kwa sababu Marcelo alipewa pesa kidogo. Hivyo Marcelo akapata nafasi ya kueleza kwamba yeye hutaka kuwa mnyoofu nyakati zote kwa sababu yeye ni Shahidi wa Yehova.

Kisa kinachofuata kilitukia Kyrgyzstan. Mvulana mmoja mwenye umri wa miaka sita, anayeitwa Rinat, alipata mfuko mdogo wa mwanamke jirani. Mfuko huo ulikuwa na som 1,100 (dola 25 hivi za Marekani). Rinat alipomrudishia mfuko huo, mwanamke huyo alihesabu pesa hizo na kumweleza mama ya Rinat kwamba som 200 (dola 5 hivi za Marekani) hazikuwepo. Rinat alisema kwamba hakuchukua pesa hizo. Wote walienda kuzitafuta, kisha wakazipata karibu na mahali ambapo mfuko huo ulipatikana. Mwanamke huyo alishangaa sana. Alimshukuru Rinat na mama yake, kwanza kwa sababu ya kurudisha pesa zilizopotea na pili, kwa sababu mama yake anamlea awe Mkristo.