Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kufasiri Ishara Ni Jambo Zito!

Kufasiri Ishara Ni Jambo Zito!

Kufasiri Ishara Ni Jambo Zito!

“Mwanzoni nilifikiri mwana wetu Andreas alikuwa akiumwa na kichwa tu. Hata hivyo, alipoteza hamu ya kula na akawa na joto sana. Maumivu ya kichwa yalizidi, nami nikaanza kuwa na wasiwasi. Mume wangu aliporudi nyumbani, tulimpeleka Andreas kwa daktari. Daktari alichunguza dalili za ugonjwa wa Andreas na kuagiza apelekwe hospitali mara moja. Tatizo lilikuwa kubwa zaidi. Andreas alikuwa na homa ya uti wa mgongo. Alitibiwa, na baada ya muda akapona.”—Gertrud, mama huko Ujerumani.

HUENDA wazazi wengi wamejionea hali kama hiyo. Wao huangalia dalili zinazoonyesha ikiwa mtoto wao ni mgonjwa. Ingawa si magonjwa yote yaliyo hatari, wazazi hawawezi kupuuza wanapoona mtoto wao akiwa na dalili za ugonjwa fulani. Kuona dalili na kuchukua hatua inayofaa kunaweza kusaidia sana. Hilo ni jambo zito.

Ndivyo ilivyo pia hata katika mambo yasiyohusiana na afya. Mfano mmoja ni ule msiba uliosababishwa na tsunami mnamo Desemba 2004 katika maeneo yaliyo karibu na Bahari ya Hindi. Mashirika ya serikali huko Australia na Hawaii yaligundua tetemeko kubwa la nchi kaskazini mwa Sumatra na kuona kimbele hatari ambayo ingetokea. Hata hivyo, hakukuwa na njia ya kuwasiliana na watu katika maeneo yaliyokuwa hatarini. Hivyo, zaidi ya watu 220,000 walikufa.

Ishara Zilizo Muhimu Zaidi

Yesu Kristo alipokuwa duniani, aliwafundisha wasikilizaji wake kuhusu kutazama ishara na kutenda kwa njia inayofaa. Alikuwa akizungumzia jambo muhimu sana. Biblia inasema: “Mafarisayo na Masadukayo wakamkaribia na, ili kumjaribu, wakamwomba awaonyeshe ishara kutoka mbinguni. Akajibu, akawaambia: ‘Inapokuwa jioni ninyi huwa na desturi ya kusema, “Kutakuwa na hali nzuri ya hewa, kwa maana anga ni jekundu”; na asubuhi, “Kutakuwa na baridi kali, na mvua leo, kwa maana anga ni jekundu, na lenye mawingu mazito.” Mnajua jinsi ya kufasiri kuonekana kwa anga, lakini ishara za nyakati hamwezi kuzifasiri.’”—Mathayo 16:1-3.

Alipotaja “ishara za nyakati,” Yesu alionyesha kwamba Wayahudi wa karne ya kwanza waliomsikiliza walipaswa kujua umuhimu wa nyakati zao. Mfumo wa Kiyahudi ulikuwa karibu kupatwa na msiba ambao ungewaathiri wote. Siku chache kabla ya kifo chake, Yesu aliwaambia wanafunzi wake kuhusu ishara nyingine, yaani, ishara ya kuwapo kwake. Alichosema wakati huo ni muhimu sana kwa kila mtu leo.