Mambo Makuu Katika Kitabu cha Kwanza cha Mambo ya Nyakati
Neno la Yehova Liko Hai
Mambo Makuu Katika Kitabu cha Kwanza cha Mambo ya Nyakati
MIAKA 77 imepita tangu Wayahudi warudi katika nchi yao kutoka utekwani Babiloni. Hekalu lililojengwa na Gavana Zerubabeli limekuwapo kwa miaka 55 sasa. Sababu kuu iliyowafanya Wayahudi warudi katika nchi yao ni kurudishwa kwa ibada ya kweli huko Yerusalemu. Hata hivyo, watu hawana bidii kwa ajili ya ibada ya Yehova. Wanahitaji kutiwa moyo, nacho Kitabu cha Kwanza cha Mambo ya Nyakati kinatoa msaada huo.
Mbali na rekodi za ukoo, Kitabu cha Kwanza cha Mambo ya Nyakati kinasimulia matukio ya kipindi cha miaka 40 hivi, tangu kifo cha Mfalme Sauli mpaka kifo cha Mfalme Daudi. Inaaminika kwamba kuhani Ezra ndiye aliyeandika kitabu hicho mwaka wa 460 K.W.K. Tunapendezwa na Kitabu cha Kwanza cha Mambo ya Nyakati kwa sababu kinatueleza kuhusu ibada katika hekalu na kinatupa habari zaidi kuhusu ukoo wa Masihi. Kikiwa sehemu ya Neno la Mungu lililoongozwa kwa roho, ujumbe wake unaimarisha imani yetu na kuboresha uelewaji wetu wa Biblia.—Waebrania 4:12.
ORODHA MUHIMU YA MAJINA
Orodha ya majina ya ukoo ambayo Ezra alikusanya ni muhimu kwa angalau sababu tatu: kuhakikisha kwamba ni watu wanaoruhusiwa peke yao ndio wanaotumika wakiwa makuhani, kusaidia kutambua urithi wa kikabila, na kuhifadhi rekodi ya ukoo wa Masihi. Rekodi hiyo ina historia ya Wayahudi kurudi nyuma mpaka kwa mtu wa kwanza. Kuna vizazi kumi kutoka kwa Adamu mpaka kwa Noa, na vingine kumi mpaka kwa Abrahamu. Baada ya kuorodhesha wana wa Ishmaeli, wana wa Ketura suria wa Abrahamu, na wana wa Esau, simulizi hilo linakazia uangalifu ukoo wa wana 12 wa Israeli.—1 Mambo ya Nyakati 2:1.
Wazao wa Yuda wanazungumziwa zaidi kwa sababu ndio wanaotokeza ukoo wa kifalme wa Mfalme Daudi. Kuna vizazi 14 kutoka kwa Abrahamu mpaka kwa Daudi, na vingine 14 mpaka wakati wa kupelekwa uhamishoni huko Babiloni. (1 Mambo ya Nyakati 1:27, 34; 2:1-15; 3:1-17; Mathayo 1:17) Baadaye, Ezra anaorodhesha wazao wa makabila ya upande wa mashariki mwa Yordani, halafu ukoo wa wana wa Lawi. (1 Mambo ya Nyakati 5:1-24; 6:1) Kisha, anazungumzia kwa ufupi baadhi ya makabila mengine yaliyo magharibi mwa Mto Yordani na kuzungumzia ukoo wa Benyamini kwa undani zaidi. (1 Mambo ya Nyakati 8:1) Majina ya wakaaji wa kwanza wa Yerusalemu baada ya utekwa wa Babiloni yameorodheshwa pia.—1 Mambo ya Nyakati 9:1-16.
Maswali ya Kimaandiko Yajibiwa:
1:18—Baba ya Shela alikuwa nani—Kainani au Arpakshadi? (Luka 3:35, 36) Arpakshadi alikuwa baba ya Shela. (Mwanzo 10:24; 11:12) Jina “Kainani” kwenye Luka 3:36 huenda lilitokana na matamshi mabaya ya jina “Wakaldayo.” Ikiwa ndivyo, huenda maandishi ya awali yalisema, “mwana wa Mkaldayo Arpakshadi.” Au huenda ikawa majina Kainani na Arpakshadi yanamrejelea mtu yuleyule. Tusisahau pia kwamba maneno “mwana wa Kainani” hayapatikani katika hati fulani.
2:15—Je, Daudi alikuwa mwana wa saba wa Yese? La. Yese alikuwa na wana wanane, na Daudi ndiye aliyekuwa kitinda-mimba. (1 Samweli 16:10, 11; 17:12) Inaonekana kwamba mwana mmoja wa Yese alikufa bila kuwa na watoto. Kwa sababu mwana huyo hangekuwa muhimu sana katika orodha za kiukoo, Ezra hakuandika jina lake.
3:17—Kwa nini andiko la Luka 3:27 linamrejelea Shealtieli mwana wa Yekonia kuwa mwana wa Neri? Yekonia alikuwa baba ya Shealtieli. Hata hivyo, inaonekana Shealtieli alimwoa binti ya Neri. Luka anamrejelea mwana-mkwe wa Neri kuwa mwana wa Neri kama alivyomwita Yosefu kuwa mwana wa Heli, baba ya Maria.—Luka 3:23.
3:17-19—Zerubabeli, Pedaya, na Shealtieli walikuwa na uhusiano gani? Zerubabeli alikuwa mwana wa Pedaya na Pedaya alikuwa ndugu ya Shealtieli. Hata hivyo, wakati mwingine Biblia inamwita Zerubabeli mwana wa Shealtieli. (Mathayo 1:12; Luka 3:27) Huenda ilikuwa hivyo kwa sababu Pedaya alikufa na Shealtieli akamlea Zerubabeli. Au huenda kwa kuwa Shealtieli alikufa bila mtoto, Pedaya alioa mke wa ndugu yake, na Zerubabeli akawa mtoto wao wa kwanza.—Kumbukumbu la Torati 25:5-10.
5:1, 2—Kupokea haki ya uzaliwa wa kwanza kulimaanisha nini kwa Yosefu? Kulimaanisha kwamba Yosefu alipokea sehemu mbili za urithi. (Kumbukumbu la Torati 21:17) Hivyo, akawa baba ya makabila mawili—Efraimu na Manase. Kila mmoja wa wale wana wengine wa Israeli alitokeza kabila moja tu.
Mambo Tunayojifunza:
1:1–9:44. Ukoo wa watu halisi unathibitisha kwamba mpango wote wa ibada ya kweli unategemea mambo ya hakika wala si hadithi tu.
4:9, 10. Yehova alijibu sala ya Yabesi ya kumsihi apanue eneo lake kwa amani ili liwatoshe watu zaidi wanaomwogopa Mungu. Sisi pia tunahitaji kusali kutoka moyoni ili tupate ongezeko tunapoendelea kushiriki kwa bidii katika kazi ya kufanya wanafunzi.
5:10, 18-22. Katika siku za Mfalme Sauli, makabila yaliyokuwa mashariki ya Yordani yalishinda Wahagri ingawa idadi ya Wahagri ilikuwa zaidi ya mara mbili ya idadi ya makabila hayo. Hiyo ilikuwa kwa sababu wanaume wenye nguvu wa makabila hayo walimtumaini Yehova na wakamwomba msaada. Acheni tuwe na hakika kabisa katika Yehova tunapoendelea na vita vyetu vya kiroho dhidi ya adui zetu walio wengi kuliko sisi.—Waefeso 6:10-17.
9:26, 27. Watunza-malango Walawi walikuwa katika vyeo vya kutegemewa. Walipewa funguo za malango ya sehemu takatifu za hekalu. Walithibitisha kuwa wanategemeka kwa kufungua malango kila siku. Tumepewa daraka la kuwahubiria watu katika eneo letu na kuwasaidia kuwa waabudu wa Yehova. Je, hatupaswi kuwa wenye kutegemeka kama Walawi waliotunza malango?
DAUDI ATAWALA AKIWA MFALME
(1 Mambo ya Nyakati 10:1–29:30)
Masimulizi haya yanaanza kwa kuzungumzia kifo cha Mfalme Sauli na wana wake watatu katika vita dhidi ya Wafilisti kwenye Mlima Gilboa. Daudi mwana wa Yese atawazwa kuwa mfalme wa kabila la Yuda. Wanaume wa vita kutoka katika makabila yote wanakuja Hebroni ili kumfanya kuwa mfalme wa taifa lote la Israeli. (1 Mambo ya Nyakati 11:1-3) Muda mfupi baadaye, anateka Yerusalemu. Baadaye, Waisraeli wanapeleka sanduku la agano Yerusalemu “kwa sauti za shangwe na kwa kupiga baragumu . . . wakipiga kwa sauti kubwa vinanda na vinubi.”—1 Mambo ya Nyakati 15:28.
Daudi anaeleza nia yake ya kumjengea nyumba Mungu wa kweli. Yehova anafanya agano la Ufalme na Daudi lakini anasema kwamba Sulemani ndiye atakayemjengea nyumba. Daudi anapoendelea na kampeni yake dhidi ya adui za Waisraeli, Yehova anampa ushindi mwingi. Kuhesabu watu isivyo halali kunasababisha vifo vya watu 70,000. Baada ya kuambiwa na malaika amjengee Yehova madhabahu, Daudi ananunua uwanja kutoka kwa Ornani Myebusi. Daudi anaanza ‘kufanya matayarisho kwa wingi sana’ kwa ajili ya kumjengea Yehova nyumba “yenye utukufu zaidi” katika uwanja huo. (1 Mambo ya Nyakati 22:5) Daudi anapanga kazi za Walawi zinazozungumziwa sana katika kitabu hiki kuliko mahali pengine popote katika Maandiko. Mfalme na watu wanatoa michango kwa ukarimu kwa ajili ya hekalu. Daudi anakufa baada ya kutawala kwa miaka 40, akiwa “ameshiba siku, utajiri na utukufu; na Sulemani mwana wake [anaanza] kutawala mahali pake.”—1 Mambo ya Nyakati 29:28.
Maswali ya Kimaandiko Yajibiwa:
11:11—Kwa nini hesabu ya wale waliouawa ni 300 wala si 800 kama inavyoonyeshwa katika simulizi la 2 Samweli 23:8? Kichwa cha wanaume watatu wenye nguvu zaidi wa Daudi alikuwa Yashobeamu, au Yosheb-bashebethi. Wale wanaume wengine wawili walikuwa Eleazari na Shamma. (2 Samweli 23:8-11) Huenda masimulizi hayo mawili yanatofautiana kwa sababu yanahusu mambo mbalimbali yaliyofanywa na mtu yuleyule.
11:20, 21—Abishai alikuwa na cheo gani akilinganishwa na wale wanaume watatu wenye nguvu zaidi wa Daudi? Abishai hakuwa mmoja kati ya wale wanaume watatu wenye nguvu zaidi waliomtumikia Daudi. Hata hivyo, andiko la 2 Samweli 23:18, 19, linaonyesha kwamba alikuwa kichwa cha wale mashujaa 30 wa vita na alikuwa mashuhuri kuliko yeyote kati yao. Abishai alikuwa na sifa kama wale wanaume watatu wenye nguvu zaidi kwa sababu alitenda tendo kubwa kama lile la Yashobeamu.
12:8—Nyuso za Wagadi zilikuwaje kama “nyuso za simba”? Wanaume hao mashujaa walimuunga mkono Daudi alipokuwa jangwani. Nywele zao zilikuwa ndefu. Nazo ziliwafanya waonekane wakali kama simba.
13:5—“Mto wa Misri” ni nini? Watu fulani wamefikiri kwamba usemi huo hurejelea kijito cha Mto Nile. Hata hivyo, watu wengi wanaamini kwamba unarejelea “bonde la mto la Misri”—lile bonde refu lililokuwa kwenye mpaka wa kusini-magharibi wa Nchi ya Ahadi.—Hesabu 34:2, 5; Mwanzo 15:18.
16:30—Maneno “maumivu makali” kwa ajili ya Yehova yanamaanisha nini? Katika mstari huu, neno “maumivu” linatumiwa kwa njia ya mfano nalo linamaanisha kumwogopa na kumheshimu sana Yehova.
16:1, 37-40; 21:29, 30; 22:19—Ni mpango gani wa ibada uliokuwapo katika Israeli kuanzia wakati Sanduku lilipopelekwa Yerusalemu mpaka wakati hekalu lilipojengwa? Tayari Sanduku lilikuwa limeondolewa katika maskani miaka mingi kabla ya Daudi kulileta Yerusalemu na kuliweka katika hema alilokuwa amejenga. Baada ya hapo, Sanduku hilo liliendelea kukaa katika hema hilo huko Yerusalemu. Maskani ilikuwa huko Gibeoni, ambako Kuhani Mkuu Sadoki na ndugu zake walikuwa wakitoa dhabihu kulingana na Sheria. Mpango huo uliendelea hadi ujenzi wa hekalu huko Yerusalemu ulipokamilika. Hekalu lilipokamilika, maskani ilitolewa Gibeoni na kuletwa Yerusalemu, nalo Sanduku likawekwa mahali Patakatifu Zaidi pa hekalu.—1 Wafalme 8:4, 6.
Mambo Tunayojifunza:
13:11. Hatupaswi kukasirika na kumlaumu Yehova tunapokosa kufanikiwa, badala yake tunapaswa kuchunguza hali na kujitahidi kutambua kwa nini hatukufanikiwa. Bila shaka Daudi alifanya hivyo. Alijifunza kutokana na makosa yake na baadaye akafanikiwa kulipeleka Sanduku huko Yerusalemu akitumia njia inayofaa. *
14:10, 13-16; 22:17-19. Kila mara tunapaswa kusali kwa Yehova na kumwomba atupe mwongozo wake kabla ya kuchukua hatua yoyote itakayoathiri hali yetu ya kiroho.
16:23-29. Ibada ya Yehova inapaswa kuwa muhimu zaidi maishani mwetu.
18:3. Yehova ni Mtimizaji wa ahadi zake. Alimtumia Daudi kutimiza ahadi yake kwamba angewapa wazao wa Abrahamu nchi yote ya Kanaani, “kutoka mto wa Misri mpaka ule mto mkubwa, mto Efrati.”—Mwanzo 15:18; 1 Mambo ya Nyakati 13:5.
21:13-15. Yehova alimwamuru malaika asimamishe tauni kwa sababu anahuzunika watu Wake wanapoteseka. Bila shaka, “rehema zake ni nyingi.” *
22:5, 9; 29:3-5, 14-16. Ingawa Daudi hakupewa pendeleo la kujenga hekalu la Yehova, bado alionyesha roho ya ukarimu. Kwa nini? Kwa sababu alitambua kwamba vitu vyote alivyokuwa navyo alivipata kutokana na wema wa Yehova. Kutamani kumshukuru Mungu kunapaswa kutuchochee sisi pia tuwe wakarimu.
24:7-18. Mpango ambao Daudi alianzisha wa kuwa na migawanyo 24 ya makuhani ulikuwapo wakati malaika wa Yehova alipomtokea Zekaria, baba ya Yohana Mbatizaji, na kujulisha kwamba Yohana angezaliwa. Wakati huo, Zekaria, aliyekuwa kuhani wa “mgawanyo wa Abiya,” alikuwa katika zamu yake hekaluni. (Luka 1:5, 8, 9) Ibada ya kweli inahusiana na watu halisi walioishi wala si watu wanaotajwa katika hadithi. Tutabarikiwa sana kwa kushirikiana kwa ushikamanifu na “mtumwa mwaminifu na mwenye busara” katika mpango wa ibada ya Yehova leo.—Mathayo 24:45.
Mtumikie Yehova kwa “Nafsi Yenye Shangwe”
Mbali na orodha ya majina, Kitabu cha Kwanza cha Mambo ya Nyakati kina habari nyingine nyingi. Pia kinasimulia jitihada za Daudi za kulileta sanduku la agano Yerusalemu, ushindi wake mbalimbali, matayarisho yake ya kujenga hekalu, na kupanga migawanyo ya makuhani Walawi. Bila shaka, mambo yote ambayo Ezra aliandika katika Kitabu cha Kwanza cha Mambo ya Nyakati yaliwasaidia Waisraeli kuonyesha tena bidii yao kwa ibada ya Yehova katika hekalu.
Daudi aliweka mfano bora kwa kutanguliza ibada ya Yehova maishani mwake. Badala ya kujitafutia mapendeleo ya pekee, Daudi alijitahidi kufanya mapenzi ya Mungu. Tunatiwa moyo kufuata shauri alilotoa, yaani, kumtumikia Yehova “kwa moyo kamili na kwa nafsi yenye shangwe.”—1 Mambo ya Nyakati 28:9.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 2 Kwa habari zaidi kuhusu mambo tunayojifunza kutokana na jitihada ya Daudi ya kulipeleka Sanduku Yerusalemu, ona Mnara wa Mlinzi la Mei 15, 2005, ukurasa wa 16-19.
^ fu. 6 Kwa habari zaidi kuhusu mambo tunayojifunza kutokana na kosa la Daudi la kuwahesabu watu isivyo halali, ona Mnara wa Mlinzi la Mei 15, 2005, ukurasa wa 16-19.
[Chati/Picha katika ukurasa wa 8-11]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Vizazi vinavyonazia kwa Adamu mpaka Noa (miaka 1,056)
4026 K.W.K. Adamu
Miaka 130 ⇩
Sethi
105 ⇩
Enoshi
90 ⇩
Kenani
Mahalaleli
65 ⇩
Jaredi
162 ⇩
Enoko
65 ⇩
Methusela
187 ⇩
Lameki
182 ⇩
2970 K.W.K. NOA azaliwa
Vizazi vinavyoanzia kwa Noa mpaka kwa Abrahamu (miaka 952)
2970 K.W.K. Noa
Miaka 502 ⇩
Shemu
100 ⇩
GHARIKA 2370 K.W.K.
Arpakshadi
35 ⇩
Shela
30 ⇩
Eberi
34 ⇩
Pelegi
30 ⇩
Reu
32 ⇩
Serugi
30 ⇩
Nahori
29 ⇩
Tera
130 ⇩
2018 K.W.K. ABRAHAMU azaliwa
Tangu Abrahamu hadi Daudi: vizazi 14 (miaka 911)
2018 K.W.K. Abrahamu
Miaka 100.
Isaka
60 ⇩
Yakobo
c.88 ⇩
Yuda
⇩
Perezi
⇩
Hezroni
⇩
Ramu
⇩
Aminadabu
⇩
Nahashoni
⇩
Salmoni
⇩
Boazi
⇩
Obedi
⇩
Yese
⇩
1107 K.W.K. DAUDI azaliwa