Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Wema Unazungukwa na Uovu

Wema Unazungukwa na Uovu

Wema Unazungukwa na Uovu

KATIKA ulimwengu wa leo, huenda ikaonekana kwamba ni watu wachache tu walio tayari kujitolea kwa ajili ya wengine. Hata hivyo, bado wengine wanataka “kutenda tofauti,” yaani, kuwatendea wengine mema kwa kadiri fulani. Kila mwaka, watu wengi hutoa mabilioni ya dola kwa mashirika fulani ya kutoa misaada. Kwa mfano, huko Uingereza, dola bilioni 13 za Marekani zilitolewa kwa ajili ya michango ya fadhili katika mwaka wa 2002. Hicho ni kiasi kikubwa zaidi cha pesa kuwahi kutolewa. Tangu mwaka wa 1999, wafadhili kumi wakarimu wametoa au wameahidi kutoa zaidi ya dola bilioni 38 za Marekani ili kuwasaidia maskini.

Baadhi ya kazi nzuri zinazofanywa na wafadhili zinatia ndani kulipa gharama za matibabu kwa ajili ya familia zenye mapato ya chini, kuwaelimisha watoto wa familia za mzazi mmoja, kugharimia miradi ya kutoa chanjo katika nchi zinazoendelea, kuwapa watoto kitabu chao cha kwanza, kutegemeza ufugaji wa wanyama katika nchi maskini na kutoa misaada kwa wanaoathiriwa na misiba ya asili.

Mambo ya hakika yanayotajwa hapo juu yanaonyesha kwamba wanadamu wana uwezo wa kuwatendea wengine mema. Hata hivyo, inasikitisha pia kuona kwamba kuna watu wanaotenda maovu yasiyoelezeka.

Uovu Waongezeka

Tangu mwisho wa Vita vya Pili vya Ulimwengu, kumekuwa na visa 50 hivi vya mauaji ya jamii na mauaji kwa sababu za kisiasa. Jarida moja (American Political Science Review) linasema hivi: “Matukio hayo yameangamiza watu milioni 12 hivi na raia zaidi ya milioni 22, hiyo ikiwa ni zaidi ya watu wote waliouawa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe na vya kimataifa tangu mwaka wa 1945.”

Katika miaka 50 ya mwisho ya karne ya 20, watu wapatao milioni 2.2 waliuawa huko Kambodia kwa sababu za kisiasa. Chuki ya kikabila huko Rwanda ilisababisha vifo vya wanaume, wanawake, na watoto zaidi ya 800,000. Watu zaidi ya 200,000 walikufa huko Bosnia kwa sababu za kidini na za kisiasa.

Akitaja matendo ya uovu ya hivi karibuni, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa alisema hivi katika mwaka wa 2004: “Huko Iraki, watu wanauawa bila huruma, huku wafanyakazi wa kutoa misaada, waandishi wa habari, na raia wengine wakichukuliwa mateka na kuuawa kinyama. Wakati huohuo, tumeona wafungwa huko Iraki wakiteswa kikatili. Huko Darfur, tumeona watu wakilazimika kutoroka makwao, nyumba zao zikiharibiwa, huku wanawake wakilalwa kinguvu. Huko kaskazini mwa Uganda, tumeona watoto wakikatwa-katwa viungo vya mwili na kulazimishwa kushiriki katika matendo ya ukatili. Huko Beslan, tumeona watoto wakichukuliwa mateka na kuuawa kikatili.”

Hata katika nchi zilizoendelea, chuki na matendo ya uhalifu yanaongezeka. Kwa mfano, katika mwaka wa 2004, gazeti moja (Independent News) liliripoti kwamba nchini Uingereza “idadi ya watu walioshambuliwa au kutendewa vibaya kwa sababu ya kuwa wa jamii nyingine iliongezeka kwa mara 11 kuliko ilivyokuwa miaka kumi iliyotangulia.”

Kwa nini wanadamu walio na uwezo wa kutenda mambo mengi mazuri hufanya maovu hayo? Je, uovu utakoma? Kama inavyoonyeshwa katika makala inayofuata, Biblia inatoa majibu yenye kuridhisha kwa maswali hayo yenye kutatanisha.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 2]

COVER: Mark Edwards/Still Pictures/Peter Arnold, Inc.