Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Umaskini Jinsi Hali Ilivyo Leo

Umaskini Jinsi Hali Ilivyo Leo

Umaskini Jinsi Hali Ilivyo Leo

MARA nyingi Vicente * huonekana mitaani akivuta mkokoteni uliojaa mizigo huko São Paulo, nchini Brazili. Yeye hukusanya katoni, vyuma, na plastiki. Giza linapoingia, yeye hutandaza katoni kadhaa chini ya mkokoteni wake na kulala. Akiwa amelala, yeye hasikii kelele za magari wala mabasi yanayopita. Wakati fulani alikuwa ameajiriwa, alikuwa na makao, na alikuwa na familia, lakini alipoteza vitu vyote hivyo. Sasa yeye hupata riziki kwa kufanya kazi mitaani.

Inasikitisha kwamba mamilioni ya watu ulimwenguni pote ni maskini wa kupindukia kama Vicente. Katika nchi zinazoendelea, watu wengi hulazimika kuishi barabarani au vibandani. Mara nyingi wanawake wenye watoto wanaonyonya, vilema, na vipofu huonekana wakiomba-omba. Watoto hukimbia katikati ya magari yaliyosimama kwenye taa za kuelekeza magari huku wakijaribu kuuza peremende na kutumaini kupata angalau pesa kidogo.

Ni vigumu kueleza kwa nini kuna umaskini wa aina hiyo. Gazeti moja la Uingereza (The Economist) lilisema: “Wanadamu hawajawahi kamwe kuwa na ujuzi mwingi wa kitiba na wa kiteknolojia na akili zinazohitajiwa ili kushinda umaskini kama walivyo nao leo.” Bila shaka, watu wengi wamefaidika kutokana na ujuzi huo. Barabara za majiji makubwa katika nchi nyingi zinazoendelea zimejaa magari mapya yenye kuvutia. Maduka makubwa-makubwa yamejaa vifaa vya kisasa ambavyo havikosi wanunuzi. Maduka mawili ya biashara huko Brazili hufanya matangazo ya kuuza vifaa fulani. Mnamo 2004, maduka hayo yalifanya kazi usiku kucha kuanzia Desemba 23 hadi Desemba 24. Mojawapo ya maduka hayo yalikodisha wachezaji wa dansi ili kuwatumbuiza wanunuzi. Jambo hilo liliwavutia wanunuzi 500,000 hivi!

Hata hivyo, watu wengi hawafaidiki kutokana na utajiri wa wengine. Tofauti kubwa iliyoko kati ya matajiri na maskini imewafanya watu wengi kukata kauli kwamba kuna uhitaji wa haraka wa kukomesha umaskini. Gazeti moja la Brazili (Veja) lilisema: “Jambo kuu ambalo viongozi wa ulimwengu wanapaswa kuzungumzia mwaka huu [2005] ni kukomesha umaskini.” Gazeti hilo pia liliripoti kuhusu pendekezo la kuanzisha tena Mradi wa Marshall ili kusaidia nchi maskini zaidi, hasa barani Afrika. * Ingawa mapendekezo kama hayo huonyesha kuna maendeleo, gazeti hilohilo liliongeza hivi: “Kuna sababu nyingi pia za kutilia shaka matokeo ya mapendekezo hayo. Nchi nyingi husita kutoa pesa kwa sababu mara nyingi pesa zinazotolewa hazipewi wale wanaokusudiwa kuzipata.” Inasikitisha kwamba kwa sababu ya ufisadi na njia za kutawala, pesa nyingi zinazotolewa na serikali, mashirika ya kimataifa, na watu mbalimbali, haziwafikii watu wanaozihitaji hasa.

Yesu alijua kwamba umaskini ungekuwa tatizo la muda mrefu. Alisema hivi: “Ninyi mna maskini pamoja nanyi sikuzote.” (Mathayo 26:11) Je, hilo linamaanisha kwamba umaskini utakuwapo daima duniani? Je, chochote chaweza kufanywa ili kuboresha mambo? Wakristo wanaweza kufanya nini ili kuwasaidia maskini?

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 2 Jina limebadilishwa.

^ fu. 5 Mradi wa Marshall ni mradi uliodhaminiwa na serikali ya Marekani ili kusaidia nchi za Ulaya kuboresha uchumi wao baada ya vita vya pili vya ulimwengu.