Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Jitihada Kabambe za Kuwahimiza Watu Wasome Biblia

Jitihada Kabambe za Kuwahimiza Watu Wasome Biblia

Jitihada Kabambe za Kuwahimiza Watu Wasome Biblia

Alisingiziwa na kuabishwa kisha akafia katika nyika zenye baridi kali huko Siberia mashariki. Ni watu wachache sana wanaokumbuka kwamba aliwasaidia sana Wagiriki wenzake kukua kiroho. Mtu huyo ambaye alipuuzwa na wengi aliitwa Seraphim. Kati ya mambo yaliyochangia kifo chake ni jitihada zake kabambe za kuwahimiza watu wasome Biblia.

SERAPHIM aliishi wakati Ugiriki ilipokuwa sehemu ya Milki ya Ottoman. Mwanahistoria wa dini ya Othodoksi ya Ugiriki George Metallinos, alisema kwamba wakati huo “hakukuwa na shule nzuri za kutosha” na “watu wengi [kutia ndani makasisi] hawakuwa na elimu.”

Kulikuwa na tofauti kubwa kati ya Kikoine (Kigiriki cha kawaida) na Kigiriki kilichokuwa kikizungumzwa siku hizo, pamoja na lahaja zake. Tofauti hiyo ilikuwa kubwa sana hivi kwamba watu ambao hawakuwa na elimu hawangeweza tena kuelewa Kikoine kilichotumiwa kuandika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo. Kufuatia mzozo uliozuka, kanisa liliamua kuendeleza Kikoine hicho ambacho hakikuwa kikieleweka.

Katika mazingira hayo, Stephanos Ioannis Pogonatus alizaliwa katika familia maarufu kwenye kisiwa cha Lesbos, Ugiriki, wapata mwaka wa 1670. Wakazi wengi wa kisiwa hicho walikuwa maskini na hawakujua kusoma na kuandika. Stephanos alipata elimu yake ya msingi katika makao ya watawa kwa sababu hakukuwa na shule za kutosha. Akiwa na umri mdogo sana, aliteuliwa kuwa shemasi katika Kanisa Othodoksi la Ugiriki naye akapewa jina Seraphim.

Karibu mwaka wa 1693, hamu ya Seraphim ya kupata ujuzi ilimfanya aende Constantinople (ambako sasa ni Istanbul, Uturuki). Baada ya muda, ujuzi wake ulimfanya kuwa mtu mashuhuri sana nchini Ugiriki. Muda si muda, alitumwa na chama cha kisiri cha kitaifa cha Ugiriki akiwa mjumbe kwa Maliki Peter Mkuu wa Urusi. Safari ya Seraphim ya kwenda Moscow na kurudi ilimwezesha kupitia maeneo mbalimbali ya Ulaya ambako aliona mabadiliko ya kidini na ya kielimu. Mnamo 1698, Seraphim alienda Uingereza na kukutana na watu mashuhuri huko London na Oxford. Alielekezwa kwa Askofu Mkuu wa Canterbury, kiongozi wa Kanisa Anglikana, ambaye baadaye alimsaidia sana Seraphim.

Achapisha Biblia

Akiwa Uingereza, Seraphim alikata kauli kwamba Wagiriki wanahitaji sana tafsiri mpya ya “Agano Jipya” (Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo) iliyo rahisi kueleweka. Akitumia tafsiri ya miaka 100 hivi mapema ya mtawa anayeitwa Maximus, Seraphim alianza kuchapisha tafsiri mpya, isiyo na makosa, na iliyo rahisi kueleweka. Alianza kazi hiyo kwa bidii lakini baada ya muda mfupi, pesa zake zikaisha. Alikuwa na matumaini makubwa wakati Askofu mkuu wa Canterbury alipomwahidi kumpa msaada wa kifedha. Akichochewa na utegemezo huo, Seraphim alinunua karatasi za kuchapa na kufanya mapatano na mchapishaji.

Hata hivyo, pesa hizo zilimwezesha kuchapisha Injili ya Mathayo, Marko, na nusu ya Injili ya Luka tu. Kisha, kwa sababu ya mabadiliko ya kisiasa huko Uingereza, Askofu Mkuu wa Canterbury akaacha kumpa msaada wa kifedha. Seraphim hakukata tamaa bali alitafuta msaada wa wafadhili wenye mali na hivyo akafaulu kuchapisha tafsiri yake mpya katika mwaka wa 1703. Kiasi fulani cha gharama hiyo kililipwa na Shirika la Kueneza Injili Katika Nchi za Kigeni.

Tafsiri ya zamani zaidi yenye mabuku mawili iliyotafsiriwa na Maximus ilikuwa pia na maandishi ya Kigiriki cha awali. Ilikuwa kubwa na nzito. Tafsiri mpya ya Seraphim ilikuwa na maandishi madogo kidogo na ilikuwa na Kigiriki cha kisasa tu, nayo ilikuwa nyembamba na iliuzwa kwa bei rahisi zaidi.

Ubishi Wazuka

“Bila shaka, tafsiri hiyo mpya ilitosheleza uhitaji halisi wa watu,” akasema msomi George Metallinos. “Hata hivyo, Seraphim alitumia nafasi hiyo kushambulia kikundi cha makasisi kilichopinga kutafsiriwa [kwa Biblia].” Makasisi hao walikasirika sana Seraphim alipoandika katika utangulizi wake kwamba alitokeza tafsiri hiyo ‘hasa kwa ajili ya makasisi na wapresbiteri kadhaa ambao hawakuelewa Kikoine. Alifanya hivyo ili kwa msaada wa ile Roho Takatifu Zaidi waweze kusoma na kuelewa maandiko ya awali, na waweze kuwafundisha Wakristo wa kawaida.’ (The Translation of the Bible Into Modern Greek—During the 19th Century) Hivyo, Seraphim akatumbukia katika mzozo wa kutafsiri Biblia uliokuwapo katika Kanisa Othodoksi la Ugiriki.

Upande mmoja kulikuwa na wale waliotambua kwamba ukuzi wa kiroho na kiadili wa watu ulitegemea kuielewa Biblia. Pia walihisi kwamba makasisi walihitaji kuongeza ujuzi wao wenyewe wa Maandiko. Isitoshe, waliounga mkono kutafsiriwa kwa Biblia walisisitiza kwamba kweli za Maandiko zingeweza kutolewa katika lugha yoyote ile.—Ufunuo 7:9.

Waliopinga kutafsiriwa kwa Biblia walitumia kisingizio cha kwamba kuitafsiri Biblia kwa njia yoyote kungepunguza uzito wa ujumbe wake na kuliondolea kanisa mamlaka ya kufasiri na kufundisha. Hata hivyo, wasiwasi wao mkubwa ulikuwa kwamba Waprotestanti walikuwa wakitumia kazi hiyo ya kutafsiri Biblia kulinyang’anya Kanisa Othodoksi la Ugiriki mamlaka. Makasisi wengi walifikiri kwamba walikuwa na wajibu wa kupinga chochote ambacho kingewapendeza Waprotestanti, kutia ndani jitihada za kuifanya Biblia ieleweke kwa watu wa kawaida. Kwa hiyo, kutafsiri Biblia kukawa suala kuu lililozozaniwa na Waprotestanti na Waothodoksi.

Ingawa hakukusudia kuliacha Kanisa Othodoksi, Seraphim aliwakashifu waziwazi makasisi wenzake ambao walionyesha upendeleo na hawakuwa na ujuzi. Katika utangulizi wa tafsiri yake ya “Agano Jipya,” aliandika hivi: “Kila Mkristo anayemwogopa Mungu anahitaji kusoma Biblia Takatifu” ili awe “mwigaji wa Kristo na atii mafundisho [yake].” Seraphim alisisitiza kwamba kuwakataza watu kusoma Maandiko kunatokana na Ibilisi.

Upinzani Mkali

Tafsiri ya Seraphim ilipofika Ugiriki, iliudhi Kanisa Othodoksi la Ugiriki. Tafsiri hiyo ilipigwa marufuku. Nakala kadhaa za tafsiri hiyo ziliteketezwa, na yeyote aliyepatikana nayo au aliyeisoma alifukuzwa kanisani. Askofu Gabriel wa Tatu, alipiga marufuku kusambazwa kwa tafsiri ya Seraphim, akiitaja kuwa isiyo na maana na isiyofaa.

Ingawa Seraphim hakukata tamaa, aliona uhitaji wa kuwa mwangalifu. Licha ya marufuku halali kutoka kwa kanisa, makasisi na waumini kadhaa waliikubali tafsiri yake. Alifaulu sana kusambaza tafsiri hiyo. Lakini adui zake washupavu waliendelea kumpinga.

Kifo cha Seraphim

Mbali na kuunga mkono kusambazwa kwa Biblia, Seraphim alijihusisha na harakati za marekebisho na za kitaifa. Ili kuendeleza harakati hizo, alirudi Moscow wakati wa kiangazi mwaka wa 1704. Akawa rafiki mkubwa wa Peter Mkuu na kwa muda alikuwa profesa katika Chuo cha Russian Royal. Hata hivyo, akihangaikia kile ambacho kingeipata tafsiri yake, Seraphim alirudi Constantinople mnamo mwaka wa 1705.

Katika tafsiri yake iliyochapwa upya mwaka huohuo, Seraphim aliondoa utangulizi hatari uliokuwa katika chapa ya kwanza. Aliongeza utangulizi rahisi uliowahimiza watu waisome Biblia. Tafsiri hiyo ilisambazwa sana wala hakuna rekodi yoyote inayoonyesha kwamba ilipingwa na makasisi.

Hata hivyo, mnamo 1714 kulikuwa na upinzani mkali kutoka kwa Alexander Helladius, msafiri Mgiriki aliyepinga kutafsiriwa kwa Biblia. Katika kitabu chake Status Præsens Ecclesiæ Græcæ (Jinsi Mambo Yalivyo Katika Kanisa la Ugiriki), aliwashambulia vikali watafsiri hao pamoja na tafsiri zao za Biblia. Helladius aliandika sura nzima kuhusu Seraphim, akimwita mwizi, tapeli, mtu asiye na elimu na mlaghai mpotovu. Je, mashtaka hayo yalikuwa ya kweli? Mwandishi Stylianos Bairaktaris, anaeleza maoni ya wasomi wengi anapomtaja Seraphim kuwa ‘mfanyakazi na mwanzilishi mwenye ujuzi’ ambaye alishambuliwa kwa sababu alikuwa na ujuzi mwingi kuliko watu wa wakati wake. Hata hivyo, kitabu cha Helladius kilichangia kifo cha Seraphim.

Watu Hawakumwamini Seraphim

Kufikia wakati ambapo Seraphim alirudi Urusi mwaka wa 1731, Peter Mkuu alikuwa amekufa. Hivyo, Seraphim hakupata ulinzi wowote rasmi. Maliki Anna Ivanovna, aliyetawala wakati huo, alihofia jambo lolote ambalo lingedhoofisha utawala wake. Mnamo Januari 1732, kulikuwa na uvumi huko St. Petersburg kwamba kulikuwa na mpelelezi Mgiriki aliyetenda kinyume cha milki ya Ugiriki. Mshukiwa huyo alikuwa Seraphim. Alikamatwa na kupelekwa katika makao ya watawa huko Nevsky, ili akahojiwe. Katika makao hayo, kulikuwa na kitabu cha Helladius kilichokuwa na mashtaka mbalimbali ya jinai dhidi ya Seraphim. Seraphim alijaribu kujibu mashtaka hayo kupitia makanusho matatu aliyoandika. Alihojiwa kwa miezi mitano hivi. Hata hivyo, ilikuwa vigumu kuondolea mbali mashtaka dhidi ya Seraphim.

Seraphim aliponea kuhukumiwa kifo kwa sababu hakukuwa na ushahidi wa kutosha dhidi yake. Hata hivyo, kwa sababu ya mashtaka ya Helladius, mamlaka ilisita kumwachilia. Seraphim alihukumiwa kifungo cha maisha nchini Siberia. Uamuzi huo ulionyesha kwamba hukumu hiyo ilitegemea mashtaka yaliyoandikwa “katika kitabu kilichochapishwa na Helladius, mwandishi Mgiriki.” Mnamo Julai 1732, Seraphim akafika mashariki mwa Siberia akiwa amefungwa mikatale kisha akafungiwa katika gereza maarufu la Okhotsk.

Miaka mitatu hivi baadaye, Seraphim akafa, akiwa ameachwa na kusahauliwa. Nyakati nyingine, hakutumia hekima kufanya maamuzi, lakini tafsiri yake ni mojawapo ya tafsiri nyingi za Biblia zinazopatikana katika Kigiriki cha kisasa. * Biblia Takatifu—Tafsiri ya Ulimwengu Mpya ni mojawapo ya tafsiri hizo, na inapatikana pia katika lugha nyingine kadhaa. Tunashukuru kama nini kwamba Yehova Mungu amehifadhi Neno lake ili watu kila mahali wawe na nafasi ya “kupata ujuzi sahihi wa kweli!”—1 Timotheo 2:3, 4.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 26 Ona makala “Jitihada za Kutafsiri Biblia Katika Kigiriki cha Kisasa,” katika Mnara wa Mlinzi, wa Novemba 15, 2002, ukurasa wa 26-29.

[Picha katika ukurasa wa 12]

Peter Mkuu

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 10]

Photos: Courtesy American Bible Society