“Pambo la Galilaya”
“Pambo la Galilaya”
KILOMETA 6.5 tu kaskazini-magharibi mwa Nazareti, mji ambamo Yesu alilelewa, kulikuwa na jiji ambalo halitajwi katika vitabu vya Injili. Hata hivyo, Flavio Yosefo, mwanahistoria Myahudi aliliita jiji hilo “pambo la Galilaya.” Hilo lilikuwa jiji la Sefori. Tunajua nini kuhusu jiji hilo?
Baada ya kifo cha Herode Mkuu, katika mwaka wa 1 K.W.K. hivi, wakaaji wa Sefori waliasi dhidi ya Roma, na hivyo jiji lao likaharibiwa. Antipasi, mwana wa Herode, alirithi Galilaya na Peraea naye akachagua mabomoko ya Sefori kuwa jiji lake jipya. Jiji hilo lilijengwa upya kwa mtindo wa majengo ya Wagiriki na Waroma, lakini wakaaji wengi walikuwa Wayahudi. Kulingana na Profesa Richard A. Batey, jiji hilo lilikuwa “kituo cha serikali cha kusimamia Galilaya na Perea,” mpaka wakati Antipasi alipojenga jiji la Tiberio karibu mwaka wa 21 W.K., ili kuwa jiji kuu badala ya Sefori. Huo ulikuwa wakati Yesu alipoishi karibu na jiji hilo.
Profesa James Strange, aliyefanya uchimbaji katika eneo la Sefori, anasema kwamba jiji hilo lilikuwa na hifadhi za nyaraka, za hazina, za silaha, benki, majengo ya umma, na masoko ya kuuza vyombo vya udongo, glasi, vyombo vya chuma, mawe ya thamani, na vyakula vya aina mbalimbali. Kulikuwa na wafumaji na wafanyabiashara wa nguo na maduka ya kuuza vikapu, fanicha, manukato, na vitu vingine. Inakadiriwa kwamba huenda idadi ya watu wakati huo ilikuwa kati ya 8,000 na 12,000.
Je, Yesu alitembelea jiji hilo lenye shughuli nyingi, ambalo lilikuwa umbali wa saa nzima kutoka Nazareti? Vitabu vya Injili havitupi jibu. Hata hivyo, kitabu kimoja (The Anchor Bible Dictionary), kinasema kwamba “njia iliyofaa zaidi kutoka Nazareti hadi Kana ya Galilaya, ilipitia Sefori.” (Yohana 2:1; 4:46) Kilima cha Sefori kinaweza kuonekana kutoka Nazareti, kikiwa karibu meta 120 kutoka bondeni. Watu fulani wanaamini kwamba Yesu alipotoa ule mfano kwamba “jiji haliwezi kufichwa likiwa limesimama juu ya mlima,” huenda alikuwa anafikiria jiji hilo.—Mathayo 5:14.
Baada ya Yerusalemu kuharibiwa mwaka wa 70 W.K., Sefori likawa jiji kuu la Kiyahudi huko Galilaya na baadaye likawa makao makuu ya Sanhedrini, ile mahakama kuu ya Wayahudi. Kwa muda fulani, jiji hilo lilikuwa kituo cha wasomi wa Kiyahudi.
[Ramani/Picha katika ukurasa wa 32]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Bahari ya Galilaya
GALILAYA
Kana
Tiberio
SEFORI
Nazareti
PEREA
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 32]
Pottery: Excavated by Wohl Archaeological Museum, Herodian Quarter, Jewish Quarter. Owned by Company for the Reconstruction of the Jewish Quarter in the Old City of Jerusalem, Ltd