Je, Televisheni Ni Mlezi Bora wa Watoto?
Je, Televisheni Ni Mlezi Bora wa Watoto?
HUENDA ikapendeza wakati mwingine kuwaacha watoto wako wafurahie kutazama televisheni huku ukishughulikia mambo mengine. Lakini hilo linaweza kuwaathirije watoto wako?
Gazeti moja (The New York Times) linasema: “Hata watoto wachanga wanaweza kuathiriwa na habari mbalimbali zinazoonyeshwa kwenye televisheni.” Katika uchunguzi uliofanywa hivi majuzi, watoto wenye umri wa mwaka mmoja walionyeshwa vipindi vifupi vya televisheni ambavyo vilionyesha jinsi mwigizaji fulani wa kike alivyotenda kwa njia mbalimbali kuelekea kifaa cha kuchezea. Gazeti hilo linasema hivi: “Mwigizaji huyo alipoonyesha kwamba anakiogopa kifaa hicho cha kuchezea, watoto waliepuka kucheza nacho, nao walionekana kuwa na wasiwasi, walikunja uso, na hata kulia. Mwigizaji huyo alipoonyesha kwamba anakifurahia, watoto walikubali kucheza nacho.”
Bila shaka, televisheni inaweza kuwaathiri watoto. Je, inaweza kuwa na madhara ya muda mrefu? Daktari Naoki Kataoka, profesa wa magonjwa ya watoto katika Chuo cha Kitiba cha Kawasaki huko Kurashiki, nchini Japani, ameona watoto wengi ambao ni wanyamavu sana na wasio wachangamfu. Wote walikuwa wakitazama televisheni kwa muda mrefu. Mvulana mmoja wa miaka miwili hangeweza kujieleza vizuri, naye hakujua maneno mengi. Alikuwa akitazama video kuanzia asubuhi mpaka jioni kila siku tangu alipokuwa na umri wa mwaka mmoja. Baada ya mama yake kutii shauri la daktari la kucheza naye na kumzuia asitazame video, hatua kwa hatua mvulana huyo aliongeza msamiati wake. Naam, wazazi wanapaswa kutumia wakati pamoja na watoto wao.
Yehova Mungu, Mwanzilishi wa familia, alikazia umuhimu wa kutumia wakati pamoja na watoto. Aliwaambia hivi watu wake zamani: “Uyakazie [maneno ya Mungu] kwa mwana wako na kuyasema unapoketi katika nyumba yako na unapotembea barabarani na unapolala na unapoamka.” (Kumbukumbu la Torati 6:7) Wazazi, wala si televisheni, ndio wanaoweza kuwafundisha watoto wao kwa njia bora kupitia maneno yao na kielelezo chao, “kulingana na njia” inayowafaa.—Methali 22:6.