Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Barabara za Roma Kumbukumbu za Uinjinia wa Kale

Barabara za Roma Kumbukumbu za Uinjinia wa Kale

Barabara za Roma Kumbukumbu za Uinjinia wa Kale

NI KUMBUKUMBU gani ya Waroma iliyo ya pekee sana? Je, ni uwanja wa Colosseum, ambao magofu yake yako Roma? Ikiwa tunazungumza kuhusu ujenzi mbalimbali wa Roma ambao umedumu kwa muda mrefu au umebadili historia, ni lazima tutaje barabara.

Barabara za Roma zilitumiwa kusafirisha bidhaa, majeshi, na vitu vingine. Mtaalamu wa michoro Romolo A. Staccioli anasema kwamba barabara hizo zilitumiwa “kueneza mawazo, sanaa, falsafa na mafundisho ya kidini,” kutia ndani mafundisho ya Kikristo.

Zamani za kale, barabara za Roma zilionwa kuwa kumbukumbu. Kwa karne nyingi, Waroma walijenga mfumo wa barabara wenye urefu wa zaidi ya kilometa 80,000 katika eneo ambalo sasa linamilikiwa na nchi zaidi ya 30.

Via Appia au Njia ya Apio, ndiyo barabara kuu ya kwanza iliyokuwa muhimu. Iliitwa barabara bora na iliunganisha Roma na Brundisium (sasa linaitwa Brindisi), jiji la bandarini lililotumiwa kuingia maeneo ya Mashariki. Barabara hiyo iliitwa kwa jina la Appius Claudius Caecus, ofisa Mroma aliyeanza kuijenga karibu mwaka wa 312 K.W.K. Pia, Roma ilitumia barabara za Via Salaria na Via Flaminia, ambazo zilielekea mashariki kwenye Bahari ya Adriatic, ili kuingia maeneo ya Balkani, Rhine, na Danube. Barabara ya Via Aurelia ilienda kaskazini kuelekea Gaul na Rasi ya Iberia, nayo barabara ya Via Ostiensis ilielekea Ostia, bandari maarufu ya Roma iliyotumiwa kuingia na kutoka Afrika.

Mradi Mkubwa Zaidi wa Ujenzi wa Roma

Barabara zilikuwa muhimu kwa Roma hata kabla ya wakaaji wake kuanza kujenga barabara mpya. Jiji hilo lilijengwa kwenye makutano ya njia upande wa chini wa Mto Tiberi. Kulingana na hati za kale, ili kuboresha barabara zilizokuwepo, Waroma waliiga mbinu za wenyeji wa Carthage. Lakini kwa kweli Waroma waliiga mbinu za ujenzi za Waeturia. Bado kuna mabaki ya barabara hizo. Isitoshe, kabla ya enzi za Roma eneo hilo lilikuwa na njia nyingi zilizotumiwa sana. Huenda zilitumiwa kuwasafirisha wanyama kwenye sehemu mbalimbali zenye malisho. Hata hivyo, haikuwa rahisi kusafiri kwenye njia hizo, kwani zilijaa vumbi wakati wa kiangazi na matope wakati wa mvua. Mara nyingi, Waroma walijenga barabara zao juu ya njia hizo.

Barabara za Roma zilichorwa kwa makini na kujengwa vizuri ili ziwe imara, zifaidi, na zipendeze. Barabara hizo zilielekea moja kwa moja kwenye maeneo mbalimbali bila kuzunguka-zunguka, na ndiyo sababu barabara nyingi zilikuwa zimenyooka. Hata hivyo, barabara hizo zilihitaji kufuata hali ya nchi. Ilipowezekana, katika maeneo yenye vilima na milima, mainjinia wa Roma walijenga barabara zilizopanda kufikia katikati ya miinuko kwenye upande wa mashariki wa mlima. Hivyo, wasafiri waliotumia barabara hizo hawakutatizika sana wakati wa hali mbaya ya hewa.

Waroma walijengaje barabara zao? Walitumia mbinu mbalimbali, lakini vitu vya kale vimefunua mbinu waliyotumia zaidi.

Kwanza, walichora ramani ya barabara. Kazi hiyo ilifanywa na wapimaji wa barabara walioishi wakati huo. Kisha, kazi ngumu sana ya kuchimba ilifanywa na askari wa Roma, wafanyakazi, au watumwa. Mitaro miwili iliyo sambamba ilichimbwa. Nafasi kati ya mitaro hiyo ilikuwa angalau meta 2.4 hivi, lakini kwa kawaida ilikuwa meta 4, na ilikuwa pana zaidi kwenye sehemu zilizopinda. Barabara iliyokamilika ilikuwa na upana wa meta 10, kutia ndani vijia vya miguu. Udongo uliokuwa katikati ya mitaro hiyo miwili uliondolewa na kuacha shimo. Mara tu walipofikia mwamba, walijaza shimo hilo kwa matabaka matatu au manne ya vitu mbalimbali. Kwanza, huenda walitia mawe makubwa au mabaki ya magofu. Kisha, walitia vijiwe au mawe mengine ambayo huenda yaliunganishwa kwa sementi. Halafu, walitia kokoto au mawe yaliyopondwa-pondwa.

Sehemu ya juu ya barabara fulani za Roma ilikuwa na kokoto zilizoshindiliwa. Hata hivyo, barabara za lami ndizo zilizowavutia zaidi watu wa kale. Sehemu ya juu ya barabara hizo ilitengenezwa kwa mawe makubwa, ambayo yalichongwa kutoka kwenye miamba ya eneo hilo. Barabara hizo ziliinuka kidogo katikati ili maji ya mvua yatiririke kwenye mitaro iliyokuwa kando ya barabara. Ujenzi huo uliwezesha kumbukumbu hizo zidumu kwa muda mrefu na baadhi yake zipo leo.

Miaka 900 hivi baada ya Njia ya Apio kujengwa, Procopius, mwanahistoria wa Byzantium alisema barabara hiyo ni ya “ajabu.” Aliandika hivi kuhusu mawe ya juu ya barabara hiyo: “Licha ya muda mrefu kupita na barabara hiyo kutumiwa sana na magari siku baada siku, bado mawe yake hayajabadilika na yangali laini.”

Barabara hizo zingepitaje juu ya vizuizi vya asili, kama vile mito? Njia moja muhimu ni madaraja, na baadhi yake bado yapo, yakithibitisha kwamba Waroma wa kale walikuwa mafundi wa pekee. Haijulikani sana jinsi Waroma walivyojenga barabara za chini ya ardhi, hata hivyo ilikuwa vigumu zaidi ukifikiria vifaa na mbinu za wakati huo. Kichapo kimoja kinasema hivi: “Mainjinia wa Roma . . . walifanya kazi ambayo haijawa na kifani kwa karne nyingi.” Mfano mmoja ni barabara ya Furlo iliyo chini ya ardhi kwenye barabara kuu ya Via Flaminia. Mnamo mwaka wa 78 W.K., baada ya mainjinia kupanga kwa makini, njia ya chini ya ardhi yenye urefu wa meta 40, upana wa meta 5 na kimo cha meta 5, ilichimbwa katikati ya mwamba. Hilo lilikuwa jambo lenye kustaajabisha sana, tukifikiria vifaa vilivyokuwepo wakati huo. Ujenzi wa barabara za aina hiyo ni mojawapo ya maendeleo makubwa zaidi ya wanadamu.

Kusafiri na Kueneza Mawazo

Askari na wafanya biashara, wahubiri na watalii, waigizaji na watu waliopigana na wanyama, wote walitumia barabara hizo. Wale waliosafiri kwa miguu wangetembea umbali wa kilometa 25 hadi 30 kwa siku. Wasafiri wangeweza kujua umbali kwa kutazama nguzo zilizoonyesha umbali. Nguzo hizo za mawe zilikuwa na maumbo mbalimbali, kwa kawaida nguzo za mche-mviringo, ziliwekwa baada ya kila meta 1,480. Na kulingana na vipimo vya Waroma, huo ulikuwa umbali wa maili moja. Pia, kulikuwa na vituo vya kupumzika ambapo wasafiri wangebadili farasi, kununua vyakula, au nyakati nyingine, kulala. Baadhi ya vituo hivyo vilisitawi na kuwa miji midogo.

Muda mfupi kabla ya Ukristo kuanza, Kaisari Agusto alianza mradi wa kutunza barabara. Alichagua maofisa wa kutunza barabara moja au zaidi. Aliamuru nguzo ya dhahabu iliyoitwa miliarium aureum ijengwe katika Baraza Kuu la Roma. Barabara zote za Roma nchini Italia zilikutana kwenye nguzo hiyo yenye maandishi ya shaba nyekundu. Ndiyo sababu kuna msemo huu: “Barabara zote zinaelekea Roma.” Pia, Agusto aliagiza ramani za barabara zote katika milki hiyo zionyeshwe wazi. Inaonekana kwamba barabara hizo zilitosheleza mahitaji na kutimiza viwango vya nyakati hizo.

Wasafiri fulani wa zamani walitumia ramani au miongozo iliyoandikwa ili kurahisisha safari zao. Ramani hizo zilionyesha umbali kati ya vituo mbalimbali na maelezo ya huduma zilizopatikana katika vituo hivyo. Zilikuwa ghali mno, na hivyo si kila mtu angeweza kuzinunua.

Hata hivyo, Wakristo walioeneza injili walipanga na kufunga safari nyingi za mbali. Mtume Paulo, sawa na watu walioishi nyakati zake, alisafiri kwa ukawaida kupitia bahari alipokuwa akienda mashariki, kwa sababu ya upepo uliokuwa ukivuma kuelekea huko. (Matendo 14:25, 26; 20:3; 21:1-3) Katika Bahari ya Mediterania, upepo huo huvuma kutoka magharibi wakati wa kiangazi. Lakini, Paulo aliposafiri kuelekea magharibi, mara nyingi alitumia barabara za Waroma. Alifanya vivyo hivyo alipofunga safari yake ya pili na ya tatu ya umishonari. (Matendo 15:36-41; 16:6-8; 17:1, 10; 18:22, 23; 19:1) * Karibu mwaka wa 59 W.K., Paulo alielekea Roma akitumia Njia ya Apio ili akutane na waamini wenzake kwenye Soko la Apio lenye shughuli nyingi, kilometa 74 kusini mashariki ya Roma. Wengine walimngoja kwenye kituo cha mapumziko cha Mikahawa Mitatu, kilometa 14 karibu na Roma. (Matendo 28:13-15) Karibu mwaka wa 60 W.K., Paulo angeweza kusema kwamba habari njema ilikuwa imehubiriwa “katika ulimwengu wote” wa wakati huo. (Wakolosai 1:6, 23) Mfumo wa barabara hizo ulisaidia kufanya hivyo.

Kwa hiyo, barabara za Roma zimekuwa za pekee na kumbukumbu za kudumu ambazo zimechangia kuenea kwa habari njema ya Ufalme wa Mungu.—Mathayo 24:14.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 18 Tazama ramani kwenye ukurasa wa 33 wa broshua ‘Ona Nchi Nzuri,’ iliyochapishwa na Mashahidi wa Yehova.

[Picha katika ukurasa wa 14]

Nguzo ya Waroma ya kuonyesha umbali

[Picha katika ukurasa wa 15]

Njia ya Apio nje ya jiji la Roma

[Picha katika ukurasa wa 15]

Barabara katika mji wa kale wa Ostia, Italia

[Picha katika ukurasa wa 15]

Alama za magurudumu ya magari ya kale, Austria

[Picha katika ukurasa wa 15]

Sehemu ya barabara ya Roma yenye nguzo za kuonyesha umbali, Jordan

[Picha katika ukurasa wa 16]

Magofu ya makaburi kwenye njia ya Apio nje ya jiji la Roma

[Picha katika ukurasa wa 16]

Barabara ya Furlo iliyo chini ya ardhi kwenye “Via Flaminia”, katika eneo la Marche

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Daraja la Tiberio kwenye barabara kuu ya “Via Emilia” huko Rimini, Italia

[Picha katika ukurasa wa 17]

Paulo alikutana na waamini wenzake kwenye Soko la Apio lenye shughuli nyingi

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]

Far left, Ostia: ©danilo donadoni/Marka/age fotostock; far right, road with mileposts: Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.