Kielelezo Kizuri cha Unyoofu
Kielelezo Kizuri cha Unyoofu
HIVI majuzi Nelma, ambaye anafanya kazi ya kusuka nywele huko Cruzeiro do Sul, Brazili, alikabili jaribu la utimilifu wake wa Kikristo. Mafuriko yalipokumba eneo lao, mmoja wa wateja wake alimpa nguo kadhaa. Nelma alipokuwa akitenganisha nguo hizo, alipata pesa zinazolingana na dola 1,000 (za Marekani) ndani ya mfuko wa suruali moja.
Pesa alizopata zinatoshana na mshahara wake wa miezi saba hivi, naye alihitaji sana pesa. Nyumba yake mwenyewe ilikuwa imeharibiwa na mafuriko, na baba na ndugu zake walipoteza vitu vingi. Pesa hizo zingemwezesha kurekebisha nyumba yake na kusaidia jamaa yake. Hata hivyo, dhamiri ya Nelma ambayo inaongozwa na Biblia haikumruhusu afiche pesa hizo.—Waebrania 13:18.
Mapema siku iliyofuata, alienda kazini kabla ya saa za kazi na kuzungumza na mwanamke mfanyabiashara aliyekuwa amempa zile nguo. Nelma alimshukuru kwa nguo hizo lakini akaongeza kwamba hangeficha kile alichopata ndani ya nguo hizo. Mwanamke huyo alifurahi sana kurudishiwa pesa hizo. Alikuwa amepanga kuzitumia kuwalipa mshahara wafanyakazi wake. “Unyoofu ni sifa ambayo haionyeshwi mara nyingi,” akasema mwanamke huyo mfanyabiashara.
Ni kweli kwamba watu fulani wanaweza kufikiri unyoofu si sifa muhimu. Lakini, unyoofu ni sifa inayothaminiwa sana na watu wanaojitahidi kumpendeza Mungu wa kweli, Yehova. (Waefeso 4:25, 28) “Singeweza kamwe kulala usingizi usiku iwapo ningetenda kwa njia tofauti,” akasema Nelma.