Ushindi Katika Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu
Ushindi Katika Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu
MNAMO Januari 11, 2007 (11/1/2007), Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu huko Strasbourg, Ufaransa, ilitangaza uamuzi wa kauli moja uliounga mkono Mashahidi wa Yehova huko Urusi katika kesi yao dhidi ya Shirikisho la Urusi. Uamuzi huo ulitetea uhuru wa kidini wa Mashahidi wa Yehova na haki yao ya kusikilizwa bila ubaguzi. Acheni tuzungumzie mambo yaliyoongoza kwenye kesi hiyo.
Kutaniko moja la Mashahidi wa Yehova katika jiji la Chelyabinsk, Urusi, ni la viziwi hasa. Kutaniko hilo lilifanyia mikutano katika jengo fulani walilokodi katika chuo cha mazoezi ya ufundi. Jumapili (Siku ya Yenga), Aprili 16, 2000 (16/4/2000), mkutano wao ulivurugwa na bibi-mwenyekiti, au Kamishna, wa Tume ya Haki za Kibinadamu ya eneo hilo akiwa pamoja na polisi wawili wenye vyeo vikubwa, na polisi mwingine mwenye nguo za raia. Kwa sababu ya ubaguzi hasa wa Kamishna huyo, mkutano huo ulivunjwa kwa dai la uwongo lililotungwa kimakusudi. Ilidaiwa kwamba mkutano huo ulifanywa kinyume cha sheria. Kuanzia Mei 1, 2000, mkataba wao wa kukodi jengo hilo ukavunjwa.
Mashahidi wa Yehova walimlalamikia bila mafanikio kiongozi wa mashtaka wa mji wa Chelyabinsk. Katiba ya Urusi na Mkataba wa Kulinda Haki za Kibinadamu na Haki za Msingi unawapa watu uhuru wa ibada na wa kushirikiana. Hivyo, kesi ilipelekwa kwenye mahakama ya wilaya, kisha rufani ikakatwa katika mahakama ya mkoa. Mapema katika Julai 30, 1999, mahakama kuu ilikuwa imeamua katika kesi nyingine kwamba “kulingana na Sheria ya Urusi ya uhuru wa dhamiri na ushirika wa kidini, maneno ‘bila kupingwa’ yanamaanisha kwamba hakuna uhitaji wa kupata kibali au kuomba mamlaka za serikali ruhusa ya kufanya shughuli za kidini katika sehemu zilizoandaliwa [kwa kusudi hilo].” (Mabano ni yao.) Bila kujali uamuzi huo, kesi iliyopelekwa katika mahakama ya wilaya na ya mkoa ilitupiliwa mbali.
Katika Desemba 17, 2001 (17/12/2001), kesi hiyo ilipelekwa mbele ya Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu. Ilisikilizwa Septemba 9, 2004 (9/9/2004). Yafuatayo ni baadhi ya mambo yaliyotajwa katika hukumu ya mwisho iliyotolewa na Mahakama hiyo:
“Mahakama imeona kwamba haki ya uhuru wa kidini ya walalamishi imeingiliwa kwa kuwa, mnamo Aprili 16, 2000, maofisa wa Serikali walivunja mkutano wa kidini wa walalamishi kabla haujakamilika.”
“Hapakuwa na msingi wowote wa kisheria wa kuvunja mkutano wa kidini uliokuwa ukifanyiwa katika jengo lililokodiwa kihalali kwa kusudi hilo.”
“[Mahakama] inaona kwamba kulingana na sheria inayotegemea maamuzi ya Mahakama Kuu ya Urusi, watu hawahitajiwi kupata kibali au kujulisha wenye mamlaka kabla ya kufanya mikutano ya kidini.”
“Kwa hiyo, kifungu cha 9 [uhuru wa kidini] cha Mkataba wa Kulinda Haki za Kibinadamu na Haki za Msingi kilivunjwa wakati Kamishna na wasaidizi wake walipovuruga mkutano wa kidini wa walalamishi mnamo Aprili 16, 2000.”
“Mahakama imeona kwamba mahakama ya wilaya na ya mkoa zilishindwa kutimiza wajibu . . . wa kuhakikisha kwamba wahusika wamesikilizwa ifaavyo na bila ubaguzi. Kifungu cha 6 [haki ya kusikilizwa bila ubaguzi] cha Mkataba wa Kulinda Haki za Kibinadamu na Haki za Msingi kilivunjwa.”
Mashahidi wa Yehova wanamshukuru Mungu kwa kuwapa ushindi katika Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu. (Zaburi 98:1) Uamuzi huo wa Mahakama utakuwa na matokeo makubwa kadiri gani? Joseph K. Grieboski, msimamizi wa Taasisi ya Dini na Sera za Umma anasema: “Huu ni uamuzi mwingine ulio wa maana sana unaohusu uhuru wa kidini katika maeneo yote ya Ulaya, kwa kuwa uamuzi huo utakuwa na matokeo juu ya haki za kidini katika nchi zote zilizo chini ya Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu.”